Bosi mpya Dart na mzigo unaomsubiri

Mkurugenzi Mkuu Dart, Dk Athumani Kihamia. Picha na mtandao

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Dk Athumani Kihamia kuwa Mtendaji Mkuu wa Dart ambaye ni mtaalamu wa uhasibu na usimamizi wa miradi ya maendeleo

Dar es Salaam. Wakati tovuti na Gazeti la Mwananchi vikiendelea kutoa mfululizo wa ripoti maalumu kuhusu changamoto zilizopo katika usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart) Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Dk Athumani Kihamia kuwa mtendaji mkuu wa wakala huo.

Awali, Dart ilikuwa inaongozwa na Dk Edwin Mhede, aliyedumu kwa siku 971 kabla ya uteuzi wake kutenguliwa.

Taarifa ya uteuzi wa Dk Kihamia imetolewa usiku wa Alhamisi, Januari 11, 2024 kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyotiwa saini na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus.

Taarifa hiyo imesema Dk Mhede ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NMB atapangiwa kazi nyingine. Dk Mhede Pia amewahi kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).


Dk Kihamia ni nani?

Kabla ya uteuzi huo, Dk Kihamia ambaye ni mtaalamu wa uhasibu na usimamizi wa miradi ya maendeleo, aliwahi kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha (RAS) pamoja na kushika nyadhifa mbalimbali kama Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Dk Kihamia alidumu katika nafasi ya Mkurugenzi wa NEC kwa siku 457 kabla ya Oktoba mosi, 2019 kutenguliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Dk Wilson Charles.

Kwa mujibu wa mahojiano aliyowahi kufanya na Mwananachi Digital yaliyochapishwa Oktoba 4, 2019, Dk Kihamia amesimamia chaguzi ndogo tisa akiwa Mkurugenzi wa NEC.

“Nikiwa NEC nimesimamia chaguzi (ndogo za ubunge) karibu tisa na kweli nilijitahidi kusimamia misingi ya Katiba na sheria kiasi kwamba malalamiko yalipungua sana kwa sababu tulijielekeza kwenye maeneo ya elimu,” alisema Dk kihamia.

Pia, Dk Kihamia amewahi kuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha na baadaye Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora.


Soma pia: Mfumo wa dijitali mwarobaini Dart -3

Mzigo unaomsubiri Dk Kihama Dart
Dk Kihamia anaingia kuwa Mtendaji Mkuu wa Dart kukiwa na adha ya usafiri na msongamano katika mabasi hayo ambayo hayatoshelezi mahitaji ya wananchi waishio katika Jiji la Dar es Salaam.

“Katika eneo linalonikera ni kusubiri mabasi ya mwendokasi kwa muda mrefu, yaani kuna wakati unakaa hadi saa mbili bila kupata usafiri na mamlaka hazitoi taarifa yoyote,” amesema Josephine Shayo mkazi wa Kimara jijini hapa anayetumia mabasi hayo katika shughuli zake.

“Ikitokea umepata basi, huo msongamano wake nahisi usipokuwa ngangari huwezi kustahimili.”
Mbali na adha hiyo ya ufinyu wa mabasi, Abdulazak Mkwenya amesema kauli mbaya za madereva pia ni changamoto katika usafiri huo.

“Hii ni huduma ya jamii, lakini unakuta watoa huduma wakiwamo madereva wamekuwa na kauli mbaya hasa wanapopitisha vituo watu. Usafiri huu una changamoto sana,” amesema Mkwenya.

Wakati watumiaji wakisema hayo, Ofisa Uhusiano wa Dart, William Gatambi akifanya mahojiano na Mwananchi Digital katika Makala iliyochapishwa Januari 8, 2024 alisema mradi huo umekuwa wa mafanikio ikiwamo kupunguza gharama na muda.

Alisema watu waliokuwa wanatumia wastani wa Sh20,000 za mafuta ya gari (binafsi) kwenda mjini na kurudi, sasa hutumia nauli Sh1,500 na foleni ikipungua saa tatu hadi dakika 45 kufika katikati ya jiji hilo.

Gatambi alifafanua mradi huo kwa miaka saba umekuwa kivutio na nchi 12 zimeutembelea kujifunza. Nchi hizo ni Zambia, Zimbabwe, Uganda, Kenya, Ethiopia, Senegal, Ghana, Rwanda, Angola, Botswana, Nigeria na Liberia.

Kwa mujibu wa Dart, mabasi yaliyopo hivi sasa ni 210, yakiwamo makubwa yanayohudumia wastani wa abiria 160 kila moja na madogo ya abiria 60 kila moja.

Kwa jumla mabasi yote yanakadiriwa kutoa huduma kwa zaidi ya abiria 200,000 kwa siku katika jiji lenye wakazi milioni 5.38.

Januari 8, 2024, akizungumza na Mwananchi Digital kuhusu changamoto za mradi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikaliza Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa amekiri mradi huo kutomfurahisha tangu Septemba mosi, 2023 alipoingia ndani ya ofisi hiyo.

“Hii ni wizara kubwa na ni wizara kama injini ya nchi, ina taasisi nyingine na ni wizara ambayo imetoa mamlaka kwa Serikali za mitaa, wilaya na mikoa na wizara ambayo lazima ifanye jambo ili kamna Taifa tuwe na utulivu.

Wizara hii ikifanya vizuri inaondosha changamoto nyingi, ina taasisi na vitengo vingi. Moja ya taasisi zilizoko chini yangu ni hii inayohusika na mwendokasi, Dart ambayo ndani yake kuna Udart,” alisema

 “Katika maeneo lazima nikiri hii ina changamoto nyingi na nikiri bado hatujazifanyia kazi na ni sehemu ambayo naiangalia kwa jicho la kipekee ili kupata mfumo wa kudumu hasa mabasi ya mwendokasi, urasimu wa uendeshaji ambayo leo tuna mwendeshaji mmoja anayeshirikiana na Serikali.”

Alisema Serikali imejenga miundombinu ili kuweka ufanisi, ni lazima kuwepo na mwendeshaji zaidi ya mmoja tofauti na ilivyo sasa na katika kulifanya hilo linatekelezwa kuna mapendekezo wameyawasilisha kwa Rais Samia Suluhu Hassan, “ambaye ndiye mwenye dhamana ya Tamisemi, akiridhia tutautangaza kwa umma jinsi utakavyokuwa.”

Waziri Mchengerwa alisema miongoni mwa mambo aliyoyakuta alipoingia kwenye ofisini hiyo ni mapendekezo ya Serikali kuingia dhamana kukopa mabasi, “na gharama yake ni kubwa sana, yaani kama Sh1.5 bilioni kwa basi moja, na hii inaingia kwenye deni la Serikali, mimi kama waziri nimekataa.”



Udart yaguswa
Kabla ya uteuzi wa bosi wa Dart, pia Kampuni ya Uendeshaji Usafiri wa Haraka (Udart) nayo uongozi wake ulifanyiwa marekebisho Oktoba 24, 2023 kwa kuteuliwa Giliard Ngewe akichukua nafasi ya John Nguya.

Ngewe alitambulishwa zikiwa zimepita siku 12 tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, aipe siku 12 Kampuni ya Udart, kutengeneza mabasi 70 yaliyoharibika ili kupunguza adha ya usafiri kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.

Oktoba 12 2023, Chalamila alifanya ziara katika kituo cha kupanda mabasi hayo cha Kimara na Mbezi, ikiwa ni siku moja baada ya Mwananachi Digital iripoti changamoto wanazopitia abiria katika kupata huduma ya usafiri huo hasa asubuhi.

Maoni ya wadau mtandaoni