Bosi Jatu aendelea kusota rumande, upelelezi haujakamilika

Mshtakiwa Peter Gasaya ambaye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jatu, akitoka kusikiliza kesi yake ya kujipatia Sh 5.1bilioni kwa njia ya udanganyifu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne
Muktasari:
- Gasaya anakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kujipatia Sh5.1bilioni kwa udanganyifu
Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mawili, likiwemo la kujipatia Sh5.1bilioni kwa njia ya udanganyifu inayomkabili Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya (33), bado unaendelea.
Gasaya anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka katika Saccos ya Jatu kwa madai kuwa fedha hizo atazipanda kwenye kilimo cha mazao ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua kuwa ni uongo.
Wakili wa Serikali, Eva Kassa ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumatatu Agosti 26, 2024 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kujatwa.
Kassa alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini kuwa shauri hilo liliitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi unaendelea.
Hakimu Mhini alikubaliana na upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hadi Septemba 19, 2024 kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo hakuletwa mahakamani hapo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kujipatia kiasi hicho cha fedha pamoja na kutakatisha Sh5.1bilioni katika kesi ya uhujumu uchumi namba 8/2023.
Katika shtaka la kwanza, mshtakiwa anadaiwa, katika ya Januari mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam, kwa udanganyifu alijipatia Sh5.13 bilioni kutoka Saccos ya Jatu.
Pia anadaiwa kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu kutoka Saccos ya Jatu kwa kujipambanua kwamba fedha hiyo ataipanda kwenye kilimo cha mazao, jambo ambalo alijua kuwa sio kweli.
Shtaka la pili ni kutakatisha kiasi hicho cha fedha tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam.
Siku hiyo ya tukio na eneo hilo, mshtakiwa akiwa mtendaji mkuu na mwanzilishi wa Jatu Saccos, alijihusisha na muamala wa Sh5.13 bilioni 9,865,733 kutoka katika akaunti ya Jatu Saccos iliyopo Benki ya NMB tawi la Temeke kwenda katika akaunti ya Jatu PLC liyopo Benki ya NMB tawi la Temeke, wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.