Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bodaboda wanavyoitazama Bajeti ya Serikali, watoa angalizo

Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya waendesha bodaboda na bajaji mkoa wa Dar es Salaam, Said Kagomba, akizungumza na waandishi wa habari

Muktasari:

  • Serikali imependekeza leseni ya uendeshaji wa pikipiki, bajaji na maguta kushushwa kutoka Sh70,000 hadi Sh30,000.

Dar es Salaam. Shirikisho la waendesha bodaboda na bajaji wamepongeza hatua ya kupunguzwa gharama za leseni za pikipiki za biashara huku wakitaka mabadiliko katika upatikanaji wake.

Pendekezo  la kupunguzwa kwa gharama hizo lilitolewa jana Juni 12, 2025 bungeni Dodoma na Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba, wakati akiwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Waziri huyo katika hotuba hiyo  alipendekeza kupunguzwa kwa ada ya leseni ya uendeshaji wa pikipiki, bajaji na guta kutoka Sh70,000 hadi Sh30,000.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Ijumaa Juni 13 2025, Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya waendesha bodaboda na bajaji Mkoa wa Dar es Salaam, Said Kagomba amesema wamefurahi kusikia kilio chao cha muda mrefu kikifikishwa bungeni.

Kutokana na hilo amesema sasa hakutakuwa na sababu ya madereva kukwepa kupata leseni kwa kuwa ilikuwa ni gharama kubwa kwao.

"Hii sekta tunashukuru imeajiri vijana wengi lakini baadhi walikuwa wakikwepa kupata leseni kutokana na gharama, kwani mtu mpaka anajikuta kaipata anatumia si chini ya Sh96, 000.

"Kwani pamoja na leseni anatakiwa alipe tena Sh6,000, GRR Sh20,000 jumla yote Sh96,000, hivyo tunaomba wabunge kama kweli wanatupenda na kutusikiliza wananchi wao walipitishe pendekezo hili kwa kauli moja," amesema

Pia mapendekezo mengine ni kupunguza gharama za usajili wa pikipiki za biashara kutoka Sh340,000 hadi Sh170,000 kwa miaka mitatu na ada husika italipwa wakati wa usajili wa awali pekee.

Akizungumzia kuhusu pendekezo hilo, Kagomba amesema ni jambo jema lakini ni vema ikaangalia katika kushusha kodi wakati zinapoingizwa hapa nchini kwa kuwa gharama hizo zinamuangukia mnunuaji wa mwisho.

"Bodaboda tuliyokuwa tunainunua Sh1.5 milioni sasa inauzwa hadi Sh2.5 milioni huku ile tuliyokuwa tunainunua Sh2 milioni inaenda karibu Sh3 milioni. Wakati bajaji kuna zilizofika hadi Sh10 milioni sawa na bei ya gari aina ya IST na bei hizi hupanda kila mzigo unapoisha na kuletwa  mwingine,” amesema.

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa "Nadhani Serikali iangalie upande huu pia na isiwaachie hawa wanaozileta kutoka nje kujipangia bei kwa kuwa inatuumiza.

Mmoja wa madereva ambaye hakutaka jina lake litajwe ambaye ni dereva wa bodaboda Gongo la Mboto, amesema kuwepo urahisi wa kuzipata hizo leseni kwa kuwa kumekuwa na kuzungushwa wanapofika kuziomba.

"Yaani kiuhalisi leseni za Sh70,000 zinazosemwa hazikuwepo la ukilipa hiyo hela utaambiwa usubiri miezi sita kupata, lakini kama unaitaka kwa haraka hata ndani ya siku tatu utaambiwa utoe si chini ya Sh200,00 hadi Sh210,000 na wengine wamefanya hivyo kwa kutumiwa vishoka wao kwa kuwa huwezi kusubiri miezi sita wakati huna kazi mtaani”

Dereva huyo ameongeza kuwa "Kwa utaratibu huu hata hiyo ya Serikali kupunguza na kufika Sh30, 000 inaweza isiwe na tija kwa madereva, kikubwa hapa kuwepo usimamizi katika kuzipata kwa bei iliyopangwa kwa kuwa huenda tukaenda kuzipata kuanzia Sh250,000 sasa"

Alipoulizwa Kamanda wa Jeshi la  Polisi Kanda Maalumu, Jumanne Muliro kuhusu tuhuma hizo, amesema hazina ukweli wowote kwa kuwa upataji wa leseni kwa sasa upo kidijitali na sio ule wa kukutana na mtu ana kwa ana.

"Huyo mtu kama ana ushahidi aje hapa na  leseni za Sh3 milioni, mie nitamrudishia hela atakazokuwa amelipia kwani hakuna kitu kama hicho," amesema Muliro.

Naye Jerome Felix, dereva wa bodaboda wa  Kijichi, amesema sababu ya madereva wengi kukwepa kupata leseni baadhi yao wanatumia za magari walizonazo.

"Watu wanatumia leseni za gari walizo nazo wakiamini kwa kuwa wameshazijua sheria za usalama barabarani wakati ukweli wanatakiwa wapate na ya pikipiki na hii hata ukikutana na trafiki ukimuonyesha hiyo hakusumbui kama ambaye hana kabisa leseni," amesema.