Bodaboda wafunguka kauli ya Rais Samia

Muktasari:
Baadhi ya madereva wa bodaboda na bajaji wamesema, vitendo vya kihalifu ikiwemo ujambazi wanavyohusishwa navyo vinatokana na baadhi yao kutokuwa waaminifu na kupelekea kuharibu taswira ya ajira hiyo.
Dar es Salaam. Baadhi ya madereva wa bodaboda na bajaji wamesema, vitendo vya kihalifu ikiwemo ujambazi wanavyohusishwa navyo vinatokana na baadhi yao kutokuwa waaminifu na kusababisha kuharibu taswira ya ajira hiyo.
Madereva hao wametoa kauli hiyo leo Jumatatu Julai 25, 2022 ikiwa ni siku moja tangu Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, kuwaonya kutumika katika vitendo vya ujambazi.
Rais Samia aliwaonya madereva hao jana Jumapili katika kongamano la kuimarisha ushiriki katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Alisema baadhi ya madereva wa bodaboda wamekuwa wakikwapua mizigo ya watu, hasa pochi za wanawake.
Wakizungumza na Mwananchi Digital jijini Dar es Salaam, baadhi ya madereva wamekiri kuwepo kwa matukio hayo na kueleza baadhi ya wasiokuwa waaminifu wamekuwa wakiharibu taswira ya ajira hiyo.
Saidi Omary, mkazi wa Mwananyamala amesema ni kweli wapo baadhi ya madereva sio waaminifu, ambapo wamekuwa wakijaribu kuwabaini na kuwachukulia hatua, ikiwemo kuwafukuza kwenye vituo vyao.
“Suala la wizi au uporaji ni tabia ya mtu, wakati mwingine mtu sio bodaboda lakini wakati anafanya tukio hilo anakuwa kwenye pikipiki, hapo lazima lawama zije kwetu,” amesema Omary.
Dereva bodaboda, Msafiri Kambi amesema matukio yanayofanyika na kuhusishwa na bodaboda, ni ya kweli matukio lakini mara nyingi hufanywa na watu wanaochukulia kazi hiyo kama sio sehemu ya ajira.
Amesema kwa watu walio waaminifu wamefanya hiyo ndio sehemu ya ajira na matukio mengi yamekuwa ya kifanywa na wale wanaoona vijiwe vya bodaboda ni kama sehemu ya kupiga stori au kupotezea muda ili mradi siku iishe.
“Kuna watu wanaitwa vishandu, hawa sio wote sio bodaboda wakati mwingine wamekuwa wakijificha nyuma ya mgongo wetu, na ndio wanaotuharibia na wakati mwingine mtu anaweza kuazima pikipiki lakini usijue lengo lake,” amesema Kambi.
Amebainisha upo umri ambao kwao wanaona ni shida, kuna kundi la vijana wadogo linalochipukia wakati mwingine wanakua wameacha shule, mtu mzima mwenye familia hawezi kujihusisha na matukio hayo.
Anasterzia Mmasi ambaye ni abiria amesema huwa wanapata wakati mgunu kukodi bodaboda kwa kuwa ni vigumu kujua nani aliyemuaminifu na nani sio muaminifu.
“Ni kweli binfsi huwa naogopa sana bodaboda, huwa tunaoa watu wanavyoporwa mikoba wakati mwingine simu, huwa tunapata shida kujua nani mzuri na yupi ni adui kutokana na matukio yao,” amesema Mmasi.