Biteko awapa mambo manne wanamichezo wa Shimiwi

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko (wa pili kushoto) akifungua michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za serikalini inayoendelea kufanyika katika viwanja mbalimbali mkoni Iringa.
Muktasari:
- Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko amewafunda mambo manne wanamichezo wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) wakati akifungua michuano hiyo, katika Manispaa ya Iringa.
Iringa. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko amesema michezo sehemu za kazi ni afya na kuwafunda wanachichezo wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) mambo matatu wakati akifungua michuano hiyo.
Kwa mwaka huu 2023, Michuano ya Shimiwi iliyokusanya wanamichezo zaidi ya 20500 inafanyika katika viwanja mbalimbali ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.
Akizungumza na wanamichezo hao leo Oktoba 4 Biteko amewataka kuendeleza mikakati ya michezo kazini, kuepuka rushwa na ubadhilifu wa mali za umma, kuitangaza Tanzania kupitia sekta ya utalii sambamba na kuwa makini na maambukizi ya Ukimwi.
Amesema watumizi wa umma wanapaswa kuendeleza suala la michezo kazini kwa sababu licha ya kuwa ni afya inasaidia kujenga mahusiano na kuwaagiza wakuu wa maeneo hayo kutowazuia wanamichezo waliopo.
Biteko amesema wanamichezo hao wanapaswa kutumia nafasi hiyo kuwa mawakili wa mazingira ili kupambana na uharibifu sambamba na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kuendelea kuitangaza Tanzania kupitia sekta ya utalii.
“Nimeambiwa mkiwa hapa mtapata nafasi ya kwenda kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ni matumaini yangu mtaenda wote na mkirudi kazini bado mtakuja Iringa kutembelea maeneo ya utalii. Shirikini utalii wa ndani,” amesema.
Awali, Mwenyekiti wa Shimiwi, Daniel Mwalusamba alisema wanamichezo wengi wamejitokeza kushiriki kwenye michezo hiyo jambo ambalo limeonyesha kuwepo kwa muamko mkubwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amesema uwepo wa wanamichezo hao katikati ya Manispaa ya Iringa umeongeza fursa kwa wakazi wake.
“Tumewapokea wageni hawa, wanaishi, kula na kulala kwenye Mkoa wetu jambo hili limekuwa fursa kubwa kwa watoa huduma wa mkoa wa Iringa. Michezo ni uchumi,” amesema.