Biteko atembelea Mtera, akutana na upungufu wa maji

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko akizungumza baada ya kutembelea Bwawa la Mtera ambako amekutana na upungufu wa maji
Muktasari:
- Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ametembelea kituo cha kuzalisha umeme katika Bwawa la Mtera na kukutana na upungufu wa maji.
Iringa. Licha ya kukutana na upungufu wa maji katika bwawa la Kuzalisha umeme la Mtera, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko amesema wanafanya kila jitihada kuhakikisha wanapambana na adha ya upungufu wa umeme nchini.
Hata hivyo amesema unahitajika mkakati kabambe wa kutunza mazingira ili kuokoa vyanzo vya maji vinavyosaidia mabwawa yanayozalisha umeme yasiwe na upungufu.
Biteko amesema hayo leo Jumanne Oktoba 3, 2023 baada ya kutembelea chanzo cha kuzalisha umeme katika bwawa la Mtera na kukutana na upungufu wa maji.
Amesema upungufu huo ndio uliosababisha changamoto ya umeme ambayo inashughulikiwa kwa kutumia vyanzo vingine ikiwemo gesi.
"Kazi yetu sisi Wizara ya Nishati ni kuwaondolea wananchi adha ya umeme, sisi tunafanya kila tunachofanya kuhakikisha tunatumia vyanzo vingine vya kuzalisha umeme," amesema Biteko.
Amewataka wananchi kutunza vyanzo vya maji kwa kuacha uharibifu wa mazingira upungufu wa maji.
Pia amesema lazima idara zinazohusika na mazingira kuungana na kuja na mikakati itakayo okoa vyanzo vya maji.
"Vinginevyo hata hii mitambo tunayonunua haitakuwa na maana kama tutaendelea kuharibu vyanzo vya maji," amesema Biteko.
Pia amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kujenga utaratibu wa kukarabati mitambo yake ili waweze kuepuka adha ya kuharibika.