Biteko aanza utekelezaji agizo la Majaliwa

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akiongoza kikao cha kujadili mikakati ya upatikanaji wa mafuta nchini.
Muktasari:
- Wakati kwa kipindi cha zaidi ya miezi miwili Tanzania iimekuwa ikishuhudia uhaba wa mafuta ya petroli na dizeli katika baadhi ya mikoa, Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko amekutana na kamati ya wataalam wanaondaa mikakati ya upatikanaji wa nishati hiyo nchini.
Dodoma. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko leo Jumatatu Septemba 11, 2023 ameongoza kikao cha kujadili mikakati ya upatikanaji wa mafuta ya petroli nchini.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba na watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Wengine walioshiriki ni Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) pamoja na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa pamoja (PBPA).
Kikao hicho kinakuja siku chache baada ya agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kumtaka, Dk Biteko kukaa na wadau wa mafuta ili kushughulikia upatikanaji wa nishati hiyo ndani ya siku saba.
Majaliwa alitoa agizo hilo, Septemba 7, 2023, wakati akijibu swali la Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi aliyehoji Serikali inaweka mkakati gani wa kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unakuwa mzuri nchini.
Akijibu Majaliwa amesema Dk Biteko alishaanza kulishughulikia kwa kukaa na wadau mbalimbali lakini akamtaka kuendelea kulishughulikia hilo ndani ya wiki moja ili wawe na majibu.
Amesema pia wapanue wigo wa waagizaji wa mafuta ili wawe na mafuta ya kutosha na kwamba suala la bei wataliangalia huko mbeleni.