Binti afariki kwa kupigwa radi Ludewa

Muktasari:
- Binti Calister Haule (15) amefariki dunia baada ya kupigwa na radi wakati akichunga mbuzi katika Kijiji cha Lifua wilayani Ludewa Mkoa wa Njombe.
Ludewa. Binti Calister Haule (15) amefariki dunia baada ya kupigwa na radi wakati akichunga mbuzi katika Kijiji cha Lifua wilayani Ludewa Mkoa wa Njombe.
Shuhuda wa tukio hilo, Alen Ngatunga amesema binti huyo alikwenda kufungua mbuzi kabla ya mvua kuanza.
“Huyu binti alikwenda kufungua mbuzi kabla ya mvua kuanza ila hata baada ya kufungua hakurudi, mama yake aliporudi kutoka shambani na kumuulizia ndipo wakaenda kumtafuta, bahati nzuri mdogo wa marehemu alimwona dada yake amelala chini na mbuzi nazo zimelala chini zikiwa zimeshakufa,” amesema Ngatunga.
Kwa upande wake baba mzazi wa marehemu, Logato Haule amesema mwanaye alifariki Desemba 17, 2022.
Haule amesema kuwa alipata taarifa ya tukio hilo na alipofika kwenye eneo la tukio alikuta mbuzi watatu wamekufa huku mwili wa mwanaye ukiwa umeshachukuliwa na kuingizwa ndani.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Desemba 20, 2022, Diwani wa kata ya Luilo, Mathei Kongo amesema kuwa mvua zinazoendelea kunyesha katika eneo hilo zimesababisha athari mbalimbali ikiwamo uharibifu wa nyumba 16.
Mbunge wa Ludewa, Joseph Kamonga ambaye alifika nyumbani kwa familia hiyo alisema, “Nilipokea simu za taarifa hii ya msiba hivyo nikaona nije kuungana nanyi ndugu zangu kwanza kuwapa pole, kuwafariji lakini vilevile kushirikiana nanyi kumwombea mtoto wetu,” amesema Kamonga.