Bima ya afya kwa wote kusaidia wananchi kutibiwa popote

Muktasari:
- Upatikanaji wa bima ya afya kwa wote, kutatoa fursa kwa watu wenye hali zote kiuchumi, kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu katika hospitali yotote nchini ikiwemo za kibingwa.
Moshi. Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali Maalumu ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto, Dk Leonard Subi amesema upatikanaji wa bima ya afya kwa wote, kutatoa fursa kwa watu wenye hali zote kiuchumi, kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu katika hospitali yotote nchini ikiwemo za kibingwa.
Ameyasema hayo mjini Moshi, wakati akitoa elimu ya bima ya afya kwa wote, kwa kundi la watoa huduma za afya, ambapo amesema bima itamuwezesha kila mwananchi kuwa na uhakika wa matibabu kwa wakati wowote atakapougua.
Amesema gharama za matibabu kwa sasa ni kubwa na zinazidi kupanda huku teknolojia nayo ikizidi kuwa kubwa hivyo kuna umuhimu mkubwa wa bima ya afya kwa wote, ili kuwezesha huduma bora na kwa wakati kwa watu wote wanapougua.
Aidha amesema baada ya muswada wa bima ya afya kwa wote kupitishwa na kuwa sheria, moja ya mambo yatakayozingatiwa ni muda wa matibabu, upatikanaji wa dawa, upatikanaji wa vipimo, lugha safi na huduma nzuri na bora kwa wagonjwa wote bila ubaguzi.
“Gharama za matibabu ni kubwa na zinazidi kupanda na teknolojia inazidi kuwa kubwa, hivyo basi kwa Mtanzania wa kawaida bila bima ya afya maisha yake yanakuwa ya shida hasa anapougua. Sasa Serikali imeona ni muda mwafaka kwa Watanzania wote kuwa na bima ya afya ili wote wawe na uhakika wa kupata matibabu wanapougua”
“Bima hii mgonjwa anaweza kupata matibabu mahala popote na serikali itahakikisha zinapatikana huduma bora na zenye uhakika. Kupitia bima hii watu wote watapata huduma zote muhimu za msingi na kwa haki na hii itaondoa ile changamoto ya watu kuomba michango ya gharama za matibabu pindi wanapougua,” amesema.
Ameongeza kuwa, “ Pia kwa mwananchi mwenye bima ya afya, atapata uhuru mzuri wa kupata huduma za matibabu na tutakuwa na sehemu ya kushughulikia malalamiko ya wananchi vilevile kitengo cha udhibiti wa ubora ndani ya Wizara ya Afya kitaimarishwa na ufuatiliaji wa huduma za afya.”
Akizungumza MganMfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi, Dk Edna-Joy Munisi amesema elimu hiyo inalenga kuwezesha wataalamu wote wa afya kuwa na uelewa sawa juu ya bima ya afya kwa wote, ili kuweza kuielimisha jamii na wananchi na kila mmoja awe na uelewa sahihi.
“Iwapo muswada wa bima ya afya kwa wote utawasilishwa bungeni na kutapitishwa utakuwa sheria hivyo tunahitaji wote tuwe na uelewa sawa ili utakapopitishwa uweze kutekelezwa kikamilifu kwani wote tunatambua umuhimu wa afya na tunahitaji wote tutambue umuhimu wa bima ya afya ili mtu anapougua maradhi mbalimbali apate wepesi wa kupata matibabu”.