Bilioni 800 kuboresha barabara za vijijini

Muktasari:
- Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imesema kukamilika kwa ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 535 katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao.
Dodoma. Serikali imetaja vigezo vitano vilivyotumika kuchagua wilaya sita zitakazonufaika na Mradi wa Uboreshaji wa Barabara za Vijijini kwa Ushirikishaji Jamii na Ufunguaji wa Fursa za Jamii na Kiuchumi (RISE), utakaogharimu Sh800 bilioni.
Vigezo hivyo ni idadi ya watu watakaonufaika, idadi ya vyombo vya moto, uzalishaji wa mazao, muunganiko na barabara kuu na mikoa pamoja na huduma za kijamii.
Barabara hizo zinakwenda kujengwa katika Wilaya za Mbogwe (Geita), Ruangwa (Lindi), Handeni (Tanga), Iringa, Mufindi na Kilolo (Iringa).
Hayo yamo katika taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Oktoba 6, 2023 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Tawala za Mitaa (TAMISEMI), Nteghenjwa Hosseah.

Amesema huo wa Rise utagharimu Sh800 bilioni, Sh690 bilioni ni mkopo wa mashrti nafuu kutoka Benki ya Dunia na Sh115 bilioni ni mchango wa Serikali.
Amesema mradi huo una vipengele vitano ambavyo ni ujenzi na ukarabati wa barabara vijijini, umimarishaji wa taasisi na raslimali watu.
Vipengele vingine ni uhusishwaji, ushirikishwaji na ulinzi wa jamii pamoja na usimamizi wa mradi, ufuatiliaji na tathimini.
Nyingine ni ushughulikiaji matukio ya dharura na majanga ya asili.
Amesema ujenzi wa barabara katika wilaya hizo sita umetengewa Sh554 bilioni na kwamba ulianza Novemba 16 mwaka juzi na unatarajiwa kukamilika Juni 30, mwaka 2027.
“Wilaya hizi ni miongoni mwa wilaya zenye uzalishaji mkubwa wa mazao pamoja na ardhi yenye uwezo wa kuzalisha mazao mengi kwa mujibu wa orodha iliyotolewa na Wizara ya Kilimo,”amesema Nteghenjwa.
Amesema uchaguzi wa wilaya hizo ulizingatia idadi ya walengwa kwenye bidhaa za kipaumbele katika mnyororo wa thamani kikanda kama ilivyopendekezwa katika program ya kuendeleza Sekta ya Kilimo ya Awamu ya Pili (ASDP II).