Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bibi asimulia mjukuu wake alivyouawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni

Picha ya marehemu, Elivia Eliud binti aliyeuawa kwa kuchinjwa Jumatano Aprili 2, 2025 Kimara Temboni Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Binti wa miaka mitano aitwaye Elivia Eliud aliyekuwa anasoma darasa la kwanza Shule ya Msingi Saranga amedaiwa kuchinjwa jana Jumatano ya Aprili 2, 2025.

Dar es Saaam. “Ilikuwa jana Jumatano ya Aprili 2, 2025 saa 10 jioni mjukuu wangu alipokatishwa uhai na mtoto wa mpangaji wangu. Tukio hili siwezi kulisahau mjukuu wangu ameenda.”

Sauti ya majonzi ya Davina Hubaizi bibi wa miaka 50 mkazi wa Mtaa wa Upendo, Kata ya Saranga Kimara Temboni Wilaya Ubungo mkoani Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu kuhusu tukio hilo.

Akisimulia ilivyokuwa anasema mjukuu wake huyo ambaye ni marehemu kwa sasa aitwaye Elivia Eliud mwenye umri wa miaka mitano, hadi mchana alikuwa na mtuhumiwa (jina linahifadhiwa).

“(Anataja jina la mtuhumiwa) alikuwa na mjukuu wangu kwenye chumba anachoishi huyo binti na nilikuwa nikimtafuta kwa kuwa muda wa kula ulikuwa umefika, lakini sikuwa namuona mjukuu wangu nikimuuliza ananiambia nisiwe na wasiwasi mjukuu wako nipo naye.”

“Kwani una wasiwasi na mimi bibi Elivia niko naye na ameshakula. Lakini roho yangu ilikuwa inakataa. Nikaenda kwenye hicho chumba nikagonga hafungui napiga simu hapokei nikazidi kupata wasiwasi,” anasimulia.

Anasema akamuita mama wa mtuhumiwa wa mauaji kwa ajili ya kumsaidia alivyofungua mlango tukakuta mjukuu wangu ameshachinjwa amelala kitandani huku mtuhumiwa akiwa ameshakimbia.

Anadai baada ya kutekeleza mauaji hayo binti huyo (anamtaja jina) mwenye umri kati ya miaka 18 na 19 alikimbia kwenda kituo cha Polisi Kimara kutoa taarifa ya kufanya mauaji hayo.

“Alivyoenda akasema nimeua nimechinja kisha polisi wakaja naye hadi hapa wakiwa wamemfunga pingu,” anasimulia.

Anasema hakuwa na wasiwasi kwa kuwa ameshakaa na mpangaji huyo kwa muda mrefu pamoja na mama yake.

Akielezea maisha yao anasema amekaa na mjukuu wake huyo ambaye ni marehemu tangu akiwa na umri wa miezi minne alipoachiwa na mama yake.

“Sijui kapata pepo gani la kumfanyia hivi mjukuu wangu kwani siku zote amekuwa akishinda nao wajukuu zangu maana wapo wawili,” anaelezea.

Anasema hajawahi kugombana naye hata siku moja alikuwa kama mtoto wa nyumbani, lakini siku ya tukio alichukua kisu sehemu wanapouza chipsi jirani na wanapoishi.

Jirani na mjumbe mstaafu wa eneo hilo, Ally Ngalakani anasema alisikia kelele za bibi huyo zilizomshtua na kwenda ili  kuangalia nini kimetokea.

“Nikainuka kwa haraka kuja kujua kuna nini nikakuta mtoto Elivia ambaye tumezoea kumuita (Koku) kachinjwa na kisu kipo pembeni kwa kweli nilishtuka sana,” anasimulia.

Anasema Koku amezoea kupita nyumbani akiwa anaenda shuleni na lazima aniite “Babu shikamoo babu shikamoo,” walinizoea kama babu yao.

“Tulipoingia ndani ya chumba hicho tukakuta mtoto amelala chali amekatwa koromeo amemchinja vibaya sana,” anasema.

Baada ya kuingia ndani ya chumba hicho na kukuta mwili wa marehemu ndipo wakaona mtuhumiwa amekuja na polisi maana alijipeleka kituo cha polisi.

“Kwa ninavyomjua huyu binti aliyetekeleza mauaji hajawahi kulewa wala kuwa mkorofi ni mpole kama anatumia vilevi au bangi pengine alikuwa akifanya kwa kujificha,” anasema.

Anasema tukio hilo sio la kawaida na anasema hadi sasa mwili wa marehemu upo Hospitali ya Mloganzila na baba wa marehemu anaishi Mbeya ambaye kwa sasa anafanya utaratibu wa kufika Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Upendo, Said Masawe amethibitisha kutokea kwa tukio hilo hapo jana ni tukio la kwanza kutokea katika eneo hilo.

“Ni mara yangu ya kwanza kuona tukio hili tangu nimeingia madarakani limenisikitisha na wananchi wote kwa ujumla.

“Ombi langu kwa wananchi na Watanzania wenzangu tuchunge familia zetu watoto wetu tufanye ibada kuepusha matukio ya namna hii,’ anasema mwenyekiti huyo.

Mariam Zaharani ambaye ni jirani wa marehemu anasema alishtushwa na taarifa za tukio hilo ambalo ni mara yake ya kwanza kushuhudia.

“Tukio hili linatisha na linasikitisha sana tuwe makini kwenye malezi na tuwachunge watoto wetu. Mungu atusaidie katika malezi maana mtoto wako anaweza akatenda au akatendewa,” anasisitiza Mariam.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema ni kweli tukio hilo limetokea na baadaye mtuhumiwa akajisalimisha kituo cha Polisi na sasa hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa.

"Mtuhumiwa tayari tumemkamata baada ya kujileta na sasa hatua  zaidi za kisheria zinaendelea," amesema Muliro.

Amesema masuala kama hayo yanapaswa kushirikiana kati ya jeshi la polisi na taasisi nyingine zikiwamo za  ustawi wa jamii na dini kwa ajili ya kuelimisha umma pamoja na kusaidia watu kisaikolojia.