Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bibi afa maji akiosha vyombo kando ya mto Ruvu

Muktasari:

  • Mtu wa kwanza kushuhudia bibi huyo akizama kwenye mto huo ni mjukuu wake wa kiume mwenye ulemavu wa kuongea (bubu), aliyekuwa akiwaonyesha watu kwa ishara kuwa bibi yake kazama lakini hawakumuelewa.

Morogoro. Mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Tatu Hamis (51) mkazi wa Kijiji cha Kibangile Tarafa ya Matombo wilayani Morogoro vijijini, amezama katika Mto Ruvu alikokwenda kuosha vyombo na kufariki dunia.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumapili Aprili 13, 2025 kuhusiana na tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro,  Mrakibu Shabani Marugujo amesema walipokea taarifa za kuzama maji kwa Tatu  Ijumaa Aprili 11, 2025.

Amesema walienda eneo la tukio wakiwa na vifaa vya uokozi kumtafuta lakini walishindwa kumpata.

“Askari wetu wakishirikiana na wananchi walifika eneo hilo na kuanza kumsaka bibi huyo kwa kutumia boti lakini hadi giza linaingia hawakufanikiwa kumpata," amesema Kamanda Marugujo.

Amesema kazi ya kumtafuta bibi huyo iliendelea tena jana lakini pia hawakufanikiwa.

“Lakini jana hiyo wakati kazi ya utafutaji ikiendelea, wachimba madini waliokuwa wakisafisha kando ya mto huo walidai kuuona mwili huo ukielea na wakatoa taarifa kwa Serikali ya kijiji, hivyo walikwenda kuuopoa na kuukabidhi kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za maziko,” amesema kamanda huyo.

Kufuatia tukio hilo Kamanda Marugujo ametoa tahadhari kwa wananchi wanaotumia mito, mabwawa na maeneo mengine yenye maji kwa shughuli mbalimbali, kuchukua tahadhari hasa katika kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha.

Awali, Mwenyekiti wa kitongoji cha Vizi, Juma Rashid amesema tukio hilo ni la pili kwa watu kuzama na kufa katika mto huo .

Amesema tukio la kwanza lilitokea mwaka jana baada ya mwanamke mmoja kuuliwa na mamba alipokwenda kufua nguo kwenye mto huo.

"Hili tukio la pili mpaka sasa tunashindwa kujua kama mwanamke huyo alikamatwa na mamba au alizama mwenyewe, mara kadhaa hapa kijijini kumekuwa na matukio ya watu kujeruhiwa na mamba huko mtoni," amesema Rashid.

Akisimulia namna tukio hilo lilivyotokea, Rashid amesema mwanamke huyo akiwa na mjukuu wake ambaye ni mlemavu wa kuzungumza (bubu), Ashraf Idrisa alikwenda kuosha vyombo mtoni.

“Mara tukamuona anakimbia anarudi nyumbani huku akionesha ishara ya kuomba msaada kwa watu aliokuwa anakutana nao njiani kuwa wamsaidie kumuokoa bibi yake amezama mtoni,” amesema na kuongeza;

"Huyu mtoto hawezi kuongea lakini aliweza kuonesha ishara mahali alipozama bibi yake, na cha kusikitisha huyo bibi alikuwa akilea mtoto mchanga ambaye ni mjukuu wake, mama wa huyo mtoto alifariki mwaka jana, hivyo amefariki na kuacha wajukuu wawili ambao ni yatima," amesema Rashid.