Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bei ya Mafuta bado moto, Dola yatajwa

Muktasari:

  • Licha ya gharama za uagizaji mafuta kushuka kwa viwango tofauti na bei ya mafuta kushuka katika soko la dunia, wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni uliongezeka kwa asilimia 1.91 Aprili 2025

Dar es Salaam. Wakati bei ya mafuta nchini ikiongezeka kwa mwezi wa tatu mfululizo, kuanzia Januari hadi Aprili mwaka huu, Chama cha Waingizaji na Wasambazaji Mafuta Tanzania (Taomac) kimesema kuadimika kwa Dola za Marekani ndicho chanzo cha hali hiyo.

 Kwa mujibu wa chama hicho, hali ya kuadimika kwa dola ilianza kushuhudiwa mwishoni mwa Desemba mwaka jana, jambo ambalo liliweka ugumu kwao katika kuagiza bidhaa hadi pale Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilipoingilia kati suala hilo.

Hayo yameelezwa leo Jumatano, Aprili 2, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Taomac, Raphael Mgaya, alipozungumza na Mwananchi, ikiwa ni saa chache tangu Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) ilipotangaza ongezeko la bei kikomo za bidhaa hizo zitakazotumika kuanzia Aprili 2, 2025.

Bei hizo zilitangazwa kuongezeka, huku miongoni mwa sababu ikiwa ni ongezeko la wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni kwa asilimia 1.91 Aprili mwaka huu.

Dola ilipanda wakati ambapo bei kikomo za mafuta kwa Aprili mwaka huu katika soko la dunia zimepungua kwa asilimia 6.92 kwa mafuta ya petroli, asilimia 6.57 kwa mafuta ya dizeli, na asilimia 7.82 kwa mafuta ya taa.

Katika Bandari ya Mtwara, bei zimepungua kwa wastani wa asilimia 4.00 kwa mafuta ya petroli na dizeli, huku kukiwa hakuna mabadiliko katika Bandari ya Tanga.

Bei zinapungua sambamba na gharama za uagizaji mafuta, ambapo petroli ilipungua kwa wastani wa asilimia 6.08, asilimia 7.09 kwa mafuta ya dizeli, na imeongezeka kwa asilimia 1.11 kwa mafuta ya taa katika Bandari ya Dar es Salaam.


Hali ikoje?

Kuadimika kwa dola kumesababisha lita moja ya mafuta ya petroli yaliyopitia Bandari ya Dar es Salaam kufikia Sh3,037 Aprili mwaka huu kutoka Sh2,793 iliyokuwapo Januari, huku dizeli ikifikia Sh2,936 kutoka Sh2,644.

Kwa mafuta yaliyopitia Bandari ya Tanga, petroli yanauzwa kwa Sh3,083 Aprili mwaka huu kutoka Sh2,800 iliyokuwapo Januari, huku dizeli ikiuzwa kwa Sh2,982 kutoka Sh2,656.

Kwa mafuta ya petroli yaliyopitia Bandari ya Mtwara, sasa yanauzwa kwa Sh3,109 kutoka Sh2,866 iliyokuwapo Januari, huku dizeli ikifikia Sh2,958 kutoka Sh2,716.


Waagizaji wanasemaje?

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Aprili 2, 2025, Mgaya alisema kuwa huenda bei ya mafuta ikaanza kupungua mwezi ujao baada ya BoT kuingilia kati kuhakikisha inapunguza makali ya dola.

"Kuanzia Desemba na Januari, dola ilianza kuadimika na baadaye ikaanza kupanda, jambo ambalo liliweka ugumu kwetu kama kampuni za uagizaji wa mafuta. Ukiangalia mafuta tunayouza sasa, tuliagiza Februari wakati ambapo dola ilikuwa imeanza kupanda, hivyo tunachokiona leo ni matokeo ya hali ya nyuma," amesema Mgaya.

Amesema hali hiyo ilifanya waagizaji kuathirika hasa Januari na Februari, ambapo baadhi ya kampuni zilipata hasara, jambo lililowasukuma kuitisha kikao cha pamoja kati yao, Ewura, BoT na Wizara ya Nishati ili kujadili hatua za kuchukua.

"Ilionekana kuwa Benki Kuu itaingilia suala hili na kuhakikisha kunakuwa na dola za kutosha. Angalau tunaona kuna ahueni kuanzia Februari yenyewe na Machi. Sasa matokeo ya kilichofanyika tutaweza kuyaona katika kupungua kwa bei za mafuta angalau Mei au Juni, lakini haya tunayoyaona leo ni matokeo ya kile kilichokuwapo Januari na Februari," amesema Mgaya.

Kuhusu BoT kuhakikisha upatikanaji wa dola, kwa nyakati tofauti, taasisi hiyo imeonekana kutangaza kufanya minada ya fedha za kigeni na benki za biashara.

Miongoni mwa minada hiyo ni ule uliofanyika Machi 17, 2025, ambapo BoT ilishiriki katika soko la jumla la fedha za kigeni (IFEM) kwa mujibu wa sera yake ya ushiriki katika soko la fedha za kigeni kwa mwaka 2023.

Katika mnada huo, BoT iliuza Dola za Marekani milioni 30 kupitia mnada wa ushindani kwa kiwango cha wastani cha kubadilisha fedha za kigeni Sh2,646 kwa dola moja ya Marekani.

Mnada huo ulifanyika kupitia mfumo wa kielektroniki wa kufanyia mnada wa fedha za kigeni, yaani FX Auction System. Mnada kama huo ulifanyika tena Machi 27, 2025, ambapo Dola za Marekani milioni 25 ziliuzwa kupitia mnada wa ushindani kwa kiwango cha wastani cha kubadilisha fedha za kigeni cha Sh2,663.16 kwa dola moja.

Kutokana na hilo, Ewura imezitaka kampuni za mafuta kuuza bidhaa za petroli kwa bei ya ushindani, isipokuwa bei hizo zisizidi bei kikomo au kuwa chini ya bei iliyoruhusiwa, kama zilivyokokotolewa kwa mujibu wa Kanuni za Ewura za Kupanga Bei za Mafuta za Mwaka 2022.

Pia imevitaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa zao katika mabango yanayoonekana bayana, yakionesha bei za mafuta, punguzo, na vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.

"Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei yanayoonekana vizuri kwa wateja," imesema taarifa hiyo ya Ewura, iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu, Dk James Mwainyekule.