Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Balaa la mvua nchini

Magari yakipita katika Barabara ya Julius Nyerere eneo la Tazara iliyofurika maji kutokana na mvua zilizonyesha jijini Dar es Salaam jana. Barabara hiyo ilifurika maji baada ya kuziba kwa mitaro. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

TMA katika taarifa iliyoitoa jana kwa vyombo vya habari inasema mvua kubwa itaendelea kunyesha leo na kesho katika mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara na visiwa vya Unguja na Pemba.

Dar/Mikoani. Mvua kubwa iliyonyesha kwa siku tatu mfululizo hadi jana imesababisha madhara kwa binadamu vikiwamo vifo vya zaidi ya watu 10, na kuulazimu uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kufunga shule kwa siku mbili huku Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ikitoa tahadhari kwamba bado itaendelea kunyesha.

TMA katika taarifa iliyoitoa jana kwa vyombo vya habari inasema mvua kubwa itaendelea kunyesha leo na kesho katika mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara na visiwa vya Unguja na Pemba.

Mkurugenzi wa utafiti na matumizi ya hali ya hewa wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a akichanganua wingi wa mvua zilizonyesha alisema jana kwamba Kituo cha Dar es Salaam kwa Aprili hutakiwa kupima milimita 250 lakini hadi jana ikiwa ni nusu ya mwezi, kilikuwa kimepima milimita 345.

“Mvua imevuka wastani zaidi ya asilimia 35,” alisema Dk Chang’a na kwamba, kwa saa 24 pekee hadi jana, kituo hicho kilikuwa kimepima milimita 91.3.

Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri wa TMA, Samwel Mbuya alisema mwaka 1995, kilipima kiwango cha juu cha milimita 173.2 na mwaka 2011 kilipima milimita 156.3; mwaka 2013 milimita 153.3; na Oktoba mwaka jana milimita 153.3. Vipimo hivyo ni ndani ya saa 24.

“Kwa hiyo mvua kwa kituo cha Dar es Salaam ni za juu ya kiwango lakini hazijafikia miaka niliyoitaja hapo juu,” alisema.

Dk Chang’a alisema kituo cha Tabora, Aprili 14, kilipima mvua wastani wa milimita 153.9 ikiwa ni kipimo cha pili cha juu zaidi, cha kwanza kikiwa mwaka 1965.

Alisema Zanzibar kwa Aprili hupima wastani wa milimita 400 lakini hadi jana walipima milimita 593.1. “Ukiona wastani wa kila kituo ikiwa ni nusu ya mwezi, unaweza kuona ni mvua kiasi gani; ni za juu ya wastani,” alisema.

Awali, mkurugenzi mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alisema mvua itaendelea kunyesha na kwamba, kwa kawaida Aprili huwa kubwa juu ya wastani na kuwataka wananchi wachukue tahadhari na si wa bondeni pekee hata maeneo mengine.

Hali ya Dar es Salaam

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa akizungumza na waandishi wa habari jana alisema watu tisa wameripotiwa kupoteza maisha huku sita wakijeruhiwa kwa kuangukiwa na ukuta na wanaendelea na matibabu.

Alisema, “Nimezunguka kwa helikopta, maeneo mengi yameathirika kutokana na mvua na kusababisha madaraja kubomoka na sehemu nyingine maji kupita juu ya barabara ikiwamo eneo la Kijichi, Buguruni, Jangwani na Kigamboni.”

Miongoni mwa waliokufa kwa kuangukiwa na ukuta ni mtoto Nasra Ally (9) katika tukio lililotokea Mtaa wa Kizinga kando mwa mto Kizinga.

Diwani wa Kijichi, Eliasa Mtalawanje alisema Nasra ni miongoni mwa wananchi waliokuwa wamejihifadhi baada ya kuondolewa bondeni ambako nyumba zao zilizingirwa na maji.

Alisema nyumba 50 zimejaa maji na wakazi wake wanalala nje wakilinda mali zao. Alisema wameanzisha kambi kuwasaidia walioathirika.

Ally Abeid, baba mzazi wa Nasra alisema walisikia kishindo saa tisa usiku huku baadhi ya kina mama wakipiga kelele kuashiria kuna hatari. Alisema mwili umehifadhiwa katika Hospitali ya Temeke na utaratibu wa mazishi unaendelea.

Kutokana na maeneo mengi kujaa maji, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameziomba mamlaka za elimu kufunga shule kwa siku mbili.

Makonda aliyetembelea maeneo yaliyoathiriwa alisema miundombinu imeharibika ikiwamo ya shule, hivyo wanafunzi wabaki nyumbani hadi hali itakapotengemaa.

“Nimeziomba mamlaka za elimu kufunga shule kwa siku mbili hadi Jumatano kulingana na hali itakavyokuwa kwa sababu mvua inaendelea kunyesha maeneo mengi yamejaa maji kwa watoto hili si salama,” alisema Makonda.

Alisema hakuna sababu ya wananchi kusubiri kuondolewa na polisi au kugombana na Serikali wanapotakiwa kuhama maeneo hatarishi ikiwamo bondeni.

“Tunaendelea kukusanya taarifa, lakini barabara nyingi zimeharibika, nyingine zimejaa maji kwa wanaoishi maeneo hatarishi wachukue tahadhari mapema hali ni mbaya,” alisema Makonda.

Uda-rt wakwama

Kampuni inayotoa huduma katika mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam (Uda-rt) ililazimika kusitisha huduma kwa baadhi ya njia.

Taarifa ya Uda-rt imesema huduma kwa baadhi ya njia zilisitishwa kuanzia saa 11:00 alfajiri kutokana na kufungwa Barabara ya Morogoro eneo la Jangwani baada ya maji kupita juu.

“Kwa sasa huduma zinatolewa kwa njia za Mbezi – Kimara; Kimara – Morocco; Kimara - Magomeni Mapipa; Kivukoni – Muhimbili; Gerezani – Kivukoni na Gerezani – Muhimbili,” inasema taarifa ya Uda-rt iliyotolewa na mkuu wa kitengo cha mawasiliano, Deus Bugaywa.

Zanzibar nako si shwari

Mvua hizo pia zimesababisha zaidi ya nyumba 120 kuharibika katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar. Kaimu mkurugenzi kamisheni ya kukabiliana na maafa Zanzibar, Makame Khatib Makame alisema takwimu hiyo ni ya awali.

Aliyataja maeneo yaliyoathirika kuwa ni Amani Kwawazee, Daraja Bovu, Seblen, Mwanakwerekwe, Fuoni na Kibonde Mzungu.

Makame alisema baadhi ya miundombinu ya barabara imeharibika ikiwamo barabara ya Fuoni na Mwanakwerekwe ambayo imefungwa kutokana na kujaa maji.

Alisema wanaendelea na tathmini ili kujua athari kwa jumla na kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na maafa.

Madhara Kanda ya Ziwa

Watoto wawili kupoteza maisha, ng’ombe 90 kupigwa radi, nyumba 56 kubomolewa na kukatika kwa mawasiliano kati ya baadhi ya vijiji kutokana na daraja kubomoka ni miongoni mwa madhara ya mvua hiyo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Usiku wa kuamkia Aprili 9, watoto wawili wa familia moja, Mussa Baraka (2) na Mariam Simoni (4) walifariki dunia kwa kuangukiwa na ukuta wa nyumba walimokuwa wamelala katika Mtaa wa Buguku eneo la Buhongwa jijini Mwanza.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema watu watatu akiwamo mama mzazi wa watoto hao, Dabacha Simon; bibi yao, Linda Kulwa na kaka yao, Simon Samson (5) walijeruhiwa katika tukio hilo lililotokea saa nane usiku na kulazwa katika hospitali ya Wilaya ya Nyamagana ya Butimba.

Wilayani Bukombe, Geita, vijiji vya Imalanguzu na Bukombe havina mawasiliano tangu Aprili 10 baada ya daraja la Mto Imalanguzu linalotenganisha vijiji hivyo kubomoka. Fundi sanifu wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) wilayani Bukombe, Joel Nyanda alisema ofisi ya yake inaendelea na tathmini kuhusu madhara hayo ili kuruhusu mchakato wa matengenezo kuanza.

Wilayani Muleba, Kagera, zaidi ya nyumba 56 zimebomoka katika kata za Karambi na Kyebitembe. Nyumba 45 kati ya hizo zimebomoka kuta wakati kumi na moja zimeanguka kabisa. Hakuna madhara kwa binadamu yaliyotokea.

Ofisa habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Lucy Binamungu alisema mvua imeharibu mashamba ya mihogo, viazi na maharagwe, “Pia imebomoa barabara katika maeneo ya Rugasha, Nyakagoma, Muziro na Kanyabwenda.”

Wilayani Ngara, diwani wa Nyamagoma, Laurent Johh alisema ng’ombe 90 wamepigwa radi jioni ya Aprili 15.

Mkoani Tabora watu watatu wameripotiwa kufa, huku barabara za Kaliua - Kigoma na Tabora - Mpanda zikishindwa kupitika kutokana na madaraja kujaa maji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Wilbrod Mutafungwa alisema Aprili 14 saa tisa usiku katika Kijiji cha Mirambo wilayani Nzega, watu watatu waliangukiwa na ukuta wa nyumba waliyokuwamo na kufariki dunia. Alisema watu hao walikuwa wakiishi katika nyumba ya tembe iliyojengwa kwa udongo.

“Kwa sasa tunashirikiana na watu wa Tanroads (Wakala wa Barabara Tanzania) kuhakikisha angalau baadhi ya maeneo yanapitika,” alisema.

Rukwa, Morogoro na Arusha

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kiando alisema Barabara ya Kaoze haipitiki kutokana na mvua.

Alisema watumiaji wa barabara hiyo wanalazimika kushuka kwenye magari na kuvuka kwa miguu hadi upande wa pili.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema maeneo ya Kilombero, Kilosa na Malinyi nyumba zilizojengwa kando mwa mito zimejaa maji.

“Natoa ushauri kwa jamii iliyojenga pembezoni mwa mito na bondeni zichukue tahadhari kwa kuwaondoa wazee, watoto na wagonjwa na hasa wakati mvua,” alisema.

Mkoani Arusha watu wawili wameripotiwa kufariki dunia na zaidi ya nyumba 50 kuharibiwa pamoja na barabara.

Kaimu kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha, Yusuph Ilembo alisema matukio mengi ya athari za mvua hayajaripotiwa na kutoa wito kwa viongozi wa vijiji na mitaa kutoa taarifa.

Kaimu mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Idd Kimanta aliyekagua athari za mvua katika maeneo ya Nduruma, Bulka na Mushono jana, alisema mwili wa mwanamke mmoja umeokotwa eneo la Mushono.

Katika jiji la Arusha, maeneo ya kata za Murieti, Unga Ltd, Sakina, Mushono na Mianzini kumeripotiwa madhara kadhaa ikiwamo barabara kuharibika.

Mji wa Mto wa Mbu wilayani Monduli baadhi ya makazi ya watu yamezingirwa na maji.

Imeandikwa na Ibrahim Yamola, Asna Kaniki, Pamela Chilongola na Kalunde Jamal (Dar); Haji Mtumwa (Zanzibar); Shaaban Ndyamukama, Ngollo John na Ernest Maghashi (Kanda ya Ziwa); Mussa Juma, Filbert Rweyemamu, Moses Mashalla na Happy Lazaro (Arusha)