Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bajeti katika mtazamo wa kijinsia

Dar es Salaam. Wanaharakati wa kutetea masuala ya kijinsia wamesema bajeti iliyowasilishwa bado haijazingatia mtazamo wa kijinsia huku wakisema ukuaji wa uchumi unaosemwa haundani na hali ilivyo mtaani.

Wanaharakati hao wametoa maoni hayo  katika mdahalo wa ‘Kijiwe cha Kahawa' kujadili Bajeti ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa mtazamo wa kijinsia, unaandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na kufanyika Mabibo, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.

Katika mdahalo huo, pia wadau hao  walipata fursa ya kufuatilia mubashara uwasilishaji wa bajeti iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba.

Wakitoa maoni yao, Mofati Mapunda, amesema taarifa za bajeti hasa inapoeleza pato la taifa limekuwa huwa inawatatanisha kwa kuwa hali halisi huko mtaani ni tofauti lakini pia haijazingatia maeneo muhimu yanayomgusa mwanamke moja kwa moja yanakuwa hayajaguswa.

“Mfano mpaka sasa  tunapozungumzia masuala ya maji ni kweli mabomba yamefika lakini maji hayajafika kwenye majumba ya watu na waliofikiwa pia kuyapata ni kwa taabu huku wanawake wakiwa waathirika wakubwa wa kufuata mbali huduma hiyo muda ambao wangeshiriki shughuli zingine za kujiingizia kipato.

“Vilevile unapozungumzia uhaba wa maji mashuleni unamgusa moja kwa moja mtoto wa shule kwa sababu uhitaji wa maji kwa mtoto wa kike ni muhimu kuliko wa kiume.

Jumanne Sako mkazi wa Kondoa, amesema kuna haja ya serikali kuangalia changamoto ya ajira hususani kwa vijana.

Sako amesema licha ya kilimo kuonekana kwamba kinaweza kuwatoa vijana, bado kumekuwepo na migogoro ya ardhi jambo linalowakatisha tamaa kujikita katika kazi hiyo huku zile zinazotangazwa na serikali zikichukua idadi ndogo ukilinganisha na vijana waliopo mtaani.

Wakati Sako akisema hivyo, katika bajeti hiyo ya serikali ya Sh56.49 trilioni, kundi la vijana limetengewa Sh38.4 bilioni, ikiwa ni kiwango kidogo zaidi cha fedha kilichotengwa kwa mujibu wa mgawanyo wa bajeti katika sekta.

Naye Cateherine kutoka Kahama, amesema kuna haja wakati wa uandaaji bajeti, serikali ianze kupokea maoni  kuanzia kwenye mitaa ili wananchi wenyewe waweze kutoa maoni ya vile wanavyotamani kuona vinaingia kwenye bajeti ili kuwa na bajeti yenye mlengo wa kijinsia na inayogusa maisha yao moja kwa moja.

Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Lisa Kabeta, amesema katika bajeti hii kuna haja ya serikali kupongezwa kudhibiti mfumuko wa bei kwani hali inavyokuwa hivyo huleta afueni hadi kwa mwananchi wa hali ya chini.

Hata hivyo Lisa amesema wakati hali ya uchumi ikionekana kukua, lakini hali ya umasikini nchini bado ni tatizo kwani katika kila watu 100, watu 43 ni masikini.

“Hali hii inasababishwa na kuwepo kwa tofauti kubwa kati ya watu matajiri na wale masikini, hivyo kuna njia tofauti zinaweza  kutumika ikiwemo kuwa na usawa wa mapato ili kila mtanzania aweze kufaidika kwa ukuaji huo wa uchumi.

Mjumbe kutoka Mtandao wa TGNP, Anna Kikwa, amesema ni kweli maendeleo katika kuongezeka kwa shule nchini wanayaona na  elimu bila malipo lakini katika utekelezaji wake sio kwani hakuna walimu wa kutosha ukilinganisha na idadi ya wanafunzi.

Lakini pia tatizo jingine hakuna vitabu vya kutosha na kushauri kuwepo kwa uwiano katika utekelezaji wa suala hilo ikiwemo kuajiri walimu ili watoto wote  wa nchi hii wapate elimu iliyo sawa.

Wakati upande wa afya, Agnes Tilya  kutoka Shirika la Msichana Initiative, amesema ni kweli hospitali na vituo vya afya vimejengwa wanaviona lakini hakuna vifaa tiba na  wahudumu ni wachache.

“Pia wakati serikali ikisema matibabu ni bure kwa wajawazito ukweli ni kwamba wanaambiwa waende na vifaa vyao ikiwemo glovu na hivyo kuondoa dhana nzima ya kumpatia haki mwanamke haki yake ya kuzaa,” amesema Agnes.

Hata hivyo amesema ili kuwasaidia watoto wa  kike wanaokosa masomo wanapoingia mwezini,  kuna haja ya taulo za kike kutolewa bure kama zinavyotolewa kondomu hali itakayowasaidia wanafunzi hao kuliko ilivyo sasa.

“Tanzania tuna uwezo wa kutoa taulo hizi bure, kwa kuwa sisi hatukujiumba hivi, kwani kuanzia siku tatu hadi tano kuna mtoto wa kike anakosa masomo kwa kuwa kakosa kifaa cha kujistiri  anapoingia mwezini.

“Katika hili hata serikali inaweza kujenga kiwanda chake cha taulo ili ziwafae watoto kutoka familia za masikini,” amesema Agnes.

Kaimu Mkurugenzi wa TGNP, Clara Kalanga, ambaye ni Mkuu wa Programu - TGNP, Clara Kalanga amesema mjadala huo una lengo la kuchochea mabadiliko chanya ya kisera na kiutendaji kupitia uchambuzi wa bajeti ya taifa kwa jicho la kijinsia.

“Tunakutana hapa siyo tu kwa ajili ya kufuatilia bajeti, bali pia kutathmini utekelezaji wake kwa kuzingatia changamoto za makundi yaliyopo pembezoni wakiwemo wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na wanaume maskini,” amesema mkurugenzi huyo.

Amesema kupitia jukwaa hilo ambalo limekuwepo tangu mwaka 2016, wameendelea kujenga ushirikiano na wadau mbalimbali katika kuhakikisha sauti za wananchi, hususan makundi ya pembezoni, zinazingatiwa katika upangaji wa bajeti ya taifa.