Baba aliyefungwa miaka 30 kwa kumbaka mwanaye aachiwa

Muktasari:
- Mahakama ya Rufani imemuachia huru baba aliyekuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 30 kwa kumbaka mtoto wake, baada ya kubaini kuwa shtaka halikuthibitishwa bila shaka na kielelezo muhimu cha PF3 kilipokelewa kinyume na utaratibu.
Arusha. Mahakama ya Rufani imemuachia huru baba aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kumbaka mtoto wake.
Baba huyo mkazi huyo wa Kijiji cha Lengurumo Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, alidaiwa kumbaka binti yake mwenye umri wa miaka 16, Septemba mosi, 2017.
Rufaa hiyo ilitokana na uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi uliotolewa Aprili 27, 2021 katika Rufaa ya jinai namba 30 ya mwaka 2020.
Uamuzi wa Makama ya Rufani umetolewa Agosti 23, 2024 na majaji watatu--- Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, Dk Mary Levira na Zephrine Galeba walioketi Moshi.
Majaji hao baada ya kupitia hoja za rufaa, walibaini shtaka hilo halikuthibitishwa bila kuacha shaka na kuondoa kielelezo kimoja ambacho ni fomu ya matibabu namba tatu (PF3) kwenye kumbukumbu za rufaa hiyo, baada ya kubaini ilipokelewa kinyume na utaratibu.
Msingi wa rufaa
Baba huyo alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Mwanga iliyoko Mwanga akikabiliwa na shtaka moja la ubakaji alilodaiwa kutenda Septemba mosi, 2017.
Baada ya kusikiliza ushahidi, Mahakama hiyo ilimhukumu kifungo cha miaka 30 jela, ndipo alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi bila kufanikiwa na kisha kukata rufaa mahakama hiyo ya juu nchini.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mwaathirika huyo na ndugu zake wawili, walikuwa wakiishi na baba yao kwani mama yake hakuwa akiishi nao.
Siku ya tukio ilidaiwa mwaathirika huyo aliitwa na baba yake chumbani kwake na alipoingia alimkuta amekaa kitandani na alimuamuru avue nguo na alipokataa, alitishiwa kuuwawa kwa kisu.
Mwaathirika huyo alidai kutokana na vitisho hivyo alilazimika kuvua nguo na baba yake alimbaka na kudai aliendelea kumbaka kwa nyakati tofauti kwa muda wa wiki nzima.
Alidai alikwenda kutoa taarifa kwa mama yake aliyekuwa akiishi eneo la Kisangara na kutokana na vitendo hivyo alishindwa kwenda shule na alipomjulisha mwalimu kuhusu suala hilo alitakiwa kukaa bweni na suala hilo likaanza kuchunguzwa.
Katika utetezi, mzazi huyo alidai katika tarehe isiyojulikana siku ya Ijumaa, mwaathirika alitoweka nyumbani na alipowauliza ndugu zake walimweleza amekwenda kwa babu yake na alipomtaka arudi, alikataa.
Alidai kuwa baada ya binti yake kuondoka alipigiwa simu na babu yake akimtaka apeleke ada ya shule na kudai alikataa kupeleka na wiki mbili baadaye alipigiwa simu Kituo cha Polisi Mwanga, na kufunguliwa shtaka akidaiwa kumbaka mtoto wake.
Katika utetezi wake alitetewa pia na watoto wake wawili ambao walidai walikuwa wakilala na dada yao chumba kimoja katika vitanda tofauti, mara nyingi walikuwa wakimsikia dada yao akilalamika kufanya kazi nyingi na kudai angeondoka na kwenda kwa babu yake.
Rufaa
Hoja za rufaa yake ilikuwa ni pamoja na kuwa na tofauti kati ya shtaka na ushahidi, kwani hati inaonyesha kosa lilifanyika Septemba mosi, 2017 huku mwaathirika akitoa ushahidi kuwa lilifanyika kwa wiki nzima, ushahidi kutothibitishwa bila kuacha shaka.
Alidai ushahidi wa mashtaka ulipingana na kujaa tofauti na kwamba kesi dhidi yake ilitungwa, kwani mwaathirika huyo alitaka kuishi na baba yake na upande wa mashtaka kushindwa kuwaita mashahidi, huku ushahidi wake wa utetezi kutokupewa uzito licha ya kuibua shaka ya kutosha.
Katika usikilizwaji wa rufaa hiyo, mrufani alijitokeza yeye mwenyewe bila kuwakilishwa na alikubali sababu zake za kukata rufaa, huku upande wa mashtaka ukiwakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Wakili Rose Sulle.
Wakili Sulle alikubali msingi kwa rufaa hiyo na kuielekeza Mahakama ukurasa wa 19 wa kumbukumbu ya rufaa inaeleza shahidi wa nne ambaye ni daktari aliitambua PF3 ambayo aliijaza baada ya kumchunguza mwaathirika na kuisoma kabla haijapokelewa mahakamani.
Wakili huyo alieleza huo ni ukiukwaji wa taratibu na kuiomba Mahakama ifute kielelezo hicho kwenye kumbukumbu zake.
Aidha, wakili Sulle alipinga hoja kuwa kulikuwa na tofauti kati ya hati ya mashtaka na ushahidi na kuwa ilikuwa sahihi mwaathirika huyo kusema alibakwa tarehe hiyo kwa sababu ndipo ilipoanza na baba yake aliendelea kufanya hivyo wiki nzima, hivyo hakuna utofauti.
Uamuzi majaji
Jaji Levira alieleza kuwa Mahakama ya kwanza ya rufaa ilipuuza ukiukwaji huo wa taratibu na wanakubaliana na wakili Sulle kuwa kielelezo hicho kilipaswa kufutwa, hivyo kukubaliana na sababu hiyo ya rufaa na kufuta kielelezo hicho kwenye kumbukumbu za Mahakama.
Jaji Levira alisema kuhusu tarehe ya tukio hilo inayodaiwa kutajwa, wanadhani wanahitaji kujiuliza swali moja zaidi, kwa nini mtoto huyo hakueleza kuwa alibakwa mara kwa mara akihojiwa na polisi.
“Tunasema hivyo kwa sababu kwa mujibu wa shtaka hilo, mwathiriwa alibakwa Septemba mosi, 2017 lakini katika kesi hiyo, shahidi alibadilisha maelezo na kueleza kuwa alibakwa wiki nzima iliyofuata,” alisema
Jaji alisema hawakubaliani na hoja ya wakili Sulle kwamba kwa kutaja tu tarehe hiyo katika ushahidi wake ilitosha kuthibitisha shtaka na kifungu cha 234 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kinaeleza iwapo kuna tofauti katika tarehe, shtaka lirekebishwe chini ya kifungu hicho.
Jaji Levira alisema ingawa wangeweza kuishia hapo kwa maana kesi hiyo haikuthibitishwa, ila kwa madhumuni ya kuonyesha mashaka zaidi katika kesi ya mashtaka, watajadili sababu ya nne ya kukata rufaa ambayo ni baba huyo kulalamika kesi hiyo ilitungwa dhidi yake baada ya kukataa kutoa hela ya ada.
“Tumechunguza kwa kina rekodi ya kukata rufaa kwa nia ya kujiridhisha, ikiwa kulikuwa na uwezekano wa kesi kubuniwa dhidi ya mrufani. Hatuwezi kukubaliana na wakili Sulle kwamba hapakuwa na kinyongo kati ya mrufani na babu ambaye hakuitwa kutoa ushahidi wake,” alisema.
Jaji alisema ni wajibu wa upande wa mashtaka kuthibitisha kesi dhidi ya mrufani bila shaka yoyote na kuwa katika ukurasa wa 95 wa kumbukumbu ya rufaa, Mahakama ya kwanza ya rufaa, mrufani alidai kesi ni ya uzushi dhidi yake kutokana na ugomvi wa kifamilia kati yake na mama wa mtoto, ila hakukuwa na ugomvi kati yake na mtoto wake.
“Tunaona kutokana na dondoo hapo juu la uamuzi wa Mahakama ya rufaa ya kwanza kwamba jaji hakuzingatia ushahidi kwa ujumla wake na kwa vile uamuzi wa sababu hizo mbili za kukata rufaa una matokeo ya kuamua rufaa nzima, tunaruhusu rufaa na kufuta hukumu ya mrufani,” alisema.