Aweso awapa tabasamu waliokatiwa maji
Muktasari:
- Mbali na hilo Aweso amepiga marufuku ubambikiaji wa bili za maji na kuagiza wote waliokatiwa maji warudishiwe mara moja na utaratibu upangwe jinsi ya kufanya malipo.
Dodoma. Waziri wa Maji Jumaa Aweso ameagiza katakata ya maji isiwepo kuanzia sasa bali ukataji uwe ni kwa sababu za msingi tena wateja wapewe taarifa za kwa nini maji yanakatwa akisema Watanzania hawataki blabla ya maneno bali wanataka maji.
Mbali na hilo Aweso amepiga marufuku ubambikiaji wa bili za maji na kuagiza wote waliokatiwa maji warudishiwe mara moja na utaratibu upangwe jinsi ya kufanya malipo.
Waziri Aweso ametoa kauli hiyo wakati akisoma hotuba ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/27 ambapo ameliomba Bunge limuidhinishie kiasi cha Sh1.12 trilioni.
“Huduma ya maji lazima iwe endelevu, siyo leo kuna maji kesho hakuna maji, hakuna kukata maji weekend na hakuna kukata maji sikukuu, Mteja kabla hajakatiwa maji apewe taarifa,” amesema Aweso.
Waziri ameagiza pia maunganisho ya maji yafanyike ndani ya siku saba na akatangaza wateja wote waliokatiwa maji na wenye faini wafike kwenye mamlaka za maji wapewe utaratibu wa kurejeshewa maji ili tabasamu lao lidumu.
“Habari ya kubambakizia watu bili za maji, hizo zilipendwa, kutafuta mivujo kwa macho zilipendwa, tumieni mita janja ambalo ni suluhisho lakini tekelezeni mkakati wa kuharakisha ufungaji wa dira za maji za malipo kabla wa mwaka 2026–2030 ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa maduhuli,” amesema Waziri Aweso.
Ametaja ufungaji wa dira hizo kwamba utasaidia kuondoa malimbikizo ya madeni, kupunguza malalamiko ya ankara bambikizi na kudhibiti matumizi holela ya maji.