ATCL yapata hasara ya Sh60 bilioni

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka akizungumza bungeni alipokuwa akiwasilisha taarifa ya shughuli za kamati hiyo kwa mwaka 2021, jijini Dodoma leo. Kamati hiyo imefanya uchambuzi wa kina katika hesabu zilizokaguliwa za ATCL na kubaini kuwa ATCL ilipata hasara ya kiasi cha Sh60.2 bilioni kwa mwaka wa fedha 2019 /2020 hivyo kufanya hasara jumuifu tangu mwaka 2015/2016 (Accumulated losses) kufikia kiasi cha Sh152.9 bilioni. Picha na Edwin Mjwahuzi
Muktasari:
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Tanzania imebaini kuwa Shirika la Ndege (ATCL) lilipata hasara ya Sh60.24 bilioni kwa mwaka wa fedha 2019 /2020.
Dodoma. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imebaini kuwa Shirika la Ndege (ATCL) lilipata hasara ya Sh60.24 bilioni kwa mwaka wa fedha 2019 /2020.
Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka ameyasema hayo leo Alhamis Februari 17, 2022 wakati akiwasilisha taarifa ya shughuli za kamati kwa kipindi cha Januari 2021 hadi Februari 2022.
Amesema katika uchambuzi wa kamati katika taarifa ya CAG kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2020 ulibaini kuwa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ilikuwa na mtaji hasi Sh246.66 bilioni.
Amesema pamoja na changamoto za mtaji, ATCL imekuwa na ongezeko la deni la Sh152. 16 bilioni ambapo deni hilo linahusisha Sh70.94 bilioni (asilimia 47 ya deni lote), deni ambalo ATCL wanadaiwa na Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA).
Amesema kamati imefanya uchambuzi wa kina katika hesabu zilizokaguliwa za ATCL na kubaini kuwa ATCL ilipata hasara ya kiasi cha Sh60.24 bilioni kwa mwaka wa fedha 2019 /2020 hivyo kufanya hasara jumuifu tangu mwaka 2015/2016 kufikia Sh152.96 bilioni.
“Uwepo wa madeni ya muda mrefu ni kihatarishi cha uendelevu wa kampuni kwa siku zijazo. Kwa msingi huo, kihatarishi hicho kimesisitizwa kwa kina katika hati ya ukaguzi iliyotolewa na CAG katika hesabu za ATCL kwa mwaka wa fedha 2019/2020,”amesema.
Amesema CAG alitoa hati safi ya ukaguzi yenye masuala ya msisitizo (Unqualified audit opinion with emphasis of matter).
Kaboyoka amesema suala la msisitizo katika hati hiyo ya ukaguzi ni hoja ya mtaji na madeni ya ATCL hali ambayo inaweza kusababisha kampuni kushindwa kujiendesha kwa siku zijazo.
Amesema hoja nyingine ambazo zinachangia ATCL kutokuwa na ufanisi wa kutosha kifedha hadi sasa na uwepo wa madeni makubwa ya siku za nyuma ambayo hayajalipwa.
Aidha, kuna deni la kiasi cha Sh87.25 bilioni (Asilimia 59 ya deni lote) ambalo ni deni la Kampuni ya Wallis Trading Inc. iliyokuwa imeikodishia ATCL Ndege miaka ya nyuma.
Pia walibaini kutofikiwa kwa malengo ya kifedha ya kampuni kwa kiwango cha asilimia ambapo mwaka 2019/2020 ATCL ilipanga kupata mapato kiasi cha Sh661.64 bilioni.
Hata hivyo, walifanikiwa kupata mapato Sh157.60 bilioni hivyo kuathiri ufanisi wa kampuni.
Amesema wamebaini uwepo wa vifungu kadhaa vya kimkataba ambavyo vinasababisha ATCL kuongeza deni ikiwemo shirika hilo kuingia mkataba wa gharama za ukodishaji wa ndege Sh15.46 bilioni kati yake na TGFA kutokuwa na kipengele cha vihatarishi visivyotabirika.
Amesema gharama hiyo ilitokana na ukodishaji wa ndege ambazo hazikufanya kazi wakati wa kipindi cha janga la uviko - 19 kati ya Machi 15 na Juni 30, 2020.
Amesema endapo kipengele hicho kingekuwepo kwenye mkataba, ATCL wasingetozwa gharama hizo.
Pia amesema ATCL iliingia gharama mara mbili ya Sh16.97 bilioni kama gharama za matengenezo ya ndege kutokana na dosari za kimkataba kati yake na TGFA.
“Masuala hayo matatu kwa kiasi kikubwa ndiyo yaliyochangia kutofikiwa malengo na ufanisi wa ATCL kwa mwaka wa fedha 2019/2020,”amesema.