Askari adaiwa kuuza dawa za Serikali

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mafia, Kassim Ndumbo akizungumza katika kikao cha wataalamu wa afya halmashauri ya Mafia na watendaji kutoka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) wakati akitoa maagizo ya kufunga asilimia 62 ya maduka ya dawa muhimu kutokana na kukiuka sheria.. Na mpiga picha maalum
Muktasari:
- Mtumishi wa Jeshi la Magereza wilayani Mafia Mkoa wa Pwani (jina limehifadhiwa) anadaiwa kukutwa akiuza dawa za Serikali katika duka lake binafsi kinyume na sheria, kanuni na maadili yanayohusika na utoaji wa huduma za afya.
Dar es Salaam. Mtumishi wa Jeshi la Magereza wilayani Mafia Mkoa wa Pwani (jina limehifadhiwa) anadaiwa kukutwa akiuza dawa za Serikali katika duka lake binafsi kinyume na sheria, kanuni na maadili yanayohusika na utoaji wa huduma za afya.
Hayo yalibainika jana baada ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kanda ya mashariki kufanya ukaguzi wa dawa na vifaatiba katika Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kuanzia Desemba 12 hadi 24.
Kutokana na sakata hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mafia, Kassim Ndumbo ameagiza mamlaka zinazomsimamia mtumishi huyo zimchukulie hatua na kumhoji, ili kujua wapi alitoa dawa hizo kabla ya hatua nyingine za kisheria hazijafuatwa.
Alipotafutwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Mzee Ramadhan Nyamka kuzungumzia suala hilo simu yake ya mkononi iliita bila majibu.
Hata hivyo, Kamanda wa Magereza Mkoa wa Pwani, Lupina Lyimo alisema hana taarifa na kuomba apewe muda, ili afuatilie suala hilo.
Alisema ikiwa anahusika anapaswa kwenda kuwajibika kwa vyombo husika ili abainishe anakozipata dawa hizo.
Baada ya dakika tano, Kamanda Lupina alipiga simu akisema, amefuatilia na kuelezwa, “dawa zilizokutwa si za Serikali, lakini ni dawa ambazo hazipaswi kuuzwa kwenye famasi ndogo, zinauzwa kwenye famasi kubwa.”
Kamanda huyo alikiri kumfahamu askari huyo.
Katika maelekezo yake, Ndumbo alisema, “aliyekutwa na dawa za Serikali anatakiwa kuchukuliwa hatua, mamlaka zinazomsimamia zimuite, zimuonye na sheria ichukue mkondo wake na nimedokezwa huyu ni mtumishi wa Jeshi la Magereza, ni mhudumu wa afya pale.
“Mwanzo nilidhani ni mtumishi ambaye yupo chini ya halmashauri, nisingeagiza mamlaka nyingine ningemchukulia hatua mimi,, sasa tunatakiwa twende mbele kidogo hizi dawa alizokutwa nazo za Serikali amezichukua kutoka zahanati ya Magereza au amezichukua kutoka katika zahanati au vituo vya afya vingine vilivyo chini ya halmashauri,” alisema.
Ndumbo alishinikiza suala hilo lihakikiwe kwa uharaka kwa mamlaka hiyo ikishirikiana na TMDA, ili kabla timu hiyo haijaondoka Mafia ukweli ujulikane.
Pamoja na hayo, TMDA ilibaini asilimia 62 ya maduka ya dawa muhimu hayana watoa huduma wenye sifa na mkurugenzi huyo aliagiza yafungwe.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Dk Zuberi Mzige alisema hatua walizochukua kwa aliyekiuka taratibu za uendeshaji kwa kukutwa na dawa za Serikali ni kulifungia duka hilo na kuandikiwa faini ya kulipa na mamlaka haitampa kibali mpaka itakapojiridhisha ametekeleza taratibu za kisheria.
Hata hivyo, Dk Mzige alisema dawa hizo za Serikali hazikutoka idara ya afya Mafia, baada ya wafamasia kujiridhisha kwa Batch number ya dawa zilizoonekana ingawa ni mali ya Serikali.
Pia alisema kufungwa kwa asilimia 62 ya maduka yaliyokiuka sheria hayawezi kuathiri mfumo wa huduma wilayani humo, kwani ni maduka ya dawa muhimu ambazo zinapatikana kwa urahisi.
Akitoa taarifa ya ukaguzi huo katika kikao cha Kamati ya Dawa na Vifaatiba (CFDC) ya Halmashauri ya Mafia, Mkaguzi wa TMDA, Japhari Said alisema katika ukaguzi huo walikagua jumla ya majengo 50 ikiwa ni vituo vya kutolea huduma za afya 24 na maduka ya dawa muhimu 26.
“Maduka 16 hayakuwa na wahudumu wenye sifa, 14 sawa na asilimia 54 yamebainika kuuza dawa zisizo ruhusiwa kuwepo kwenye maduka ya dawa muhimu.
“Pia tumebaini maduka tisa hayakuwa na kibali, tisa mengine yakiwa na dawa zilizokwisha muda wa matumizi zikiwa hazijatengwa sawa na asilimia 35 ya maduka yote,” alisema Japhari.
Baada ya kupokea ripoti hiyo, Ndumbo alimwagiza Dk Mzige kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu maduka yote yaliyofungwa kutofunguliwa hadi watakapotimiza vigezo na masharti na kuhakikisha wanafanya ukaguzi mara kwa mara, ili kuchukua hatua kwa wanaokiuka sheria, kanuni na maadili.