Arusha waadhimisha siku ya wanawake kwa kuwakumbuka wenye saratani

Baadhio ya wanawake wa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Wanawake Wafanyabiashara na Wajasiriamali mkoani Arusha wakiadhimisha siku ya wanawake duniani kwa kuhamasisha uchangiaji damu kwa watoto wenye saratani ya damu.
Muktasari:
Katika kuelekea kilele cha siku ya wanawake duniani, baadhi ya wanawake mkoani Arusha wamejitokeza katika uchangiaji damu kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye saratani wanaotibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC)
Arusha. Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, baadhi ya wanawake mkoani Arusha wamejitokeza katika uchangiaji damu kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye saratani wanaotibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC)
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo jijini Arusha, Mwenyekiti wa Bodi wa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Wanawake Wafanyabiashara na Wajasiriamali, Nsendo Olasa amesema katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani wameona wajikite katika kuwasaidia watoto wenye saratani ya damu walioko katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC)
"Pamoja na kujitolea damu pia wametoa vitu mbalimbali kwa kuwasaidia watoto ikiwemo unga wa uji, mafuta ya kupaka, sabuni, miswaki na dawa za meno,"amesema Olasa.
Kwa Upande wake meneja wa chama hicho, Maria Maembe amesema katika maadhimisho hayo wamepata fursa ya kuwakumbushana juu ya umuhimu wa mahusiano ya biashara hali itakayowasaidia kutambua majukumu yao katika familia na biashara.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Arusha, Mkumbwa Musa amewataka wanawake kuwa waadilifu ili waweze kufanya vizuri katika chama chao pamoja na jamii kwa ujumla.
"Napenda kusisitiza kuwa ili ushirika huu uweze kufanya vizuri ni lazima wanachama wote tuwajibike vizuri na bodi ya chama ihakikishe usimamizi uwe vizuri katika kuzingatia uboreshaji wa shughuli mbalimbali za chama ikiwemo kusaidia jamii,"amesema Musa.
Amewataka watendaji wawe wabunifu katika uwekezaji kwa njia ya kufanya utafiti wa kutosha ili waweze kusaidiana pamoja na kusaidia jamii katika kutatua changamoto kwa jamii kulingana na nafasi waliyonayo.
Daktari kutoka idara ya magonjwa ya saratani KCMC, Atukuzwe Kahakwa ameshukuru wanawake hao kujitolea damu kwani hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto ya kutibu ugonjwa huo kutokana na uhitaji wa damu kila mara.
"Upungufu wa damu unasababishwa na ugonjwa wenyewe pamoja na dawa anazotumia mgonjwa lakini ni vyema watu wote wajitokeze kupima ili kufahamu afya yako kwani endapo ukigundulika katika hatua za awali unapona kabisa na ugonjwa huu wanawake wanaongoza kwa saratani ya matiti na wanaume tezi dume,"amesema Dk Kahakwa.