Anayedaiwa kumuua mtoto wake wa kufikia, apandishwa kizimbani

Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Kilombero. Picha Hamida Shariff
Muktasari:
- Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 18, 2024 itakapotajwa tena mahakamani hapo na mshtakiwa amerudishwa rumande.
Ifakara. Baba wa kufikia wa mtoto wa Johnson Ngonyani (6) aliyeuawa kwa kuchinjwa na kukatwakatwa viungo, Erick Magulu (33) amefikishwa mahakamani katika mahakama ya wilaya ya Kilombero kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
Magulu amefikishwa mahakamani hapo leo Juni 8, 2024, mbele ya Hakimu Bestina Saningo na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Dastan William ambapo amedai kuwa mshtakiwa huyo ametenda kosa hilo usiku wa Juni 1 mwaka huu.
Willam amedai kuwa Magulu alimuua mtoto huyo kwa kumchinja shingo na kumkata mikono, viganja na sehemu za siri. Amedai kuwa mshtakiwa huyo ametenda kosa hilo la mauaji huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Baada ya kusomewa hati ya mashitaka yanayomkabili mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kisheria kusikiliza shitaka hilo la mauaji.
Hakimu Saningo ameahirisha kesi hiyo mpaka Juni 18, 2024 itakapotajwa tena mahakamani hapo na mshtakiwa amerudishwa rumande.