Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyembaka shemeji yake ashindwa rufaa licha ya dosari katika hukumu

Muktasari:

  • Licha ya Mahakama Kuu kuibaini dosari katika hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Moshi, ambapo ilitumia baadhi ya mambo ambayo hayakuungwa mkono na ushahidi uliorekodiwa, kasoro hiyo haikumnasua Ayubu Abdala Mhera katika hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa kumbaka shemeji yake.

Arusha. Licha ya Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Moshi kuikosoa Mahakama ya Wilaya ya Moshi kwa kutumia baadhi ya mambo ambayo hayakuungwa mkono na ushahidi uliorekodiwa katika kumtia hatiani Ayubu Mhera, dosari hiyo haijaweza kumnasua na kifungo cha miaka 30 jela kwa kumbaka shemeji yake.

Badala yake, Mahakama Kuu imesema baada ya kuondoa mambo hayo katika uchambuzi wa kesi, ushahidi uliobaki bado ulikuwa wa kutosha kuthibitisha kosa la ubakaji bila shaka yoyote inayoweza kueleweka.

Mhera alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na Mahakama ya Wilaya ya Moshi baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka shemeji yake, lakini hakuridhika na uamuzi huo na akakata rufaa Mahakama Kuu akitaka hukumu hiyo itenguliwe.

Katika rufaa yake, alidai Mahakama ya Wilaya ilifanya makosa katika kuchambua ushahidi, ilitegemea ushahidi dhaifu na unaopingana, pia ilihamisha mzigo wa kuthibitisha kesi kutoka kwa upande wa mashtaka kwenda kwake.

Hukumu iliyothibitisha adhabu hiyo ya miaka 30 jela imetolewa Julai 21, 2026 na Jaji Adrian Kilimi aliyekuwa akisikiliza rufaa hiyo ya jinai namba 23327/2026 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Amesema Mahakama ya Wilaya ilifanya dosari katika uchambuzi wa baadhi ya ushahidi, lakini dosari hiyo haikuathiri ushahidi wa msingi uliothibitisha kosa dhidi ya Mhera.

Jaji amesema Mahakama ya Wilaya ilitaja katika hukumu yake baadhi ya maelezo ambayo hayakuonekana katika ushahidi uliorekodiwa, ikiwemo madai kwamba Mhera alimuuliza mwathiriwa kama alikuwa amekubali kufanya naye ngono na pia kwamba alikiri kuwa mwathiriwa alikuwa amekubali tendo hilo.

Hata hivyo, Jaji Kilimi amesema baada ya kupitia rekodi ya kesi, hakukuwa na ushahidi wa swali hilo wala jibu lake katika mahojiano ya Mhera na mwathiriwa.

“Baada ya kuchunguza kwa makini kesi, naona kwamba swali wala jibu lolote halionekani wakati mrufani alipokuwa akimhoji mwathiriwa,” amesema.

Kuhusu madai ya kukiri, Jaji amesema ushahidi huo ulitolewa na ofisa wa uchunguzi aliyedai kuwa Mhera alikiri wakati wa mahojiano kwamba alifanya ngono na mwathiriwa kwa sababu walikuwa wamekubaliana, na kuwa hakuna ungamo lililorekodiwa lililowasilishwa mahakamani kuthibitisha madai hayo.

Jaji amesema ushahidi huo ulibaki kuwa wa kusikia kutoka kwa mtu mwingine kwa kuwa haukuungwa mkono na hati au ushahidi mwingine unaokubalika.

Licha ya dosari hizo, Jaji amesema Mahakama Kuu ilipaswa kuangalia kama ushahidi uliobaki ulikuwa wa kutosha kuthibitisha kosa dhidi ya Mhera.

Tukio hilo lilidaiwa kutokea Juni 25, 2025, katika eneo la Samanga, Wilaya ya Moshi, baada ya Mhera kwenda shambani na shemeji yake, aliyetajwa kwa jina la ‘NH’.

Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, wakati wakirejea kutoka shambani, Mhera alimshawishi mwathiriwa kufanya naye ngono, lakini alikataa.

Mwathiriwa alidai kuwa baada ya kukataa, alijaribu kukimbia, lakini Mhera alimpiga teke na kuanguka kwenye mtaro, kisha akamshika shingoni na kumwekea kitambaa mdomoni ili kumzuia kupiga kelele. Baadaye akamvua nguo kwa nguvu na kumbaka.

Baada ya kufika nyumbani, mwathiriwa aliripoti tukio hilo kwa dada yake, ambaye alilifikisha kwa kiongozi wa eneo hilo na baadaye polisi.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa uchunguzi wa kitabibu uliofanywa katika Hospitali ya Pasua ulibaini kupenya kwa kitu butu katika sehemu za siri za mwathirika wa tukio hilo.


Utetezi

Katika utetezi wake, Mhera alikana kumbaka shemeji yake na kudai mwathirika wa tukio hilo alikuwa na chuki dhidi yake, jambo alilodai ndiyo sababu alimshtaki.

Aidha, alipinga ushahidi wa kitabibu uliotolewa dhidi yake akisema daktari hakubaini kuwepo kwa mbegu za kiume katika uchunguzi wa mwathirika wa tukio hilo na kudai hiyo inathibitisha hakukuwa na ubakaji.

Mahakama ya Wilaya ya Moshi haikukubaliana na utetezi huo na ilimtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka 30 jela.


Rufaa

Katika rufaa yake, mrufani huyo aliendelea kudai ushahidi wa mashtaka ulikuwa dhaifu, unaopingana na haukuwa wa kuaminika kiasi cha kuthibitisha kosa hilo.

Katika rufaa hiyo, Wakili wa Serikali aliomba Mahakama itupilie mbali rufaa hiyo akisema ushahidi wa mashahidi wa mashtaka ulikuwa thabiti na wa kuaminika.


Uamuzi Mahakama

Jaji Kilimi amesema baada ya kupitia upya ushahidi, Mahakama imejiridhisha kuwa mwathiriwa alitoa ushahidi wa kuaminika kuhusu namna alivyopigwa, kuzuiwa kupiga kelele, kuvuliwa nguo kwa nguvu na kubakwa.

Amesema ushahidi huo uliungwa mkono na ushahidi wa kitabibu pamoja na hatua ya mwathiriwa kuripoti tukio hilo mara baada ya kufika nyumbani.

Jaji amesema mwathiriwa alimfahamu Mhera vizuri kwa kuwa alikuwa shemeji yake, hivyo uwezekano wa kumtambua mtu mwingine kimakosa haukuwepo.

“Katika hali zilizotajwa, nakubaliana na uamuzi wa mahakama ya mwanzo kwamba upande wa mashtaka ulithibitisha kesi yake bila shaka yoyote inayoweza kueleweka,” amesema.

Amesema utetezi wa Mhera ulikuwa wa kukana tu kuhusika katika kosa hilo na haukuweza kuibua shaka yoyote dhidi ya ushahidi wa upande wa mashtaka, hivyo kutupilia mbali rufaa hiyo.