Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyehoji mkataba wa Bandari Dar ajisalimisha kwa mahakama

Dar es Salaam. Mwananchi aliyekuwa amefungua kesi Mahakama Kuu Dar es Salaam akihoji mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii, kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai (Inter-governmental Agreement-IGA), amejisalimisha kwa Mahakama baada ya kuiomba iitupilie mbali kesi yake hiyo.

Kesi hiyo ya namba 8 ya mwaka 2023 ilikuwa imefunguliwa na Fredrick Anthony Mboma Mahakama Kuu Masjala Kuu Dar es Salaam, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Hata hivyo, Mboma amejisalimisha mwenyewe kwa mahakama hiyo baada ya kuiomba iitupilie mbali kesi yake hiyo, baada ya uamuzi wa kesi nyingine kama hiyo iliyokuwa imefunguliwa Mahakama Kuu Majala Ndogo Mbeya.

Kesi hiyo ya awali namba 5 ya mwaka 2023 ilikuwa imefunguliwa na Alphonce Lusako na wenzake watatu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Katibu wa Bunge la Tanzania, iliyoamuriwa Agosti 10, mwaka huu.

Hata hivyo, tofauti na kesi ya awali ya kina Lusako Mbeya, iliyotupiliwa mbali na Mahakama baada ya kuisikiliza madai ya msingi, na kutoa hukumu kuwa madai yao hayakuwa na mashiko, Mboma ameiomba Mahakama hiyo iitupilie mbali kesi yake kabla hata ya kufika hatua ya usikilizwaji wa madai ya msingi.
 

Alifikia uamuzi huo wa kujihukumu kwanza mwenyewe kabla ya kusubiri uamuzi wa mahakama kwa kujipendekezea uamuzi huo, akitumia hukumu ya kesi hiyo ya Mbeya.

Mboma alifikia uamuzi huo kwa kutumia kanuni ya kisheria inayozuia suala lililokwishaamuriwa katika kesi ya awali kufunguliwa tena mahakamani kama kesi ya msingi, isipokuwa kwa njianya rufaa au mapitio inayojulikana katika taaluma hiyo kama res judicata.

Mahakama hiyo baada ya kusikiliza hoja zake pamoja na za mlalamikiwa, Serikali kupitia kwa AG, ambaye aliunga mkono maombi hayo, ilikubaliana na maombi hayo ya Mboma na kutoa amri ya kuitupilia mbali kesi hiyo, Alhamis, Agosti 17, 2023.

Mahakama hiyo ilikubaliana na maombi na hoja za pande zote mbili ikisema kesi hiyo inakidhi vigezo vya kisheria kuwa res judicata kulingana na msingi wa hoja na au madai kuwa sawa na kesi ya kina Lusako, kama ambavyo kifungu cha 9 cha Sheria ya Kanuni za Mwenendo wa Madai (CPC).

Uamuzi huo ulitolewa na jopo la majaji watatu, Dunstan Ndunguru (Kiongozi wa jopo) Mustafa Ismail na Abdi Kagomba, ambao pia ndio walioisikiliza na kuamua kesi ya kina Lusako, Mbeya.

Hivyo Mahakama hiyo ilisema kwamba uamuzi katika kesi ya awali ya kina Lusako kuhusiana na uhalali wa Kikatiba wa kesi hiyo unamfunga na mlalamikaji  katika kesi ya sasa, Mboma.

"Matokeo yake, shauri hili linatupiliwa mbali", imesema Mahakama hiyo katika uamuzi wake huo baada ya kujadili hoja za pande zote katika mizania ya kisheria na kuhitimisha kuwa kwa kuwa shauri hilo linahusu maslahi ya umma haitoi amri kuhusu gharama bali kila upande utabeba gharama zake wenyewe.

Pamoja na hoja nyingine kesi zote hizo mbili zilikuwa zikihoji uhalali wa mkataba huo unaohusu uwekezaji katika Bandari za kwenye baharini na maziwa pamoja na miundombinu yake nchini Tanzania, maeneo ya maegesho na maeneo ya kibiashara.

Mboma katika kesi hiyo alikuwa aliomba Mahakama itoa amri kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa nakala ya mkataba ulioridhiwa, itamke kama IGA hiyo ni Mkataba, Mdaiwa (Serikali ) kueleza kama baada ya kuridhiwa Sasa IGa ni Mkataba wa Kimataifa au la na kama ni Sheria Sheria ya Bunge au la.

Pia aliomba mdaiwa kueleza kuwa kama bado si mkataba au Sheria ya Bunge ni kwa nini,  na pia aliiomba Mahakama itamke kama IGA( mkataba) huo unakiuka Ibara 9 (b-d), 9(I) (k), 25(1), 25(3) (d) (III), 27(2), 9(h) ilisomwa pamoja na 4(3)sehemu ya 11 kuhusiana na mambo ya Muungano. 

Kwa upande wao8 kina Lusako walikuwa  wanapinga mkataba huo wakidai kuwa ni batili kwa kuwa masharti ya baadhi ya Ibara zake  yanakiuka Sheria za Nchi za Ulinzi wa Raslimali na Maliasili za Nchi na Katiba ya Nchi.

Vile vile walikuwa wanadai kwamba yanahatarisha mamlaka ya Nchi na usalama wa Taifa na kwamba yaliridhiwa na Bunge kinyume cha utaratibu bila kuwapa nafasi ya kutosha wananchi kutoa maoni yao.

Hata hivyo Mahakama hiyo katika hukumu yake ilibainisha kasoro kadhaa katika mkataba huo, unaohusu uwekezaji katika Bandari za bahari na maziwa, ikiwemo kukiuka   Sheria namba 5 na 6 za mwaka 2017 za Ulinzi wa Raslimali na Maliasili za Nchi.

Pia ilikubaliana na walalamikaji kuhusu ushirikishwaji wa wananchi kuwa mchakato huo ulikuwa na kasoro ikiwa ni pamoja na kitokutoa muda wa kutosha kwa wananchi kwenda kutoa maoni.

Hata hivyo, ilisema kuwa siyo kasoro ya kuufanya mkataba huo kuwa batili.

Hivyo ilihitimisha kuwa mkataba huo haukiuki Katiba na au vifungu vya Sheria zilizotajwa (za Mikataba na Manunuzi ya Umma) wala kupoka uhuru na mamlaka ya Tanzania katika kutumia Raslimali asili bila kuingiliwa na nchi wala kuhatarisha usalama wa Nchi kama walalamikaji walivyokuwa wakidai.

Hivyo iliitupilia mbali kesi hiyo ikisema kuwa hoja za walalamikaji hazina mashiko