Ajali za pikipiki bado tishio kwa Tanzania, Afrika

Uzinduzi wa kampeni ya Mpango wa Safiri Salama na Usalama wetu kwanza ya mkoani Njombe Mei 28, 2021. Katika tukio hilo, elimu ilitolewa kwa madereva wa pikipiki na bajaji.
Muktasari:
- Matukio ya ajali za barabarani yanashika nafasi ya nane duniani kwa kusababisha vifo.
Matukio ya ajali za barabarani yanashika nafasi ya nane duniani kwa kusababisha vifo.Na hii kwa kiasi kikubwa inasababishwa na namna matukio hayo yanavyotokea kwa kuogofya mara kwa mara, siku baada ya siku, pengine hata saa baada ya saa.
Pia takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 40 ya waathirika wa ajali za barabarani ni watembea kwa miguu nchini huku asilimia 60 ikibakia kwa watumiaji wengine wa barabara kama vile waendesha bodaboda, baiskeli na magari.
Kinachostaaajibisha wengi kwa miaka ya hivi karibuni matukio ya ajali zitokanazo na pikipiki (maarufu kama ‘bodaboda’) ni mengi zaidi kuliko yale yatokanayo na vyombo vingine vya moto.
Biashara ya pikipiki ni moja ya sekta muhimu za usafiri nchini ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kupunguza changamoto ya foleni nyakati ambazo tutahitaji kufika katika maeneo ya kazi, shule, hospitali, michezoni nk.

Kamanda wa Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, Wilbroad Mutafungwa akiwa katika moja ya vikao na wadau wa usafirishaji na usalama barabarani.
Ni usafiri rahisi na pendwa miongoni mwa watu wengi kwa uwezo wake wa kuwafikisha kule wanakoelekea kwa haraka zaidi licha ya miaka ya karibuni kuonekana kuwa si salama kulingana na mambo mbalimbali.
Barabara zimekuwa machinjio ya waendesha bodaboda wasio makini na hata wale wanaojitahidi kumakinika. Na hili linaufanya usafiri huo ulioajiri idadi kubwa ya Watanzania wa kipato cha chini kuwa si salama zaidi.
Kulingana na tafiti, wanaume ni wahanga wakubwa wa matukio ya ajali za bodaboda kwa kuwa hulazimika kutumia muda mwingi na nje ya masaa ya kawaida ya kazi, kutafuta riziki zao wakiwa barabarani baada ya kuhakikisha wameshakamilisha mahesabu ya mmiliki wa chombo.
Tatizo hilo si tu limekuwa janga la Taifa bali limeendelea kuwa tishio na kuathiri nchi nyingine za ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Moja ya sababu za ajali ni tabia ya baadhi ya madereva pikipiki hao kutokufuata matumizi sahihi ya barabara na sheria zinazoongoza usalama barabarani kuwa moja ya sababu hatarishi za ajali hizo.

Uzinduzi wa kampeni ya Mpango wa Safiri Salama na Usalama wetu kwanza ya mkoani Njombe Mei 28, 2021. Katika tukio hilo, elimu ilitolewa kwa madereva wa pikipiki na bajaji.
Kwa tafsiri rahisi, kutokufuatwa kwa sheria hizo za usalama barabarani kunahusisha kutokuvaa kofia ngumu (helmet) kwa madereva wengi, tabia ya kupakia abiria zaidi ya mmoja (mishikaki), matumizi ya vileo, kutokupitia mafunzo rasmi ya uendeshaji pikipiki nk.Zipo sababu nyingine ambazo hazipewi nafasi kubwa lakini ni miongoni mwa vyanzo vya ajali za pikipiki.
Suala la miundombinu kwa baadhi ya maeKariakoo eneo ambalo limebanana kiasi cha watumia barabara kukosa nafasi ya kupita na kusababisha ajali wakati mwingine.
Mitazamo ya visababishi vya ajali za pikipiki hata kwa madereva bodaboda imegawanyika miongoni mwao. Wapo wanaokubali huwa zinatokana na uzembe wao na wanaosema kuwa huwa wanasababishiwa.
Mwenyekiti Mstaafu wa Kituo cha Bodaboda cha Mwananchi, Rashid Mwanga ambaye ana uzoefu wa miaka 10 ya biashara ya pikipiki yeye anaamini kuwa ajali hutokana na mambo yote mawili, uzembe na wakati mwingine kusababishiwa.
Akielezea matukio ya ajali aliyoyapata na hatakaa kuyasahau, ambayo baadhi ni ya kujitakia na mengine ya kusababishiwa, anaikumbuka kwa karibu zaidi ajali aliyoipata maeneo ya Tabata Bima.“Unajua ukiwa barabarani huku umetawaliwa na mawazo mengi basi unaweza ukajisahau.
Nilikuwa nimepakia abiria wangu mmoja naelekea naye Segerea, wakati nakaribia njia pacha ya kwenda Kimanga na Segerea nikiwa katika mwendokasi nilijikuta nahamasika kulivuka gari ambalo lilishanionyesha kuwa linakuja uelekeo wangu hivyo nikaligonga na kuanguka chini.
Kwa kuwa nilikuwa nimevaa kofia ngumu niliteleza kwa kichwa mpaka mtaroni.”Mwanga anakiri kuwa sehemu kubwa ya ajali hiyo anaona ni uzembe wake na alichubuka kidogo mwilini.
“Kitu kingine nachomshukuru Mungu abiria wangu yule alifanikiwa kuruka mapema alivyoona kuwa chombo kinapoteza uelekeo.”
Anasema pia alishawahi kupata ajali maeneo ya Tazara wakati daraja la juu la Mfugale likiwa katika hatua za mwisho za ukamilikaji.
Mwanga anaongeza zaidi kuwa watu wa daladala nao kwa asilimia kubwa wanachangia kuwapo kwa ajali za pikipiki nchini.
Katika mahojiano hayo anaeleza sababu zinazochangia kuongezeka kwa ajali za pikipiki ikiwamo; umakini mdogo miongoni mwa waendesha bodaboda, kutokuzingatia kanuni za usalama barabarani, elimu ndogo miongoni mwa waendesha bodaboda nk.
Naye Katibu wa Kituo cha Bodaboda cha Mwananchi, Mwita Magele anasema ana uzoefu wa miaka 7 katika biashara hiyo na anakiri kuwahi kupata ajali japo ni zile ndogo ndogo na anadhani kuwa ajali zitaendelea kuwepo kwa sababu ya kundi dogo miongoni mwa waendesha bodaboda kutokutaka kutii sheria na kanuni za usalama barabarani.
“Unajua sisi bodaboda tunaonekana wahuni na tunadharaulika kutokana mienendo na tabia zetu na hii ndiyo sababu wakati mwingine ya kupata ajali za mara kwa mara,” anaeleza zaidi.
Katika upande mwingine, Magele anaamini kuwa hata maofisa wa usalama barabarani wakati mwingine nao ni chanzo cha ajali kwa kuwa baadhi ya waendesha bodaboda wanaohisi kuwa na makosa kujaribu kuwakwepa maofisa hao na kwa sababu matukio hayo hufanywa katika mazingira hatarishi zaidi, inasababisha ajali kutokea.
Magele, katika nafasi yake ya ukatibu ambayo ameihudumu mara mbili katika vipindi viwili tofauti, anasema, “sisi katika kituo chetu cha Mwananchi huwa tunamuomba Mungu sana na kwa kweli kumekuwapo na majanga madogo madogo na katika miaka saba ya uongozi hatujawahi kupata tukio la ajali lililosababisha kifo ispokuwa kuvunjika kwa mguu kwa mwenzetu mmoja,” anaeleza.
Taasisi ya Tiba za Mifupa ya Muhimbili (MOI) imekuwa ikipokea majeruhi si chini ya 10 mpaka 15 kwa siku wa ajali zinazohusisha pikipiki.Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kufikia hadi majeruhi 20 kwa siku kunapokuwepo kwa matukio rasmi makubwa ya kiserikali yanayokusanya idadi kubwa ya watu, mpira nk.
Kulingana na uzoefu, ajali hizo zimekuwa zikisababisha majeraha kwa zaidi ya mtu mmoja (kwa maana dereva, abiria na mtu wa tatu kutoka katika chombo kingine kilichohusika na ajali).
“Wengi wanapata majeraha ya aina mbalimbali yanayohusisha miguu, kiuno, kichwa, kifua wakati mwingine na inategemea ajali hiyo imetokana na nini; wakati mwingine ni pikipiki kwa pikikipi zinagongana, wakati mwingine pikipiki kwa gari na pia, pikipiki kwa waenda kwa miguu,” anaeleza Dk Kennedy Nchimbi kutoka Taasisi ya Tiba za Mifupa Muhimbili (MOI).
Pia, anasema kuwa wengi wao hupata majeraha ya kuvunjika mfupa wa mguu ambao unakuwa na kidonda.
Majeruhi wengi hufikishwa kwa dharura, wapo wale ambao wanashindwa kupatiwa matibabu katika mikoa yao husika na kupelekwa MOI na wengine hutibiwa na hospitali zingine za serikali za rufaa kama vile Hospitali ya Temeke, Mwananyamala na Amana.
Hali hiyo inasababisha kuwe na mlundikano wa wagonjwa ukizingatia wengi wao hupata majeraha makubwa ambayo matibabu yake pengine yanahitaji siku nyingi kuweza kuwarudisha katika hali zao za kawaida.
Akijibu swali kuhusiana na uwezekano wa majeraha hao kupata maambukizi kutokana na vidonda baada ya ajali, Dk Nchimbi anasema ajali inatokea barabarani na kwa mfano mtu anagongwa halafu anatumbukia katika mtaro wa maji machafu (yawe ya mvua au yale yanayohusisha vyoo) na mkono wake uliopata jeraha ukagusa maji hayo, inaweza kusababisha jeraha kuwa kubwa zaidi na hata mtu huyo kupoteza mfupa wa mkono.
Majeraha mengine yanayoweza kumpata mtu ni katika kiuno kumbuka unapokuwa katika bodaboda unakuwa umekaa umetanua miguu, na mko watatu hadi wanne, unaweza ukapata jeraha baya zaidi la kupoteza kikombe cha kiuno inapotokea ajali kwa sababu mwendo wa pikipiki na mwendo wako unakuwa sawa wakati pikipiki inatembea.
Kwa mtu aliyepata jeraha la kuvunjika kiuno hata kama atatibiwa bado yuko katika hatari ya kupata ulemavu wa kudumu kama vile kushindwa kufanya shughuli zingine za kimwili kama vile kushiriki tendo la ndoa, kushindwa kutembea kama hapo awali.
Wapo ambao wanapata ajali na kupata maambukizi kutoka eneo alilopatia ajali kupitia kidonda mguuni na baadaye mguu huo kuathirika kiasi cha kutaka kuoza na hivyo taratibu za kuukata mguu zitachukuliwa.
Inawezekana pia wakati mwingine mtu anapata maambukizi ya vijidudu ambavyo vinakwenda katika damu na kuathiri eneo fulani ambalo litashindwa kufanya kazi kwa baadaye na kupoteza moja kwa moja kiungo hiko.
Kutokuvaa kofia ngumu maana yake unatumia kichwa kama ngao, na ipotokea umerushwa na kwenda kugonga eneo fulani utapata maumivu ya kichwa yatakayosababisha damu kuganda kichwani na mwishowe kupata changamoto ya uzezeta.
Kwa jicho lingine, ajali za barabarani zina athari kubwa za kijamii na kiuchumi. Kulingana na Dk Kiwango, miongoni mwa athari hizo ni upotevu wa mali, uharibifu wa miundombinu, kupungua kwa nguvukazi katika uzalishaji mali, ulemavu wa kudumu, nk.Katika miaka michache iliyopita, Serikali na wadau wake wengine wamekuwa macho katika eneo hili la ajali za barabarani.
Jambo ambalo limesababisha leo kuwapo kwa jitihada mbalimbali za kudhibiti biashara ya usafiri wa bodaboda ili kupunguza ajali; ikiwamo mafunzo kwa waendesha bodaboda hususan kwa wale ambao hawakupata mafunzo rasmi.Sambamba na jitihada, pia Serikali iliweka katazo la uuzwaji wa pombe za katika vifungashio vya plastiki (viroba) ambazo zilikuwa zikitumiwa aghalabu na waendesha bodaboda wengi na kuhatarisha usalama wa abiria, na wakati mwingine kusababisha ajali.
Kampeni ya kudhibiti matumizi ya pombe iliyofanyika wilayani Moshi chini ya Dk Kiwango, Mkoa wa Kilimanjaro ni moja ya mikakati hiyo.
Pia, ipo mikakati ya uboreshaji wa mifumo ya ukusanyaji wa taarifa za ajali za pikipiki.MOI nayo kupitia wawakilishi wake wa afya wamekuwa wakipitia vituo vya bodaboda na kutoa elimu kwa kundi hilo.
Anaeleza kuwa wameshafanya hayo katika maeneo ya Kinondoni, Ubungo na Magomeni lakini pia wamekuwa wakitoa elimu mahususi kwa wagonjwa wenyewe kwa kuwa wao ndiyo walengwa namba moja licha ya wagonjwa wengi kutokusikiliza elimu hiyo kutokana na kuugulia maumivu ya majeraha waliyoyapata.
Majeruhi kutoka MOI na sehemu zingine huelezwa athari ya kutokuzingatia sheria za usalama barabarani na kuwashauri nini wanatakiwa kufanya baada ya matibabu yao.
Magele anathibitisha kuwa kituo chao ni moja ya vituo bora na vya mfano kwa kuwa asilimia kubwa ya wanachama wana mafunzo muhimu ya usalama barabarani kwani kupitia viongozi wa mkoa wa waendesha bodaboda waliweza kuomba mafunzo hayo kutoka kwa Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani.
Hivyo anasema fursa za mafunzo zipo lukuki huku akitolea mfano wa Chuo cha Ufundi cha Polisi, Kurasini pia kuendesha mafunzo ya aina hiyo kwa wanaohitaji.
“Hapa katika kituo chetu, asilimia kubwa ya waendesha bodaboda wanamiliki vyeti vya kuhitimu mafunzo.”Kama hiyo haitoshi, na kwa kuwa tatizo hili linahitaji nguvu ya pamoja, Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani limeendesha programu za mafunzo kwa zaidi ya madereva 500 na kupatiwa vyeti wilayani Makambako, Njombe.
Pia, limefanya kwa Mkoa wa Mbeya kwa kuwafundisha madereva zaidi ya 300.Hatua hizo miongoni mwa nyingine nyingi zimezaa matunda kwani idadi ya matukio ya ajali zitokanazo na pikipiki zimepungua.
Idadi ya majeruhi wawili wa ajali za pikipiki waliokuwa wakifikishwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa siku mwaka 2015-16 imepungua na hatimaye kufikia majeruhi mmoja kwa siku hospitalini hapo mwaka 2019.
Bado kuna imani kubwa kuwa idadi hiyo itaendelea kushuka.Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani inayo mezani mikakati mitatu kabambe ya kukabiliana na tatizo la ajali za barabrani hususan za pikipiki.
Kamanda wa Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, Wilbroad Mutafungwa anasema mkakati wa kwanza mkubwa ni zoezi la kuendelea kutoa elimu kupitia madawati ya elimu.
Mkakati wa pili ni ushauri endelevu kwa waendeshabodaboda kwa kuwaambia nini wanapaswa kukifanya wanapohitimu mafunzo kwa maana ya faida na hasara za kutokufuata sheria za usalama barabaani.
Mkakati wa tatu na wa mwisho, anasema ni kusimamia sheria zenyewe.
Na tayari Jeshi hilo linaendelea na operesheni mbalimbali nchini ya kukamata pikipiki zinazokiuka utaratibu na kuzifungulia mashtaka na kisha kuzipeleka mahakamani.
Kamanda anafafanua kuwa kasumba iliyojengeka miongoni mwa watu wengi kuwa madereva wa vyombo vingine vya moto huweza kubadili mienendo wanapokabidhiwa pikipiki si kweli kwani kama dereva anatii sheria za usalama barabarani bado ataendelea kufanya hivyo bila ya kujali ni chombo gani anakitumia kwa wakati huo.
Anasema hao ambao wanaamini hivyo ni kati ya wale madereva wachache wakaidi na hawana nia njema.
Kulingana na utafiti uliofanywa, kuna maeneo mengi ambayo kama nchi tunaweza kuboresha ikiwamo kuangalia namna ya kudhibiti tabia hatarishi za waendesha bodaboda wengi kuendesha kwa kutozingatia usalama, ulevi wakati wa kuendesha na suala la mikataba na waajiri wao ambalo linawalazimu kutumia muda mrefu kufikisha hesabu za mwajiri na zake binafsi.
Kuna fursa ya kuboresha huduma kwa majeruhi wa ajali za pikipiki baada ya kutokea kwa ajali, ukusanyaji wa taarifa zao na ujengaji uwezo kwa huduma za kwanza kwa majeruhi hao katika ngazi ya jamii.
Ili kukabiliana na ajali za pikipiki, bado kuna umuhimu wa kuendeleza tafiti hizo ili kutambua, kuboresha na kudhibiti michakato yetu kwa wakati wote.
Pia, kwa upande wa Serikali, wadau wanaeleza uhitaji wa kuwapo kwa sera na mifumo ambayo itasaidia kuweka mfumo utakaosaidia waendesha bodaboda kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa na usalama zaidi.
Mwenyekiti wa Waendesha Bajaji Kituo cha Mwananchi, ambaye kabla ya kuhamia katika biashara hiyo ya sasa aliwahi kuendesha bodaboda, Japhet Kamuga anaufananisha mfumo wa uendeshaji biashara ya usafiri wa bodaboda kama ulivyo ule wa elimu hapa nchini.
Kamuga ambaye ana uzoefu wa miaka 10 wa biashara ya bodaboda anasema tangu usafiri huo uingie hapa nchini hakukuwapo na mfumo mzuri wa kuusimamia na ndiyo sababu ajali nyingi zinatokana na usafiri huo kwa sasa.
“Tulioupokea ghafla, tukaishi nao na ndiyo maana sasa unatutesa kwa sababu ya kutokuwekea misingi imara.”Anasema kuwa leo hii ukimchukua dereva mwenye leseni C kutoka NIT ambaye anafuata sheria zote za usalama barabarani na ukaamua kumpa pikipiki aendeshe, unaweza ukashangaa anavyobadilika ghafla kwa kuwa dereva asiyetii sheria wala kanuni za usalama barabarani ndani ya muda mfupi.
Anaendelea kusisitiza kuwa kwa bahati mbaya biashara hii wakati inaingia hapa nchini vijana wengi ambao hawakuwa na ajira ndiyo walioikimbilia akibainisha kuwa ni zaidi ya asilimia 80 ya kundi hilo.
“Kwa hiyo mimi niseme hili janga limeikumba nchi yetu tayari ambapo hata elimu itolewe kwa kiasi gani lakini bado madereva bodaboda wataendelea kubakia na mienendo yao ile ile ya siku zote,” anahitimisha kwa kutoa maoni yake.
Na kwa hayo yote yaliyofanyika tunaanza kuona taratibu wananchi wameanza kuelewa zaidi kuhusu sababu za matukio ya ajali za pikipiki, mgawanyiko wake na njia bora za kuboresha huduma kwa majeruhi wa ajali kwa kadri wanavyoendelea kufanya tafiti.
Kuhusu watafiti
Kutokana na ukubwa wa changamoto hiyo inayotafuna nguvukazi ya Taifa, iliwaleta pamoja watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dk George Kiwango ambaye alifanya utafiti katika eneo la ajali za barabarani zitokanazo na pikipiki na Dk Menti Ndile ambaye yeye amejikita katika utafiti wa kuhudumia majeruhi wa ajali za barabarani.
Kwa upande wa Dk George Kiwango ambaye alikuwa anafanya utafiti katika Shahada ya Uzamili (Master’s Degree) chuoni MUHAS.Anakiri kuwa kufanya kazi na wadau wa masuala ya utafiti wa ajali za barabarani kutoka nje ya nchi, kulibadilisha mawazo yake na kuanzia hapo akajikuta anasoma zaidi kuhusiana na ajali za barabarani na kuangalia njia gani ambazo zinaweza kutumika kutafutia ufumbuzi.Dk Kiwango anasema hali imebadilika ambapo waendesha pikipiki ndiyo wamekuwa wahanga wakubwa wa ajali baada ya watembea kwa miguu.
Anathibitisha kuwa hata Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, mwanzoni haikuwa ikipata majeruhi wa ajali za bodaboda, baadaye ikaanza kupata majeruhi wengi na hapo ndipo ilimsukuma kujikita zaidi katika utafiti za ajali za pikipiki. Miaka mitatu ilimchukua Dk Kiwango kuufanya na kuukamilisha utafiti huu yaani kuanzia 2017-2020.
Kama hiyo haitoshi, aliona mfumo wa usafiri wa pikipiki umekuwa mkubwa na tegemeo la watu wengi na kwa kuwa utaendelea kuwapo kwa miaka mingi hivyo ilimlazimu kutafuta njia za kuboresha ili uwe msaada kwa watumiaji wake ambao wengi ni wananchi wa kawaida.
Kwa upande wa Dk Menti Ndile, ambaye ni mtafiti na mhadhiri pia kutoka MUHAS, alivutiwa kuchukua Shahada ya Uzamivu (PhD) katika masuala ya utoaji huduma kwa majeruhi wa ajali za barabarani kutokana na ongezeko la majeruhi na vifo vya ajali za barabarani.
Shahada yake ya uzamivu aliichukulia MUHAS na Chuo Kikuu cha Umea nchini Sweden kwa kipindi cha miaka minne akishirikiana na mhadhiri msaidizi Gift Lukumay kutoka MUHAS.Anasema matukio ya ajali ya barabarani yamekuwa yakiongezeka na anakiri kuwa Tanzania haijaachwa nyuma.
Dk Ndile anataja moja ya mambo yanayosababisha ajali za barabarani ni hali ya miundombinu. Zingine ni elimu ndogo, kutokuzingatia kanuni za usalama barabarani, ongezeko la watu na vyombo vya moto ambalo limekuwa kisababishi cha matukio ya ajali, vyombo vya moto vibovu nk.
“Matukio hayo ya ajali za barabarani ya pikipiki yamesabababisha majeruhi wa ajali kuhitaji rasilimali nyingi kwa ajili ya matibabu yao na ikiwa bado kama nchi hatuna rasilimali za kutosha kukidhi matakwa yanayoongezeka kila siku,” anaeleza Dk Ndile.
Watafiti hawa bado ni hazina kubwa kwa taifa kwani eneo la ajali za barabarani hususan pikipiki bado ni miongoni mwa maeneo yasiyofanyiwa tafiti mara kwa mara.
Hitimisho
Kutokana na matokeo ya tafiti, inapendekezwa kuwapo kwa mikakati mbalimbali ya kurekebisha tabia na kudhibiti tabia hatarishi miongoni mwa waendesha bodaboda.
Pia, sambamba na hilo, kutokana na ukweli kuwa matumizi ya vilevi yamekuwa sababu kubwa ya matukio ya ajali za bodaboda, hivyo inashauriwa kuwepo kwa njia za kudhibiti matumizi ya pombe na vilevi vingine kwa ajili ya kuzuia ajali kwa siku za usoni.
Kwa upande wa huduma za tiba kwa majeruhi, ni wakati wa kuhamasisha zaidi tafiti katika eneo hili ili kuona kama huduma zinazotolewa kwa majeruhi wa ajali za bodaboda zinawasaidia walau kurejea katika hali zao za kawaida kama si kupona kabis