Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ajali yaua sita, watatu viongozi CCM

Muktasari:

  • Watu sita wafariki dunia kwa ajali wakiwepo viongozi watatu wa UWT ngazi za Kata, waliokuwa wakisafiri kutoka kwenye mkutano uliokuwa umeitishwa na Mlezi wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Njombe, Halima Mamuya.

Mbeya. Watu sita wamepoteza maisha wakiwemo viongozi watatu wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) na wengine ni abiria baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupinduka katika kijiji cha Ndulamo Wilaya ya Makete Mkoa wa Njombe.

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, John Imori, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambapo amesema waliofariki kuwa ni wanawake watatu na wanaume watatu.

Amesema ajali hiyo imetokea saa 11 za jioni katika eneo lenye kona kali katika Kijiji cha Ndulamo ambapo gari aina ya Toyota Hiace ilikuwa ikitokea Wilaya ya Makete kwenda Tandala ilipofika kwenye kona ilimshinda dereva ndipo lilipinduka na kusababisha vifo majeruhi.

“Gari hiyo ilibeba abiria 18, kati ya hao sita wamepoteza maisha huku majeruhi 11 wamekimbizwa hospitali kwa matibabu zaidi, huku chanzo cha ajali ni mwendo kasi na dereva kushindwa kulimudu gari hilo alipofika katika eneo lenye kona na mteremko mkali,” amesema.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Juma Mfanga amesema wamepokea majeruhi 11 huku wengi wao wakiwa wamevunjika maeneo kadhaa ya miili yao na kwamba wanaendelea na matibabu katika Hosptali za Wilaya ya Makete na Ikonda.

Mlezi wa Chama na Mjumbe wa Kamati Kuu CCM, Halima Mamuya ametoa pole kwa familia za watu aliopoteza maisha na majeruhi na kwamba ajali hiyo ni pigo.

“Wakati ajali inatokea, Mkutano ulikuwa umekwisha huku akibainisha waliopoteza maisha walikuwepo kwenye mkutano na kupata fursa ya kuzungumza na ilikuwa ni kauli zao za mwisho...nashukuru kwa uharaka wa upatikanaji wa huduma kwa majeruhi na kuwahifadhi waliopoteza maisha,” amesema.

Pia imeelezwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka ametoa pole kwa familia na kwamba Serikali itagharamia matibabu kwa majeruhi wote 11 sambamba na taratibu zote za maziko kwa waliopoteza maisha .