Ajali ya lori, Coaster yaua wanane, kujeruhi Handeni

Muktasari:
- Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amethibitisha kutokea kwa ajali leo Desemba 24, 2024, saa 11:00 asubuhi, Kitongoji cha Kwachuma, Kata ya Segera, Wilaya ya Handeni, Barabara Kuu ya Segera-Chalinze
Handeni. Watu wanane wamefariki dunia na wengine kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha lori na Toyota Coaster iliyotokea Kijiji cha Michungwani, Kata ya Segera wilayani Handeni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo leo Desemba 24, 2024, saa 11:00 asubuhi, Kitongoji cha Kwachuma, Kata ya Segera, Wilaya ya Handeni, Barabara Kuu ya Segera-Chalinze.
Amewataja majeruhi katika ajali hiyo ni Godlisen Minja (20) mfanyabiashara na mkazi wa Mabibo Dar es Salaam, Riziki Mboya (28) dereva na mkazi wa Njiapanda Moshi, Lina Swai (25) mfanyabiashara, Gospan Lema (24) fundi umeme na mkazi wa Temeke, Dar es Salaam.
Wengine ni Loyce James (27) mkazi wa Buguruni Dar es Salaam, Lucy Urio (24) mkazi wa Dar es Salaam, dereva wa lori Yohana Stephano (35), mkazi wa Goba Dar es Salaam na utingo Samweli Hossen (24), mkazi wa Dar es Salaam.
Kamanda Mchunguzi amesema ajali hiyo imehusisha lori mali ya Kampuni ya Starling Gulf Trading likitokea Tanga kuelekea Dar es Salaam na basi dogo aina ya Toyota Coaster, mali ya Naman Joel Mkumbo likitokea Dar es Salaam kuelekea Kilimanjaro.
“Ajali ilitokea baada ya dereva wa Toyota Coaster kushindwa kulimudu gari lake na kuyumba kuelekea upande wa pili wa barabara, hali iliyosababisha kugongana uso kwa uso na lori,” amesema Kamanda Mchunguzi.
Majeruhi wote walipelekwa katika Hospitali ya Magunga, Wilaya ya Korogwe kwa ajili ya matibabu na miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Magunga kwa uchunguzi wa kitabibu na utambuzi wa ndugu.
Ametoa wito kwa madereva wote kuhakikisha wanazingatia sheria na kanuni za usalama barabarani wakati wote na si tu wanapoona askari polisi, ikiwa ni pamoja na kuendesha kwa mwendo unaoruhusiwa na kuzingatia matumizi sahihi ya alama za barabarani.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Instagram akisisitiza dereva akifika Kijiji cha Manga wilayani humo, asipofuata sheria za usalama barabarani asilaumu, kwa kuwa ajali zinaepukika.
“Ajali hii sababu ni uzembe wa dereva, kwa sababu ya kujirudia rudia kwa uzembe nimemuelekeza OCD (mkuu wa polisi wilaya) atakayekiuka Sheria ya Barabarani eneo la Handeni tutampandisha mahakamani na kuomba adhabu ya kifungo,” amesema Msando.
Pia, amewataka abiria kuacha kukaa kimya wakati dereva anaendesha hovyo, hivyo ashuke na atarejeshewa nauli yake na atoe taarifa kwa Jeshi la Polisi ili kuzuia uzembe huo.