Ajali Pwani, miili ya watu watano yatambulika, wanne bado

Muktasari:

Miili ya watu wanne kati ya tisa ya watu  waliopoteza maisha kwa ajali ya gari aina ya coaster kugongana uso kwa uso na lori mkoani Pwani, bado haijatambuliwa na ndugu zao.

Dar es Salaam. Maiti za watu watano kati ya tisa zilizohifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani kufuatia ajali iliyohusisha magari mawili yaliyogongana jana Jumapili, Machi 10,2024, imetambuliwa.

Ajali hiyo iliyotokea saa 11 jioni ikihusisha magari ya Toyota Coaster iliyokuwa ikisafirisha abiria kuelekea Bagamoyo mkoani Pwani na Fuso lililobeba mawe, yaligongana uso kwa uso huku chanzo kikitajwa ni uzembe wa dereva wa Fuso aliyejaribu kuyapita magari yaliyo mbele yake.

Akizungumza na Mwananchi leo  Jumatatu Machi 11, 2024, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, Luiyana Denis amesema miili ya watu wanne ndio haijapata ndugu.

"Kwa upande wa majeruhi mmoja tumebaki naye na anaendelea vizuri wawili tumewahamishia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani na hatujapata taarifa ya hali ya afya zao kuwa mbaya maana yake wanaendelea vizuri," amesema.

Mapema leo asubuhi akizungumza na Mwananchi Digital, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge alisema taarifa za awali zilionyesha kuwa dereva wa Fuso alikuwa anayapita magari yaliyo mbele yake eneo lisiloruhusiwa.


Amesema ajali hiyo ilitokea eneo la Kiromo wilayani Bagamoyo na dereva wa Fuso alikuwa akitokea Bagamoyo kuelekea Dar es Salaam.

Desemba mwaka jana mkoani Pwani,  Watu wawili walipoteza maisha na wengine 50  kujeruhiwa baada ya kutokea ajali ya basi dogo aina ya TATA lililokuwa likitokea Kigogo Dar es Salaam kuelekea Mloka Rufiji kupitia njia ya Kisarawe kupinduka na kutumbukia mtoni.