Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

AJALI PRECISION AIR BUKOBA: Abiria wadai fidia ya Sh7.2 bilioni

Muktasari:

  • Ni ajali iliyoua watu 19 wakiwamo marubani. Jaji atupa mapingamizi ya awali.

Dar es Salaam. Abiria wawili kati ya 39 waliokuwamo ndani ya ndege ya Precision Air iliyopata ajali mjini Bukoba, Mkoa wa Kagera na kuua watu 19, wamefungua kesi ya madai wakidai fidia ya zaidi ya Sh7.2 bilioni kutokana na madhara ya kiafya na kiuchumi waliyoyapata.

Katika ajali hiyo iliyotokea Novemba 6, 2022, ndege hiyo iliyokuwa ikitokea uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, ilikuwa na marubani wawili, abiria 39 na wahudumu wawili.

Abiria 17 na marubani wawili walifariki dunia na abiria 24 walinusurika kifo huku baadhi wakiwa na majeraha katika viwango tofautitofauti.

Kulingana na hati za madai, Nickson Kawiche anadai fidia ya Dola za Marekani 1,896,195 sawa na Sh5 bilioni  wakati Josephine Mwakisambwe akidai fidia ya Dola za Marekani 849,771 sawa na Sh2.28 bilioni.

Precision Air kupitia kwa wakili Gerald Nangi iliwasilisha mapingamizi ya awali, ingawa hata hivyo baada ya Jaji Hussein Mtembwa wa Mahakama Kuu masjala ya Dar es Salaam, kuyasikiliza aliyatupilia mbali.

Katika kesi mbili tofauti za msingi, wawili hao wanaeleza Novemba 6, 2022, walipanda ndege hiyo  iliyoondoka JNIA saa 12:10 asubuhi kuelekea Bukoba na ilitarajiwa kutua saa 2:25 asubuhi.

Kulingana na taarifa ya awali iliyotolewa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), marubani waliokuwa wakiendesha ndege hiyo,  walikumbana na hali mbaya ya hewa wakati ikikaribia uwanja wa ndege za Bukoba kutokana na mvua, dhoruba ya radi na uoni hafifu.

Ndege hiyo ilijaribu kutua na kushindwa ambapo iliahirisha kutua na kupaa umbali wa futi 5,500 kutoka usawa wa bahari lakini ikashuka hadi futi 5,300 na kusababisha vifaa maalumu uwanjani, kutoa alamu (alarm) ya kutahadharisha.

Kulingana na madai ya abiria huyo, saa 2:43 asubuhi wakati ikijaribu kutua katika uwanja huo wa Bukoba, ilitua meta 500 nje ya njia ya kutua ndege na kujipiga katika uso wa Ziwa Victoria huku eneo lote la mbele likimezwa kabisa na maji.

Eneo la katikati la abiria na nyuma ya ndege liliharibika na kuathiri uokoaji wa abiria na wahudumu wa ndege na kati ya watu 43 waliokuwemo katika ndege hiyo, abiria 17 walifariki dunia, rubani wawili wakifariki na majeruhi wakiwa 24.

Kawiche na Josephine walikuwa ni miongoni mwa abiria walionusurika kifo ambapo Kawishe alipata madhara ya moja kwa moja ya kiafya ikiwamo ‘disc’ za uti wa mgongo kupishana na madhara mengine ya kiakili na msongo wa mawazo.

Kwa upande wake, Josephine naye alisema ajali hiyo imemsababishia majeraha ya kichwa, kupata michubuko usoni na mwilini, majeraha katika goti la kushoto, maumivu ya tishu na kwenye miguu na maumivu ya msongo wa mawazo.


Pingamizi la awali lilivyokuwa

Upande wa wadaiwa katika majibu yao ya maandishi kuhusiana na madai hayo, waliyapinga na kuwasilisha pingamizi la awali wakieleza hati za madai zina dosari za kisheria ambazo haziwezi kutibika, chini ya sheria ya ukomo.

Kuhusiana na madai ya Kawiche, Wakili Nangi alieleza baada ya kupitia hati ya madai, madai hayo hayaangukii katika uzembe kwa kuwa taarifa kuhusiana na suala hilo inakosekana katika maelezo ya mdai.

Kulingana na wakili huyo, muda wa kisheria uliowekwa kufungua shauri la kudai fidia ni mwaka mmoja tangu suala lililoleta madhara litokee na kueleza ajali ilitokea Novemba 6,2022 hivyo kesi ilipaswa kufunguliwa  kabla ya Novemba 6, 2023.

Katika hoja yake ya pili, wakili huyo alisema hati ya madai ina dosari za kisheria ambazo hazitibiki, ambapo inataka mdai aeleze thamani ya shauri ili kuwezesha kupima mamlaka ya Mahakama na kiwango cha ada.

Wakili huyo alipinga vikali aya ya 17 ya hati ya madai akisema haionyeshi wazi wazi kama Mahakama hiyo ilikuwa na uwezo wa  kusikiliza shauri hilo, hivyo kwa sababu hiyo na ya kwanza aliomba shauri hilo litupwe.

Akijibu hoja hizo, wakili Patrick Malewo alisema pingamizi hilo limejielekeza vibaya akisema ajali ilitokea Novemba 6, 2022 na kwamba ukomo wa kufungua madai katika kesi ya aina hiyo ni miaka mitatu.

Kuhusu hoja ya pingamizi la mamlaka ya Mahakama, wakili Malewo alisema pingamizi hilo limeibuliwa isivyofaa, akisema katika aya ya 17 iliyorejewa, mdai ameonyesha wazi wazi ni kwa namna gani Mahakama hiyo ina mamlaka.

Wakili huyo alirejea kitabu cha mwandishi Mulla kiitwacho “The Code of Civil Procedure, 7th edition”, akisema mamlaka ya Mahakama itapimwa kwa kuegemea malalamiko yaliyoelezwa katika hati ya mdai aliyoiwasilisha mahakamani.


Ni kwa msingi huo, wakili huyo aliiomba Mahakama kulitupa pingamizi hilo.

Kwa upande wa pingamizi dhidi ya kesi iliyofunguliwa na Josephine, wakili Nangi alieleza hati ya madai ilikuwa na dosari za kisheria kuhusiana na muda wa ukomo wa kufungua shauri hivyo kueleza shauri hilo litupwe.

Hata hivyo, Februari 25, 2025 wakati kesi hiyo ilipoitwa ili kutolewa kwa amri mbalimbali, pande mbili zilikubaliana kuwasilisha hoja zao kwa maandishi, lakini upande wa wadaiwa haukutekeleza amri hiyo ya Mahakama.


Uamuzi wa Jaji

Katika uamuzi wake alioutoa Aprili 22, 2025 kuhusiana na pingamizi dhidi ya shauri la Kawishe, Jaji Mtembwa alisema hoja iliyopo mbele ya Mahakama inayohitaji kuamuliwa ni kama pingamizi hilo lina mashiko kisheria.

Akirejea mabishano ya kisheria, Jaji alisema wakili Nangi alijenga hoja kuwa kesi hiyo imefunguliwa nje ya muda na kueleza kuwa muda unaotolewa na sheria wa kufungua shauri la aina hiyo ni ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Hata hivyo, Jaji alisema katika majibu yake, wakili wa mdai, Malewo alisema shauri hilo la madai linaangukia katika sheria ya uzembe ambalo muda wa kisheria wa kulifungua ni miaka mitatu tangu ajali ilipotokea Novemba 6,2022.

“Kwa kuzingatia ukweli uliosisitizwa katika hati ya madai, ninalazimika kukubaliana na wakili Malewo kwamba mzizi wa lalamiko umejikita katika uzembe na wala si fidia kama wakili Nangi alivyotaka Mahakama hii iamini,” alisema Jaji.

“Kwa vile hakuna ubishi kuwa muda wa kuandaa na kuwasilisha kesi ya aina hii ni miaka mitatu, kwa kuhesabu kuanzia siku ya ajali naona pingamizi hilo linakosa mashiko. Kama lingefunguliwa Novemba 6, 2025 lingekuwa nje ya muda,” alisema.

Kuhusu dosari za hati ya madai ambazo wakili Nangi alisema hazitibiki mdai alipaswa kuonyesha mahakama ilikuwa na uwezo wa kusikiliza shauri hilo, Jaji hakukubaliana na hoja hiyo na kurejea maudhui yaliyomo katika hati ya madai.

Aya hiyo inasema ajali ilitokea katika Ziwa Victoria karibu na Bukoba, lakini makao makuu ya mdaiwa yapo Dar es Salaam na madai ya mdai ni fidia ya Dola 1,896,195 za Marekani, ambayo ipo ndani ya mamlaka ya mahakama hiyo.

“Kwa kutazama aya hiyo, ni wazi msingi wa sababu za kuchukua hatua ni ajali iliyotokea Ziwa Victoria karibu na Bukoba lakini ofisi za mdaiwa ziko Dar es Salaam. Kiwango cha fidia kimetajwa ni Dola 1,896,195 milioni,” alisema.

Jaji alisema kwa maoni yake, aya hiyo ina taarifa zinazojitosheleza kutimiza takwa la kisheria katika kupima uwezo wa Mahakama na kufanya hesabu ya ada ya kufungulia kesi na kiwango cha fidia imeachiwa mahakama iamue.

Kutokana na hayo, Jaji alisema kwa heshima anatofautiana na wakili Nangi kuwa hati ya madai ni lazima ionyeshe msingi wa sheria ambao madai yanaegemea.

Jaji Mtembwa alisema anaona hoja hiyo imepotea kwa sababu Mahakama inaweza kuendelea kuamua shauri hadi mwisho hata kama hakuna sheria ambayo madai yameegemea au kunukuliwa.

Kulingana na Jaji, alisema lililo muhimu zaidi katika lalamiko ni ukweli unaojumuisha sababu ya kuchukua hatua na mambo mengine yanayohusiana na kufuata sheria, hivyo aliona pingamizi hilo halina mashiko na linatupiliwa mbali.

Kuhusiana na pingamizi dhidi ya shauri lililofunguliwa na Josephine, aliyewakilishwa mahakamani na wakili Malewo, Jaji alisema pingamizi hilo linatupwa kwa kuwa wadaiwa hawakuwasilisha hoja zao za pingamizi kwa maandishi na Mahakama inahesabu kama hakukuwa na pingamizi.

Kutokana na msimamo huo, pingamizi lililokuwa limewekwa nalo limetupwa.