Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aina ya elimu waitakayo wadau nchini

Mkurugenzi wa TenMet, Ochola Wayoga (katikati) akiongoza wanajopo kujadili masuala ya elimu katika mkutano wa pili wa kimataifa wa ubora wa elimui. Picha ndogo sehemu ya washiriki wa mkutano huo uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Wakati Serikali ikieleza juhudi inazofanya ili kuboresha elimu nchini, wadau wamejadili mfumo wa elimu inayotolewa Afrika, hususan Tanzania na kupendekeza maboresho zaidi.

Wakati Serikali ikieleza juhudi inazofanya ili kuboresha elimu nchini, wadau wamejadili mfumo wa elimu inayotolewa Afrika, hususan Tanzania na kupendekeza maboresho zaidi.

Miongoni mwa juhudi zilizofanywa na Serikali ni pamoja kutoa elimu bila malipo kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi kidato cha sita, ujenzi wa madarasa, ambapo hivi karibuni Serikali ilikamilisha ujenzi wa madarasa 15,000 ili kukidhi idadi kubwa ya wanafunzi wanaoandikishwa.

Kama hiyo haitoshi, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imeanza kupitia upya Sera ya Elimu ya mwaka 2014, mitalaa na Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 ili kuboresha elimu inayotolewa.

Hata hivyo, wakijadili mfumo wa elimu katika mabadiliko ya ulimwengu katika mkutano wa pili wa kimataifa wa ubora wa elimu (IQEC) uliofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni, baadhi ya wadau wamehoji ubora wa elimu inayotolewa kama inaleta mabadiliko chanya kwa wanafunzi.

Akijadili suala hilo, mwanaharakati wa elimu nchini, Rakesh Rajan alimtaja Mwalimu Julius Nyerere kuwa kiongozi aliyekuwa akikosoa mfumo wa elimu hata katika utawala wake.

“Ukisikiliza hotuba za Mwalimu Julius Nyerere, hakujikita sana kwenye majengo na miundombinu, bali alijadili zaidi elimu hiyo ina manufaa gani kwa watu na kwa jamii?

“Alikuwa akikosoa na kuhoji kushindwa kwa elimu katika Serikali aliyoiongoza kwa kushindwa kufikia matarajio waliyojiwekea,” alisema Rajan.

Alisema kutokana na mtazamo huo, Mwalimu Nyerere, aliamini uongozi siyo kueleza mambo mengi uliyotekeleza bali pia kuonyesha upungufu na kukaribisha mijadala.

“Mwalimu alijua kwamba, shule katika nchi yetu na bara zima (la Afrika) ulikuwa mradi wa wakoloni, lengo lake lilikuwa ni kuzuia watu kufikiri, kuzuia watu kuhoji bali kutii watawala tu. Ndiyo maana alitaka kuondokana na mradi huo, kama Bob Marley alivyosema; ‘Jinasue katika fikra za kitumwa,” alisisitiza.

Rajan alinukuu kauli za Mwalimu Nyerere kuhusu elimu ikiwamo inayosema: “Elimu lazima iunge mkono maendeleo ya watu wake; fikra za kuhoji, uwezo wa kujifunza kwa wengine na kukataa au kukubali walichonacho na tatu ni hitaji la msingi la kuwa na jamii yenye usawa. Hiyo ni elimu kwa ajili ya kujitegemea.”

Kwa mujibu wa Rajan, msimamo wa Mwalimu Nyerere katika elimu ni kwamba inapaswa kumpa mtu hali ya kujiamini kama mtu huru na kuleta jamii yenye usawa.

“Uwe mvulana, msichana, mwanaume, mwanamke, mwanafunzi au mwalimu, mkulima au waziri katika Serikali, tunaaminiana wote. “Katika hayo yote, Mwalimu hakuzungumzia cheti, elimu siyo cheti. Kwake elimu ni pale mtu anapojiamini kujenga jamii huru yenye demokrasia,” alieleza.

Bajeti ya elimu

Uwekezaji katika sekta ya elimu ni suala lililojadiliwa kwa kina katika mkutano huo uliowashirikisha wadau kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Zambia, Lesotho, Sudani Kusini na wahisani wa Ulaya. Walisema uchangiaji unapaswa kuchukuliwa kama uwekezaji na siyo matumizi tu.

Mdau wa elimu nchini, Julie Juma anasema mara nyingi, Wizara zinazohusika na fedha barani Afrika, zinaona uchangiaji huo ni matumizi tu na siyo uwekezaji.

“Elimu ni uwekezaji mkubwa na matokeo yake huonekana baada ya muda mfupi na mrefu.

Akitoa mfano wa Tanzania, alisema kiwango cha kodi kwa pato la ndani (GDP) ni asilimia 11 ambacho kiko chini kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara cha asilimia 17.2 na pia chini ya kiwango chini kwa asilimia 15 ya matumizi ya kawaida ya Serikali

“Kuna kiwango kimewekwa kwa nchi za Afrika kuchangia katika bajeti za wizara ya elimu ambacho ni asilimia 15 hadi 20, lakini nchi za Afrika zinashindwa kufikia,” alisema.

Akishauri uwekezaji zaidi katika elimu, Julie anasema: “Kwanza wajizatiti katika kodi kwa uongeza kodi kwa uwiano wa GDP ili kuwekeza katika elimu.

Aliongeza: “Pia Serikali inatakiwa kudhibiti upotevu wa mapato unaofanyika kwa njia haramu, kudhibiti deni la Taifa na kuongeza walimu.’’

Naye Richard Olong ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kijamii kutoka shirika la Oxfam, akirejea utafiti walioufanya,anasema utafiti huo unaonyesha kwamba, kuwekeza maradufu kwenye elimu na sekta ya jamii, kuna uwezekano wa kuzalisha ajira 269 milioni kwa miaka saba ijayo barani Afrika.

“Pia utafiti umeonyesha kuwa ukiwekeza dola moja kwenye elimu, inaweza kukurejeshea faida ya dola nyingine 17,” alisema.

Akifafanua zaidi, Olong alisema elimu inasaidia kuleta amani na utulivu.

“Kwa watu walioelimika hawaoni sababu ya kuanzisha vita bila sababu ya msingi. Kinyume chake, watu walioelimika hawaendi vitani mstari wa mbele, bali hutumia wasio na elimu kwenda kupigana badala yao.”

Akijibu swali kwa nini viongozi hawatoi kipaumbele kuhusu elimu? Olong alisema kuna hali ya kukosekana kwa utashi wa kisiasa na kukosekana kwa rasilimali za kutosha.

“Ndiyo utaona kwamba, wakati nchi za Afrika zimekubaliana kutenga asilimia 20 ya bajeti zao kwa elimu, hazitekelezi,” anasema.

Lugha ya kufundishia

Katika kujadili lugha ya kufundishia, wadau walihoji kama lugha za Afrika zinafaa kufundishia.

Akiongoza mjadala huo, Dk Irene Otieno kutoka nchini Rwanda, alitaja baadhi ya nchi zinazotumia lugha za kigeni na lugha zao zikiwemo za Marekani, Ulaya na Asia, huku Bara za Afrika likitegemea zaidi lugha za kigeni katika elimu.

“Tanzania wao wanatumia Kiswahili, tunawapongeza kwa hilo. Bunge la Uganda limeamua kwamba Kiswahili litakuwa somo la lazima na kitakuwa moja ya lugha za Taifa,” alisema.

Akichangia mjadala huo, Meneja program wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet), Nicodemus Shauri, alisema tatizo la elimu siyo lugha, kwani nchi za Afrika zina lugha nyingi na hivyo kuleta mkanganyiko.

“Ukiangalia lugha zinazozungumzwa Afrika utaona watu milioni 237 wanaozungumza Kiingereza, wengine kwao hiyo ni lugha ya mama.

“Unakuja kwenye Kiarabu, ambacho kina wazungumzaji zaidi ya 140 na wengine kwao ni lugha ya mama, Kifaransa kinazungumzwa na zaidi ya watu milioni 145. Kiswahili kinazungumzwa na zaidi ya watu milioni 100,” anasema.

Alitoa mfano wa Nigeria, ambayo watu zaidi ya milioni 45 wanazungumza Yoruba, huku watu zaidi milioni 30 wakizungumza Igbo.

“Kwa hiyo kwa Afrika tatizo siyo lugha, tuna matatizo mengineyo yanayorudisha nyuma,” alieleza.

Akichangia zaidi mjadala huo, Profesa Aldin Mutembei kutoka Chuo Kikiuu cha Dar es Salaam, alisema inawezekana kutumia lugha za Kiafrika kufundishia.

“Wengine wanasema, huwezi kujifunza bila Kiingereza, Kwa hiyo Wajapan hawawezi kujifunza bila Kiingereza? Wajerumani wamejifunzaje sayansi? Sweden, Finland zimejifunzaje?

“Tuna mradi wa kufundisha Kiswahili kule Afrika Kusini katika Chuo Kikuu cha Kwazulu Natal kwa kutumia Isizulu, Zimbabwe tunatumia Kishona na Ndebele, Namibia tunajaribu kufundisha Kiswahili kwa kutumia Oshvambo.

‘’Wanasema uwekezaji utakuwa mkubwa sana kama tutaanza matumizi ya Kiswahili, basi kama haiwezekani, tuwekeze kwenye ujinga,’’ alisema.

Akieleza maazimio ya mkutano huo, Mkurugenzi wa TenMet, Ochola Wayoga amesema wamekubaliana kutafakari upya kuhusu mfumo wa elimu katika mabadiliko ya dunia, kwa kuweka mijadala endelevu kati ya asasi za kiraia, wataalamu wa elimu, wadau wa maendeleo na Serikali yenyewe.