Aina mpya ya migomba yagunduliwa

Muktasari:
Taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania (TARI) kwa kushirikiana na taasisi ya kimataifa ya kilimo katika ukanda wa kitropiko(IITA) wamegundua aina mpya ya mbegu za migomba.
Arusha. Taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania (TARI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo katika Ukanda wa Kitropiko (IITA) wamegundua aina mpya ya mbegu za migomba ya ndizi aina ya (Tariban) inayoleta tija ya uzalishaji kwa wakulima wa zao hilo.
Akizungumza katika uzinduzi wa aina mpya za migomba zinazozaa kwa wingi nchini Tanzania uliofanyikia katika Chuo kikuu cha Nelson Mandela(NM-AIST) Mkurugenzi wa TARI,Dkt.Godfrey Mkamilo amesema mbegu hizo zinaongeza uzalishaji kutoka tani 25 hadi 35 kwa hekta moja mwaka.
"Kazi hii ya ugunduzi wa mbegu ya Tariban imefanywa kwa ushirikiano kati ya wizara ya kilimo kupitia TARI,IITA pamoja na Taasisi ya utafiti wa kilimo nchini Uganda inayojulikana kwa jina la NARO lengo likiwa ni kuhakikisha wanapata mbegu za migomba ya ndizi inayoleta tija kwa wakulima wetu,"amesema.
Dkt.Mkamilo amesema mbegu hizo zimeshasambazwa kwa baadhi ya wakulima pamoja na mashamba 18 ya mfano katika Mkoa wa Arusha,Kilimanjaro,Morogoro pamoja na Kagera kwa lengo la kuzifikisha katika wahitaji na kuzitumia
Kwa upande wake mtafiti kutoka IITA ,Allan Brown amesema utafiti wa mbegu hiyo imechukua zaidi ya miaka 15 kutokana za zao hilo kuwa na changamoto ya upatikanaji wa mbegu halisia hali ambayo iliwabidi wafanye kazi hiyo pole pole ili waweze kupata kile walichokisudia.
Naye Mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Arusha,Hargney Chitukulo amesema mbegu hiyo aina ya Tariban itawasaidia wakulima kuinuka kiuchumi kutokana na uzalishaji wake kuongezeka.
"Uzuri wa aina hii ya mbegu inahimiri magonjwa ya minyoo ya ndizi kwa hiyo hii itaongeza pia usalama wa chakula,"amesema Chitukulo.
Mkurugenzi msaidizi wa uendelezaji wa mazao masuala ya pembejeo na ushirika wa kilimo,Beatus Malema amesema Tariban pia zipo aina nne za migomba ambapo tafiti yake imetoa matokeo chanya ambapo masoko ya zao hilo nje ya yapo hivyo wakulima watanufaika zaidi.
Mmoja wa wakulima kutoka Mkoa wa Kagera, Anacret Ishemoi amesema mbegu pamoja na kuongeza uzalishaji pia zinavumilia ukame hivyo wanaiomba serikali kuweka mazingira ya masoko ya pamoja ili wawe na maeneo maalumu ya kuuzia mazao hayo.
"Sasa hivi hatuna muundo mzuri wa masoko kila mtu anajiuzia anavyoona ikiwa wengine barabarani kutegea magari hali ambayo inahatarisha uhai wa mfanyabiashara wa ndizi,"amesema Ishemoi.