Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aga Khan yawanoa wauguzi, wakunga nchini

Baadhi ya wanufaika wa mpango wa mafunzo kwa wauguzi unaotekelezwa na Shule ya Uuguzi na Ukunga ya Chuo Kikuu cha Aga Khan Afrika Mashariki, wakifurahia wakati wa mkutano wa tathmini wa chuo hicho Julai 27, 2024 Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Kwa zaidi ya miaka mitano, Shule ya Uuguzi na Ukunga ya Chuo Kikuu cha Aga Khan Afrika Mashariki, imekuwa ikitoa mafunzo kwa wauguzi na wakunga nchini ili kuwawezesha kushughulikia kesi mbalimbali

Dar es Salaam. Katika kukabiliana na upungufu wa wahudumu wa afya, Shule ya Uuguzi na Ukunga ya Chuo Kikuu cha Aga Khan Afrika Mashariki, imekuja na mpango wa kuzalisha wauguzi wenye ubora.

Mpango huo umekuja wakati Serikali inajikita kutekeleza mkakati wa kutoa huduma bora za afya kwa wote ifikapo mwaka 2030.

Kwa zaidi ya miaka mitano, chuo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo kwa wauguzi na wakunga nchini ili kuwawezesha kushughulikia kesi mbalimbali.

"Tumekuwa tukiwafundisha wauguzi na wakunga kuwa na uwezo wa kuwahudumia wagonjwa wanaofika hospitalini wakiwa na mahitaji," amesema Mratibu wa Maendeleo ya Utaalamu Endelevu chuoni hapo, Aminieli Usiri.

Ametoa maelezo hayo Julai 27, 2024 wakati wa mkutano wa tathmini kati ya chuo hicho na wanufaika wa mpango huu wa mafunzo, uliowaleta pamoja wawakilishi wa wauguzi na wakunga kutoka mikoa minane inayofaidika.

"Mengi ya mafunzo haya yalilenga kuwasaidia wauguzi na wakunga kutumia vifaa vya kisasa, ikiwemo mashine za kusaidia wagonjwa walioko katika hali mbaya," amesema Usiri.

Amesema katika miaka miwili iliyopita, programu hiyo imewafikia wauguzi 332 katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Mwanza, Shinyanga, Arusha, Morogoro, na Mtwara.

"Mbali na mafunzo ya ana kwa ana tunayotolea, pia tunatoa mafunzo mengine kupitia mfumo wa mtandaoni wenye kozi 14, kuhakikisha kwamba wauguzi wanaweza kufikia na kujifunza. Katika miaka miwili iliyopita, kupitia mfumo huu, tumekuwa na wauguzi 982 waliofanikiwa kumaliza na kupata vyeti," amesema.

Mratibu wa Huduma za Kliniki na Maendeleo ya Utaalamu Endelevu katika Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Pius Kamana amesisitiza umuhimu wa wauguzi katika huduma za afya.

"Asilimia 80 ya kazi zote zinazofanywa katika vituo vya afya, zahanati na hospitali zinafanywa na wauguzi. Kwa hiyo, kwa kujenga uwezo wa wauguzi, tunaunda nguvu kubwa inayoweza kusaidia kuboresha utoaji wa huduma za afya katika hospitali zetu."

Ameongeza kuwa asilimia 60 ya wafanyakazi wote wa sekta ya afya, katika sekta za umma na binafsi, ni wauguzi.

"Hivyo, Aga Khan walifanya chaguo zuri kwa kuongeza uwezo wa kundi kubwa katika sekta ya afya ili kuwezesha safari ya kuwafikia wengi kwa huduma bora,"

Amesema upanuzi wa vituo vya huduma za afya nchini Tanzania unaonyesha haja ya kuwa na wauguzi waliopata mafunzo mazuri.

Mwaka 2015, Tanzania ilikuwa na hospitali za manispaa 77 pekee, lakini sasa zipo 182. Vituo vya afya vimeongezeka kutoka 488 hadi zaidi ya 900 na zahanati zimeongezeka kutoka chini ya 4,800 hadi zaidi ya 6,000.

"Hivyo, Tanzania bado inahitaji watoa huduma wenye uwezo ambao wamepata mafunzo mazuri na wana maarifa na ujuzi wa kutosha kuwahudumia wale wanaohitaji," amesema Dk Kamana.

Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Redemta Matindi, amesema Aga Khan ni moja ya sekta binafsi zinazounga mkono Serikali katika kuhakikisha huduma za afya zinafikia viwango vya juu.

Amebainisha jitihada za chuo hicho kupunguza pengo la ujuzi na uhaba wa maarifa katika sekta ya afya, hasa miongoni mwa wauguzi na wakunga. "Hii imeendelea kuchangia kuboresha huduma za afya nchini."

Mkuu wa Wauguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Elias Haali, amebainisha manufaa ya wazi ya mafunzo hayo.

"Mafunzo haya yamewawezesha wanufaika kutumia vifaa vya kisasa vilivyopo katika vituo vya afya ambavyo wauguzi na wakunga wasingekuwa na uwezo wa kuvifanya kabla."