Aga Khan kusaidia kupoza gharama matibabu kwa wajasiriamali wanawake

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Women Tapo, Lulu Yassin (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa hospitali ya Aga Khan Tanzania,Karim Dharani wakisaini mkataba wa kuwasaidia wajasiliamali wanawake wanaofanya shughuli mbalimbali masokoni katika kupata huduma za afya,jijini Dar es Salaam,kulia ni Mkurugenzi wa vituo vya Afya Aga Khan Tanzania, Hassan Ali. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Aga Khan kwa kushirikiana na Taasisi ya Women Tapo, zasaini makubaliano kusaidia wajasiriamali wanawake.
Dar es Salaam. Taasisi ya Huduma za Afya Aga Khan (AKHS) na ya Women Tapo zimesaini makubaliano yanayolenga kutoa unafuu wa gharama za matibabu kwa wanawake wajasiriamali wanaofanya shughuli zao katika masoko jijini Dar es Salaam.
Kupitia makubaliano hao, wanawake hao watawezeshwa kupata bima za matibabu kwa gharama ya Sh40,000 kwa mwaka.
Hayo yamebainishwa na Lulu Yassin, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Women Tapo inayojishughulisha na masuala ya wanawake wajasiriamali, alipozungumza na waandishi wa habari leo Septemba 13, 2024 baada ya kusainiwa makubaliano kati ya AKHS na taasisi hiyo yanayolenga kuwapa unafuu wa matibabu wanawake hao, hasa wajasiriamali wadogo katika masoko yaliyopo Dar es Salaam.
Lulu amesema katika gharama hizo wajasiriamali watachangia Sh20,000 na kiasi kilichobaki kitalipwa na wafadhili.
"Lengo ni kila mwanamke mjasiriamali wa masokoni aweze kulipa Sh10,000; ili hilo liweze kufanyika tunahitaji wadau wengine kuunga mkono jambo hili," amesema.
"Aga Khan itawezesha kina mama waliopo masokoni kufahamu hali za afya zao na watakapobainika na changamoto waweze kupatiwa matibabu mapema," amesema.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa vituo vya Aga Khan Tanzania, Hassan Ali amesema kutokana na changamoto zilizobainishwa na baadhi ya wanawake wenye kipato cha chini kushindwa kumudu gharama za matibabu, kwa kushirikiana na taasisi hiyo, wameingia makubaliano ili kuwasaidia kupata unafuu wa matibabu katika vituo vya afya vya Aga Khan kwa kuanzia katika Jiji la Dar es Salaam.
Baadhi ya vituo ambavyo watakuwa wakipatiwa huduma amesema ni vilivyopo Sinza, Kimara, Tabata, Ukonga na Hospitali ya Aga Khan.
"Ushirikiano huu unalenga kuboresha ustawi wa kiuchumi na kijamii wa wanawake wajasiriamali wanaofanya shughuli zao masokoni kwa kuwapa unafuu wa matibabu," amesema.
Akifafanua namna wajasiriamali hao watakavyonufaika, Kaimu Mkuu wa Idara ya Biashara, Masoko na Mawasiliano wa AKHS, Olayce Steven amesema watapatiwa huduma kupitia vifurushi maalumu vilivyowekwa ambavyo vitawasaidia kumuona daktari, kufanyiwa uchunguzi wa awali na kupatiwa dawa.
"Ili kunufaika na mpango huu hatua ya awali ilikuwa ni kwa wajasiriamali hao kujisajili katika Taasisi ya Women Tapo ambayo tayari imekamilika, sasa tupo katika hatua ya utekelezaji," amesema.
Amesema katika vituo hivyo pia watawafikia wanawake hao na kuwafanyia uchunguzi wa awali wa magonjwa mbalimbali na kuwapatia elimu ya afya na msaada wa kisaikolojia.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Mohammed Mang'una amesema kinachofanywa na taasisi hizo kinalenga kuboresha ustawi wa mwanamke.
Amesema wanawake ndio tegemeo katika upande wa familia na jamii kwa ujumla, kwani wanabeba majukumu ya malezi hata utafutaji wa kiuchumi.
Amesema ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu wanahitajika kuwa na afya njema.
Aminata Rashid, mfanyabiashara wa matunda katika Soko la Tabata amesema kutokana na kipato duni, baadhi ya wanawake hushindwa kuwa na utaratibu wa kwenda hospitali kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa afya zao, hivyo wakati mwingine hufika hospitali wakati tayari ugonjwa umeshakua mkubwa.
Ametoa mfano wake akisema alipopata changamoto ya maumivu ya miguu kutokana na kushindwa kufika mapema kituo cha afya, sasa hawezi kutembea vizuri.
"Nilikuwa sina namna ya kufanya, kipato changu kwa siku hakizidi Sh11,000 ambayo inanisaidia kwa chakula na kusomesha watoto wangu na wajukuu," amesema.