Afrika Mashariki kushirikiana usimamizi miradi ya umeme

Muktasari:
- Hatua hiyo inalenga kuhakikisha ushirikiano wa kutosha na uwezo wa kusaidiana kati ya nchi za eneo hilo kwenye uzalishaji na usambazaji wa nishati.
Dar es Salaam. Mawaziri wa Nishati wa Nchi za Afrika Mashariki, wamekubaliana kuwa na usimamizi madhubuti wa miradi ya umeme katika nchi hizo, ili ikamilike kwa wakati na kuwahudumia wananchi.
Makubaliano hayo yamefanyika katika mkutano wa 18 wa Baraza la Mawaziri wanaohusika na mfumo wa pamoja wa umeme kwa nchi za Mashariki mwa Afrika.
Akizungumza katika kikao hicho jijini Nairobi nchini Kenya jana Jumanne, Februari 27, 2024, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dk Doto Biteko amesema hatua hiyo itawezesha mataifa hayo kusaidiana pale inapotokea nchi moja ina upungufu wa nishati hiyo.
"Kukamilika kwa miradi kutoka vyanzo mbalimbali vya umeme, kutawezesha nchi hizo kusaidiana pale nchi mojawapo inapokuwa na upungufu wa umeme," amesema.
Katika hotuba yake hiyo, Dk Biteko ameweka msisitizo katika miradi ya usafirishaji wa umeme.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dk Doto Biteko
“Baraza hili ni muhimu katika kuhakikisha nchi za Afrika zinaungana kwa ajili ya kuendeleza rasilimali za umeme zilizopo pamoja na kupata umeme wa uhakika kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii," amesema.
Ameeleza kila nchi imeonyesha utayari wa kufanya biashara ya umeme pale inapokuwa na ziada.
Amesema, Tanzania itakuwa sehemu ya soko la umeme pale nchi jirani zitakapohitaji nishati hiyo.
Hatua hiyo, amesema itafikiwa baada ya kuwashwa kwa mashine zote tisa katika Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere linalotarajiwa kuzalisha megawati 2,115.
“Tanzania kuna njia mbalimbali za usafirishaji umeme, mfano Tanzania na Uganda, Tanzania na Burundi pamoja na Tanzania na Rwanda na sasa kuna laini ya umeme kutoka Tanzania hadi Kenya iliyokamilika na ipo kwenye majaribio," amesema.
Amesema laini hiyo itawezesha kufanyika kwa biashara kati ya nchi hizo pale kila nchi ikiwa na umeme wa kutosha.
Ameeleza kwa sasa kuna upembuzi yakinifu unafanyika chini ya Benki ya Dunia (WB) kwa ajili ya kujenga mradi mkubwa wa usafirishaji umeme wa msongo wa Kilovoti 400 kutoka Tanzania hadi Uganda.
Mradi huo, amesema utatokea Shinyanga na utasafirisha umeme mwingi zaidi kwa baadhi ya mikoa kama Kagera hivyo kuiwezesha nchi kufanya biashara ya nishati hiyo.
Katika hatua nyingine, Dk Biteko amesema sekta ya nishati ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hivyo suala la kupeleka nishati ya kutosha, salama na ya gharama nafuu kwa wananchi si hiari, ni wajibu kwa ajili ya shughuli za uzalishaji.
Kwa mujibu wa Dk Biteko, ukuaji wa nishati kwa nchi za Afrika Mashariki ni asilimia sita kwa mwaka na kwamba kuna kazi kubwa inatakiwa kufanywa, ili kuhakikisha wananchi wanapata nishati ya uhakika.
Kupitia mfumo wa pamoja, Dk Biteko amesema miradi mbalimbali inatekelezwa ukiwemo wa ujenzi wa miundombinu ya umeme wa Kenya-Uganda, Kenya-Ethiopia, Kenya-Tanzania,Tanzania-Rwanda, Tanzania-Uganda, Tanzania-Burundi na DRC-Burundi.
"Nchi Wanachama zinapaswa kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili kupunguza changamoto za umeme," amesema.
Awali, Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Waziri wa Nishati na Petroli wa Kenya, Davis Chirchir amesema kufanya biashara ya mauziano ya umeme pale kunapokuwa na ziada.
Majadiliano ya viongozi hao, amesema yamelenga katika kuimarisha muundo wa umoja huo na ushirikiano, kadhalika kuonyesha njia za kukabiliana na changamoto mbalimbali za umeme pale zinapojitokeza.
Ameeleza tayari Kenya inafaidika na mfumo huo baada ya kupokea magawati 200 kutoka nchini Ethiopia, hivyo kuongeza kiasi cha umeme katika nchi hiyo.
Ameongeza kati ya watu bilioni 1.5 Afrika, milioni 600 bado hawajapata nishati ya umeme katika bara hilo.