Kisa uhaba wa umeme Serikali yawaita wawekezaji

Muktasari:
- Lengo ni kupata taarifa kuhusu sekta ya nishati nchini, kuangalia uwezekano wa namna ya kutumia wawekezaji na kuiendeleza kwa kushirikiana na nchi nyingine za Afrika.
Arusha. Serikali imewaalika wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza katika miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mbadala ikiwamo gesi, upepo, jua na joto ardhi ili kuongeza vyanzo vya kuzalisha nishati hiyo.
Hayo yamebainishwa leo Januari 31, 2024, jijini Arusha na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga wakati akizungumza kwenye mkutano wa tano wa ushirikiano wa nishati Tanzania ambao umewakutanisha wadau wakuu wa sekta ya nishati kutoka nchi za Afrika Mashariki.
Amesema mkutano huo unalenga kupata taarifa kuhusu sekta ya nishati hapa nchini, kuangalia uwezekano wa namna ya kutumia wawekezaji na kuiendeleza kwa kushirikiana na nchi nyingine za Afrika.
“Hapa tumewaambia wawekezaji kuna fursa katika miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia jua, upepo na maeneo yapo tayari na maandiko yameshaandaliwa, hivyo tumetoa fursa kwa wawekezaji ili waje tufanye nao mazungumzo kwa ajili ya kuwekeza miradi hiyo ili tuwe na vyanzo vingi vya kuzalisha umeme siyo kutumia gesi na maji tu,” amesema Luoga.
Amesema kupitia mradi wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) unaokaribia kukamilika, utazalisha megawati 2,115 za umeme.
Mkutano huo uliohusisha wadau mbalimbali, ulitokana na azimio la kutumia vyanzo mbadala vya umeme badala ya kutumia vya kuzalisha umeme kama maji na gesi ambavyo wakati mwingine kunakuwa na ukame, hivyo kusababisha upungufu wa nishati hiyo.
“Mkutano huu moja ya azimio ni nchi za Afrika kutumia vyanzo mbadala kuzalisha umeme na katika kuongeza upatikanaji wa umeme, tutazungumza kuhusu kuunganisha nchi zote katika mtandao mmoja wa umeme ili kukiwa na shida katika nchi moja, nchi nyingine itapata umeme kutoka kwao,” amesema Luoga.
Akizungumzia hali ya umeme nchini, amesema inaendelea kuimarika, bado kuna upungufu wa umeme katika baadhi ya maeneo lakini Serikali inaendelea kutekeleza mikakati ya kuhakikisha upatikanaji wa umeme nchini unaimarika.
“Ukiangalia hali ya umeme mwaka uliopita kuanzia Agosti hadi Desemba na sasa hivi ni tofauti, hali ya umeme imeanza kuimarika, hadi Machi hali itakuwa nzuri, tunashughulikia matatizo ya umeme huku tukiendelea kuboresha miundombinu na kusimamia miradi,” amesema Luoga.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi Gisima Nyamuhanga amesema Watanzania wamepitia katika kipindi kigumu cha hali ya umeme na kwa sasa wanaendelea kuhakikisha hali hiyo inaisha.
“Tanzania tuna upungufu mkubwa wa umeme, vilio ni kila mahali na lawama kila mahali, Watanzania tumepitia kipindi kigumu cha hali ya umeme hapa katikati na tunashukuru wananchi wametuelewa na wamekuwa wavumilivu lakini sasa jibu la matatizo liko mlangoni, adha hii tutaisahau,” amesema Nyamuhanga.
“Kupitia mkutano huu, tutaboresha ushirikiano na nchi hizo katika sekta ya umeme kwa kufungua mipaka, tuna mipango ya kutumia vyanzo vingine vya nishati kama mtaona tumeanzisha kampuni ya jotoardhi itakayozalisha umeme ni jambo ambalo halijawahi kusikikika, kampuni ipo na tafiti zimeshafanyika, tunaangalia taratibu za kuwekeza ili tuzalishe umeme,” amesema.
Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela amesema ni muhimu sekta binafsi kujitokeza kukabiliana na changamoto ya maendeleo ya soko hasa katika miundombinu ya umeme na gesi asilia.