Aenda jela miaka 20 kutokana na nyama ya kiboko

Muktasari:
Hukumu hiyo metolewa leo Ijumaa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda, Chiganga Ntengwa baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka uliokuwa ukiongozwa na mwanasheria wa Serikali, Flaviani Shio.
Sumbawanga. Mahakama ya Wilaya ya Mpanda imemuhukumu Omary Maganga (45) kutumikia jela kifungo cha miaka 20 baada ya kupatikana na hatia ya kukamatwa na nyama ya kiboko zaidi ya kilo 110.
Hukumu hiyo metolewa leo Ijumaa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda, Chiganga Ntengwa baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka uliokuwa ukiongozwa na mwanasheria wa Serikali, Flaviani Shio.
Awali, katika kesi hiyo mwendesha mashitaka huyo alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa Maganga alitenda kosa hilo Oktoba 10 mwaka 2016 nyakati za saa 10 jioni.
Alidai kuwa siku ya tukio mshitakiwa alikamatwa akiwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi huku akiwa na nyama ya kiboko yenye uzito wa kilo 118 ambayo thamani yake Sh 3.2 milioni.
Mwanasheria huyo wa Serikali aliiambia mahakama kuwa mshitakiwa huyo alikamatwa na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi baada ya kuwa wamepata taarifa kutoka kwa raia wema za kuwa mshitakiwa amekuwa akifanya ujangili kwenye hifadhi hiyo.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Chiganga amesema kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo Mahakama pasipo shaka yoyote inamtia hatiani mshitakiwa.