Dk Mpango ataja hatua sita kuongeza ukusanyaji mapato ya ndani

Muktasari:
- Dk Mpango amesema ni muhimu kongamano la kodi na uwekezaji linalofanyika nchini kuibua mipango na mikakati mipya itakayosaidia kuongezeka kwa mapato ya ndani na Serikali kupata fedha kuboresha huduma
Dar es Salaam. Makamu wa Rais Dk Philip Mpango ameelekeza hatua sita zinazopaswa kuchukuliwa na Wizara ya Fedha kuongeza mapato nchini, ikiwemo kuboresha mfumo wa kodi wenye usawa na kuondokana na msamaha wa kodi usio na tija.
Pia, Dk Mpango ambaye aliwahi kuwa waziri wa fedha amesisitiza kupunguzwa kwa gharama za kurasimisha biashara isiyo rasmi kuwa rasmi, mlolongo wa kodi ambao wajasiriamali wanalalamikia unawakwaza kurasimisha biashara zao.

Dk Mpango ametoa maelekezo hayo leo Aprili 15, 2025 ikiwa ni sehemu ya kutafuta majawabu ya kero zinazowakumba wawekezaji nchini, ambao wamelalamikia mfumo wa kodi kutokuwa rafiki na unarudisha nyuma jitihada za wajasiriamali kurasimisha biashara zao.
Akizungumza wakati akizindua kongamano la kodi na uwekezaji lililoandaliwa na Wizara ya Fedha, Dk Mpango amesema hatua hizo alizozieleza zikichukuliwa zitaongeza mapato ya ndani.
“Kwanza tuweke mkazo wa kuimarisha uwezo wa ukusanyaji wa kodi na matumizi ya mapato ya ndani, jambo la tatu mtoe vivutio kwa mawakala na taasisi za kukusanya kodi ili kukabiliana na vitendo vya rushwa, hatua nyingine tunatakiwa tukuze matumizi ya Tehama katika ukusanyaji wa kodi na uwekaji wa akiba, tuongeze matumizi ya mashine za kielektroniki EFD,” amesema.
Hatua ya mwisho aliyoieleza Dk Mpango ifanyiwe kazi ni kuboreshwa kwa mazingira ya biashara na kujengwa kwa kanzidata ya taarifa ya walipakodi pamoja na kuongeza wigo wao ili kupunguza mzigo kwa kundi dogo linalolipa kodi.
“Hapa nakubaliana na maoni ya sekta binafsi kwamba Wizara ya Fedha, Wizara ya Mipango na Uwekezaji zitoe elimu ya kikodi kwa wajasiriamali wetu wadogo na kupunguza gharama za kurasimisha biashara ili zitoke sekta isiyo rasmi kwenda sekta rasmi.”
Dk Mpango amesema upo uhitaji mkubwa wa kufanyika maboresho ya kisera, kanuni na taratibu za uwekezaji na biashara, lengo likiwa ni kufikia malengo stahiki ya ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Dk Mpango ametoa maelekezo hayo baada ya kuibuliwa kero na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Angelina Ngalula, ambaye amesema wajasiriamali hawarasimishi biashara zao kutokana na kutofahamu faida za kufanya hivyo.
“Mama ntilie leo anayeuza chai chini ya mti, mfanyabiashara huyu anajitafuta. Akifungua eneo lake auze chakula kwa usafi, anaanza kufuatwa na taasisi nyingi za Serikali ili alipe kodi. Tungeondoa hii kero ya taasisi kudai kodi kabla ya biashara kukua,” amesema.
Angelina ambaye amependekeza Wizara ya Fedha iwe na kitengo maalumu cha utoaji wa elimu ya kodi kwa wananchi ili kupata kundi kubwa la wajasiriamali wanaorasimisha biashara zao.
Amedokeza kikwazo cha watu kutokwenda kusajili biashara zao ni tozo nyingi wanazokumbana nazo, huku akibainisha kuwa wafanyabiashara wengi wakubwa wapo sekta isiyo rasmi.
Njia wanazotumia wafanyabiashara hao kubaki sekta isiyo rasmi, Angelina amesema ni kununua mizigo na kugawa kwa machinga jambo linalowawezesha kutolipa kodi.
Mbali na hayo Angelina ameishauri Serikali kuweka mipango mipya itakayoiwezesha kukuza uchumi wake yenyewe bila kutegemea sana wahisani, ambao wanakuja na masharti yanayobana.
Akiitolea mfano Marekani amesema mabadiliko ya kisheria nchini humo yameathiri biashara na baadhi ya shughuli za kijamii Tanzania na hivyo kuathiri uchumi.
"Ukiangalia athari za moja kwa moja za kibiashara kati ya Marekani na Tanzania huzioni, lakini tumekuwa tukifanya biashara na nchi nyingi ambazo zinashirikiana na Marekani hivyo kuathiri uchumi wetu, Serikali iangalie njia ya kuepuka kuwa wategemezi ili kutoathiri uchumi wetu wahisani wanapojiondoa," amesema Angelina.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Augustine Holle, ameibua kero inayowaandama wafanyabiashara kuhusu mashine za kielektroniki.
Hoja yake katika hilo, wafanyabiashara wanapokwenda kudai malipo ya huduma walizotoa serikalini hupaswa kutoa risiti za EFD, na wakati akisubiri malipo kwa zaidi ya wiki, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) humfuata mfanyabiashara huyo alipe kodi ya ongezeko la thamani (VAT) wakati hajapokea fedha.
Akieleza maboresho yaliyofanyika sekta ya uwekezaji, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo amesema kupitia mapitio ya sheria 66 za kisekta, tozo na kodi 383 zimeondolewa na Serikali ili kuvutia uwekezaji nchini.
Kutokana na maboresho mbalimbali sekta ya uwekezaji, Nyongo amesema mwaka 2024 ulikuwa wa uwekezaji kwani Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kilisajili miradi 901, kati ya hiyo 321 ya Watanzania, 176 ubia baina ya Watanzania na wageni, 404 ni miradi ya wawekezaji kutoka nje ya nchi.
Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi, Balozi Ombeni Sefue amesema katika kutatua kero za kikodi nchini tayari wamepokea maoni ya wananchi wa kada mbalimbali kupitia mikutano 160 iliyowakutanisha wadau na maoni 2,300 yamepokelewa kupitia barua pepe.