ACT-Wazalendo yapigania viwanda vya kahawa Kigoma

Waziri Kivuli wa Uchukuzi wa ACT-Wazalendo, Kiza Mayeye akihutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Kalinzi Wilaya ya Kigoma.

Muktasari:

Chama cha ACT-Wazalendo kimeitaka Serikali kujenga viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo ikiwemo kahawa kuwahakikishia wakulima soko la uhakika la mazao yao.

Kigoma. Chama cha ACT-Wazalendo kimeitaka Serikali kujenga viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo ikiwemo kahawa kuwahakikishia wakulima soko la uhakika la mazao yao.

Wito huo umetolewa na Waziri kivuli wa Uchukuzi wa ACT-Wazalendo, Kiza Mayeye wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Kalinzi Wilaya ya Kigoma.

“Wakazi wa maeneo ya nyanda za juu mkoani Kigoma ni wakulima wa mazao mbalimba ya chakula na biashara ikiwemo kahawa na tatizo kubwa linalowakabili ni ukosefu wa soko na bei ya uhakika. Tatizo hili linaweza kumalizika kwa  Serikali kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda au kuweka mazingira bora kwa sekta binafsi kuwekeza ili kuongeza tija kwa wakulima," amesema Kiza

Miongoni mwa maeneo ya ukanda wa juu katika Wilaya za Kigoma na Buhigwe ambako zao la kahawa linalimwa ni pamoja na Kalinzi, Mkingo, Matiazo, Mnanila na Nyarubanda.

Mwanasiasa huyo aliyegombea ubunge jimbo la Kigoma Kaskazini mwaka 2020 amesema ujenzi wa viwanda siyo tu utawanufaisha wakulima, bali pia Taifa kupitia kodi na ushuri mbalimbali.

Ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuwadhibiti wanunuzi wa kahawa wasiozingatia kanuni maarufu kama kangomba wanaolangua mazao ya wakulima kwa bei ya chini na wao kwenda kuiuza kwa bei ya juu.

Akizungumzia kilimo cha kahawa na mazao mengine ya biashara na chakula ikiwemo mananasi na ndizi, Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amewataka viongozi na wawakilishi wa wananchi mkoani Kigoma kutumia nafasi zao kutafutia ufumbuzi kero zinazowakabili wananchi ikiwemo ukosefu wa masoko na bei nzuri ya mazao ya wakulima.

"Kazi ya kiongozi ni kutafutia ufumbuzi matatizo ya wananchi; kwetu Kigoma changamoto zetu ni masoko ya mazao yetu na miundombinu ya barabara. Haya ndiyo matatizo ambayo viongozi wetu wanatakiwa kuyashughulikia," amesema Zitto

Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Kigoma, Sendwe Ibrahim ameunga mkono hoja ya viongozi kutafutia ufumbuzi kero za wananchi akitaja usumbufu unaotokana na masuala ya uraia kuwa miongoni mwa mambo yanayowakera wakazi wa mkoa huo.