ACT Wazalendo wataka uungwaji mkono Zanzibar mpya

Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud
Pemba. Chama cha ACT Wazalendo kimesema ndicho chama pekee chenye maono ya kujenga Zanzibar mpya hivyo kuwataka Wananchi kukiunga mkono ili maono hayo yafikie ifikapo mwaka 2025.
Kauli hiyo imetolewa leo Juni 12, 2023 na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho ambaye pia ni Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud katika muendelezo wa ziara za chama hicho Mtambile Kusini Pemba
"Naomba tuamke tusimame imara kwa waliokuwa wamelala, tushikamane tuwe na nguvu ya pamoja kwa waliokuwa wameshakata tamaa maana wakati ni sasa," amesema
Othman amesema Zanzibar ni tajiri lakini wananchi wake ni masikini katikati ya utajiri huo kutokana na kukosa mikakati imara na kutumia rasilimali zake kwa ubunifu.
Amesema iwapo chama hicho kitapata ridhaa kipaumbele chao cha kwanza ni wananchi na kila mmoja atanufaika kutokana na utaratibu watakaokuwa wameweka.
Amesema licha ya madai kwamba Zanzibar ardhi yake ni ndogo, Othman alisema madai hayo si ya kweli ila kinachokosekana ni utaratibu maalumu na maeneo mengine ya wanachi yakichukuliwa bila kuzingatia misingi
"Uwekezaji unatakiwa lakini uzingatie matakwa ya wananchi, kwahiyo haya ndio tunasema tukikabidhiwa dola tutayabadilisha," amesema.
Kuhusu muungano amesema wananchi wanatakiwa waamue na kila upande upate haki zake zinazostahili tofauti na kuonekana kama upande mmoja unaulalia upande mwingine wa muungano.
Naye Mjumbe wa kamati kuu ya Chama hicho, Ismail Jussa amesema wamekuwa wakisema madudu yanayofanywa na kuonekana waongo lakini ripoti ya CAG imefichua ukweli huo.
Amesema kwa mujibu wa ripoti ya CAG, fedha zilizotolewa kwa ajili ya kupunguza ahueni ya Uviko-19 imeonyesha jinsi zilivyotumika bila utaratibu.
Amesema wataendelea kuyasema hayo na kazi ya chama hicho ni kuleta uwajibikaji na kusimamia mali za umma.
"Haya yote yanaonyesha kwamba hawa watu hawawezi na dawa yao tuwaondoe madarakani mwaka 2025," amesema.
Mkutano huu ni sehemu ya mikutano 12 iliyopangwa kufanywa na chama hicho katika visiwa vya Unguja na Pemba kueleza dhamira ya chama hicho na kufafanua masuala mbalimbali wanayodai yanakiukwa hivyo kuifanya Zanzibar kuwa masikini.