ACT-Wazalendo, ADC kuzindua kampeni Amani, NCCR yajitenga

Muktasari:

Kampeni za uchaguzi mdogo ubunge wa Aman, Zanzibar zimeanza kwa vyama kuwania jimbo hilo katika uchaguzi utakaofanyika Desemba 17, 2022 kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wake kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Hassan Mussa kufariki dunia.

Dar es Salaam. Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikitangulia kuzindua kampeni za uchaguzi Jimbo la Amani visiwani Zanzibar, vyama vya ADC na ACT Wazalendo vinatarajia kufanya hivyo huku NCCR-Mageuzi kikiweka wazi sababu za kutoweka mgombea.

 Uchaguzi katika jimbo hilo unafanyika kuziba nafasi ya Mussa Hassan Mussa, aliyefariki dunia Oktoba 13, 2022.

Pazia la uzinduzi wa kampeni katika jimbo hilo, lilifunguliwa na CCM Desemba mosi, 2022 ambapo mgeni rasmi alikuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka.

Chama cha ACT-Wazalendo kinatarajia kufuatia katika uzinduzi huo, Desemba 8, 2022, kwa mujibu wa Katibu wa Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa chama hicho, Salim Bimani.

Leo Jumapili, Desemba 4, 2022 akizungumza na Mwananchi Digital, Mwenyekiti wa chama cha ADC Taifa, Hamad Rashid amesema Desemba 11, 2022 ndiyo siku wanayotarajia kuzindua kampeni.

Naye Katibu Mkuu wa ADC, Doyo Hassan Doyo ndiye anayetarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, huku Hamd Rashid akiwa mgeni maalum siku ya kufunga Desemba 13, 2022.

“Tutafungua kampeni Desemba 11 na kuzifunga Desemba 13 mwaka huu,” amesema Hamad.

Kwingineko katika chama cha NCCR Mageuzi, kimesema hakitashiriki uchaguzi huo kwa kuwa hakikuweka mgombea.


Alipotafutwa kulifafanua hilo, Kaimu Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Joseph Selasini amesema uamuzi huo umetokana na ukweli kwamba nguvu ya NCCR-Mageuzi katika jimbo hilo ni ndogo ukilinganisha na washindani wake.

“Tumefanya tathmini ya kuangalia nguvu ya chama chetu katika jimbo hilo na kuangalia nguvu ya mgombea, baada ya tathmini tumebaini hatuna nguvu kuzidi washindani wetu, hakuna haja ya kuweka mgombea kwenye mazingira hayo,” amesema

Hata hivyo, amesema watashiriki uchaguzi mdogo katika maeneo mengine ikiwemo katika kata moja iliyopo Tanga Mjini na ule wa Kata ya Majohe Dar es Salaam.

“Kuhusu utaratibu wa kampeni katika chaguzi hizo nitakuwa na nafasi nzuri ya kueleza baada ya kuwasiliana na viongozi wa chama wa maeneo husika,” amesema Selasini.


NCCR-Mageuzi inaungana na Chama Cha Wananchi (CUF) ambacho kimekwisha kuweka wazi kutoshiriki uchaguzi huo.