Abiria wa KQ waliokuwa wasafiri kuja Dar kutoka Kenya wakwama JKIA

Abiria kutoka nchi mbalimbali waliokuwa wakielekea Dar es Salaam-Tanzania kwa ndege Kenya Airways (KQ), wamekwama katika uwanja Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta(JKIA), baada ya ndege hiyo kupata hitilafu na safari kuahirisha
Muktasari:
Ndege ya Kenya Airways (KQ), yenye namba KQ482 iliyokuwa isafiri kutoka Kenya kwenda Dar es Salaam nchini Tanzania imekwama Uwanja Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA)
Nairobi. Abiria kutoka nchi mbalimbali waliokuwa wakisafiri kwenda Dar es Salaam nchini Tanzania kwa ndege ya Kenya Airways (KQ), wamekwama katika uwanja Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) Kenya, baada ya ndege hiyo kupata hitilafu na safari kuahirishwa.
Abiria hao ambao walitakiwa kusafiri na ndege yenye namba KQ482 saa 2:30 asubuhi wakiwa kwenye harakati za kuhakikiwa tiketi zao asubuhi, ghafla walitaarifiwa kuwa ndege itachelewa kuondoka.
"Ndege ya KQ yenye namba 482 inayoelekea Dar es Salaam, itachelewa kuondoka. Tutawapa tena mrejesho ifikapo saa 10 kamili jioni," umesema uongozi wa KQ wakati ukiwatangazia wasafiri kupitia vipaza sauti vilivyopo uwanjani hapo.
Ilipofika saa 4 asubuhi uongozi huo uliwatangazia abiria wanaoelekea Dar es Salaam kuwa wanatakiwa kuhamia mlango namba 17 kwa kukutanishwa pamoja wakitokea mlango namba 16.
Baada ya kufika kwenye mlango namba 17, mmoja wa wasimamizi aliyejitambulisha kwa jina la Joseph Mwaniki amewaambia abiria wa ndege waliotakiwa kusafiri kuwa ina tatizo la kiufundi lakini uongozi unafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanaondoka saa mbili usiku.
Kauli iliwafanya baadhi ya abiria hao kuhamaki huku wengine wakisema hawakubali lazima wafike Dar es Salaam kwa kuwa wana shughuli nyingi za kufanya.
"Nimetoka Ndola (Zambia) natakiwa nifike Dar es Salaam leo asubuhi, ndiyo maana nilikata tiketi ya mapema. Mkuu fanya unavyoweza nifike Dar es Salaam mchana siyo usiku," amesikika mmoja wa abiria.
Abiria mwingine alisikika akisema: “Sitaki cha fidia wala kurudishiwa fedha ninachohitaji ni kufika Dar es Salaam kwa sababu kuna shughuli muhimu na watu wananisubiri otherwise (vinginevyo), sitowaelewa."