Prime
2025 waitakayo Watanzania

Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan ameungana na baadhi ya wananchi kutoa salamu za mwaka mpya ambao wameeleza wanayoyataka 2025, ikiwamo Tanzania isiyo na ajali, inayozingatiaji wa haki na kurekebisha kasoro zilizojitokeza 2024.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameungana na baadhi ya wananchi kutoa salamu za mwaka mpya ambao wameeleza wanayoyataka 2025, ikiwamo Tanzania isiyo na ajali, inayozingatiaji wa haki na kurekebisha kasoro zilizojitokeza 2024.
Kwa nyakati tofauti wakizungumza na Mwananchi, viongozi wa dini, siasa na wanataaluma wamezungumzia kuhusu kuboreshwa huduma za jamii, wakitaka uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kusimamiwa kwa haki ili kudumisha amani na kupata viongozi wanaokidhi matarajio ya wananchi.
Kwa upande wake, Rais Samia katika salamu za Mwaka Mpya kwa Watanzania alizozitoa Desemba 31, alisema moja ya changamoto zilizojitokeza mwaka 2024 ni jinamizi la ajali za barabarani.
“Takwimu za Jeshi la Polisi Tanzania zinaonyesha kati ya Januari hadi Desemba, 2024 nchi yetu ilishuhudia jumla ya ajali 1,735. Ajali 1,198 kati ya hizo, zilisababisha vifo vya ndugu zetu 1,715. Hii ni idadi kubwa sana.
“Ndugu zetu wengine 2,719 walijeruhiwa katika ajali za barabarani. Asilimia 97 ya ajali hizi zimetokana na makosa ya kibinadamu, kubwa kabisa ikiwa uzembe wa madereva, uendeshaji hatari na mwendo kasi ambayo kwa pamoja ni asilimia 73.7 ya ajali zote,” amesema na kuagiza:
“Niwatake Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi kuongeza mikakati ya kuzuia ajali zinazosababishwa na makosa ya uzembe.”
Rais Samia amesema 2025 ni mwaka maalumu kwa maendeleo ya kisiasa na kidemokrasia nchini kwa kuwa utafanyika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani na kwa upande wa Zanzibar, watachagua Rais, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani.
“Miongoni mwa maandalizi ya awali ya uchaguzi huo, ilikuwa ni kufanya mashauriano na wadau wote wa kisiasa yaliyopelekea kurekebishwa kwa sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya Vyama vya Siasa. Ni imani yetu kwamba sheria hizo zitatuongoza vyema katika kusimamia kwa ufanisi chaguzi zijazo.
“Nitoe rai kwa wananchi na wadau wote wa uchaguzi kuhakikisha tunaidumisha sifa ya nchi yetu ya kuwa na demokrasia iliyojengeka juu ya msingi wa uhuru na haki,” amesema.
Amesema nchi imeendelea kusimamia utekelezaji wa falsafa ya 4R inayohimiza maridhiano, ustahamilivu, mageuzi na kujenga upya nchi.
“Vilevile tunaendeleza uhuru wa habari unaoashiriwa na idadi kubwa ya vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza na uhuru wa kutoa maoni kupitia vyombo mbalimbali, hata uhuru wa kukusanyika na kujumuika,” amesema.
Katika utekelezaji wa mapendezo ya Tume ya Haki Jinai, amesema mwaka 2025 Serikali itakamilisha sera na kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali zinazohusiana na masuala ya haki jinai.
“Tutaendelea pia kutoa msaada wa kisheria kwa wahitaji. Hadi sasa, jumla ya wananchi 495,552 wameshanufaika na msaada wa kisheria wa kampeni ya Mama Samia Legal Aid chini ya Wizara ya Katiba na Sheria,” amesema.
Amesema Serikali itaendeleza mchakato wa kupata maoni ya wananchi ili kukamilisha uandishi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kuwezesha kuanza utekelezaji.
“Niwapongeze wananchi wote waliochangia katika mchakato huu, niwasihi tuendelee kutoa maoni yetu hadi mchakato utakapokamilika,” amesema.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali itapokea ripoti ya Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi itakayosaidia kuboresha wigo na mifumo ya kodi na kustawisha mazingira ya kibiashara nchini.
CCT, TEC
Wakati Rais Samia akisema hayo, Askofu Wolfgang Pisa, rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), pia amesema kwa kuwa 2025 ni mwaka wa uchaguzi mkuu, ni matamanio ya kanisa kuona kasoro za uchaguzi wa serikali za mitaa hazijirudii.
“Tunaomba makosa yasijirudie na mambo yafanyike kwa uwazi na ukweli na naomba Mungu, watu waendelee kumuogopa na kumcha Mungu,” amesema askofu huyo Jimbo la Lindi.
Hata hivyo, Rais Samia akizungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa, amesema ulifanyika kwa amani na utulivu.
“Katika uchaguzi ule (wa Novemba 27, 2024), kwa mara ya kwanza, wagombea ambao hawakuwa na washindani ilibidi wapate ridhaa ya wananchi kwa kupigiwa kura ya Ndiyo au Hapana. Hii imeondosha rasmi utaratibu wa kupita bila kupingwa ambayo ni hatua kubwa katika ujenzi wa demokrasia nchini,” amesema.
Askofu Pisa amesema mwaka 2025 unapaswa kuwa wa haki, utawala bora, wenye baraka, ukweli na mafanikio kwa watu binafsi, familia na Taifa, huku akitaka kila mmoja awajibike kutokana na eneo lake.
Kuhusu tathmini yake kwa mwaka 2024, amesema ulikuwa na mazuri hasa kukamilika kwa baadhi ya miradi ya huduma kwa wananchi, ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR) na hatimaye treni zinafanya safari na kukamilika kwa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere lililoanza kuzalisha nishati hiyo, mambo ambayo pia Rais Samia aliyagusia.
Suala la haki limezungumzia pia na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji Mosses Matonya akizungumzia Uchaguzi Mkuu wa 2025:
“Haki isimamiwe na uchaguzi uwe na utulivu kama ambavyo imekuwa siku zote, tuwe mfano kwenye demokrasia na amani," amesema.
Amesema wananchi pia wanapaswa kuhakiki majina kwenye daftari la kudumu la wapigakura.
"Uhakiki umeshaanza kila mwenye sifa ya kujiandikisha afanye hivyo ni matamanio yetu uchaguzi utakuwa huru na haki, ili tupate viongozi wanaopendwa na wananchi," amesema.
Kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, mchungaji huyo amesema maoni ya wananchi yafanyiwe kazi na malengo yatekelezwe kwa masilahi ya wote.
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa amesema mwaka 2024 ulikuwa mwaka wa amani na utulivu kwa upande mmoja, akitoa wito wa kujiandaa kuyakabili baadhi ya matukio yaliyoshuhudiwa kwa upande mwingine.
“Janga la ajali ya kuanguka ghorofa pale Kariakoo na ajali nyingi za barabarani zingeweza kuepukika endapo waliopewa dhamana wangesimamia vizuri,” amesema.
Amesema 2024 pia ulikuwa na matukio mengi ya ukatili hasa kwa watoto, yakihusishwa na imani za kishirikina.
“Inadhihirisha watu wengi bado wako katika giza. Hivyo neno la Mungu lihubiriwe zaidi pia kwa usahihi,” amesema.
Vyama vya siasa
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Khatibu ameisihi Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kutenda haki, akiwataka viongozi wa vyama vya siasa kuheshimu sheria za uchaguzi, mambo aliyosema ni nyenzo ya kufanyika kwa uchaguzi huru.
“2025 ni mwaka utakaokuwa na mambo mengi, nimefurahishwa na kauli ya Rais Samia aliyowahi kuitoa kuwa anataka uchaguzi huru na wa haki, ni vyema wasimamizi wote wa uchaguzi wazingatie sheria,” amesema.
Kuhusu wafanyakazi
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamhokya amesema mwaka 2025 wafanyakazi wajiepushe na vitendo vinavyokiuka uaminifu maeneo ya kazi.
“Kwa upande wa waajiri wafahamu jinsi wanavyowajali wafanyakazi wao na kuzisikiliza shida zao ndivyo wanavyoongeza morali katika utendaji kwa wafanyakazi wao,” amesema.
Ameiomba Serikali kuendelea kushirikiana na vyama vya wafanyakazi ili kutotoa nafasi ya kutoaminiana kwa pande zote mbili.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema matarajio ya madaktari ni kuuanza mwaka 2025, huku afya za wananchi zikiwa imara, mifumo ya utoaji huduma iliyoboreshwa na wananchi wakishiriki kwenye mikakati ya kupunguza vifo vinavyozuilika.
Amesema ni furaha yao kuona 2025 inaingia kukiwa na ajali kidogo, Watanzania wanaishi muda mrefu, wananchi wanamudu kugharimia afya zao na wajiunge na mifumo ya bima za afya.
Pia amesema mwaka 2024 zimeshuhudiwa ajali zilizopoteza uhai wa watu wengi.
“Huenda tukaenda kwenye uchaguzi mkuu utakaokuwa na ajenda mpya zinazoamsha ari ya kukabili maadui kama maradhi, ujinga na njaa,” amesema.
Kwa upande wao, wafanyabiashara wanatarajia matumizi ya nguvu wakati wa ukusanyaji wa kodi hayatakuwepo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabishara Taifa, Khamis Livembe amesema:
“Hatukuona matumizi makubwa ya nguvu baina ya mamlaka za kikodi na wafanyabiashara tunategemea 2025 hakutakuwa na matumizi yoyote ya nguvu kwenye ukusanyaji wa kodi, tunategemea ushirikiano zaidi baina ya Serikali na wafanyabiashara."
Pia kutatuliwa kwa changamoto za kikodi ili wawe na mazingira rafiki ya biashara.
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi amesema mwaka 2024 ulikuwa na changamoto na mafanikio katika utawala wa sheria.
Amesema marekebisho ya sheria yalifanyika kuendana na mahitaji ya sasa, zikiwemo zinazohusu haki za binadamu na masuala ya kiuchumi.
Katika usimamizi wa haki, amesema Mahakama zimeonyesha jitihada za kuongeza uwazi na ufanisi, hasa kwa kutumia teknolojia katika kushughulikia kesi kwa haraka.
Hata hivyo, amesema kulikuwa na changamoto, katika utekelezaji wa sheria, uhuru wa mahakama, uhuru wa kujieleza na ucheleweshwaji wa kesi.
Mwabukusi amependekeza kuwekwa mifumo madhubuti ya uwajibikaji kwa vyombo vya dola ili kupunguza ukiukwaji wa haki za binadamu.