15 wafariki kwa ajali Arusha, wengine wajeruhiwa

Wananchi wakiangalia magari yaliyopata ajali eneo la Kibaon (Ngaramtoni), barabara Kuu ya Arusha-Namanga leo.
Arusha. Watu 15 wakiwemo raia wa kigeni watatu, wamefariki dunia katika ajali iliyohusisha magari manne baada ya lori kudaiwa kufeli breki na kisha kugonga magari mengine madogo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Justine Masejo,amesema ajali hiyo imetokea leo Jumamosi, Februari 24,2024, saa 11 jioni eneo la Kibaoni (Ngaramtoni), kwenye Barabara Kuu ya Arusha-Namanga.
Amesema ajali hiyo ilihusisha magari madogo matatu ikiwemo basi dogo la abiria, gari dogo binafsi na basi la shule.
"Lori linaonekana lilifeli breki na kugonga magari mengine matatu--- mawili ni mabasi madogo na gari binafsi na kusababisha vifo vya watu 15 na majeruhi kadhaa ambao wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali za Mt Meru na Selian, ingawa wengine wako katika hali mbaya.
"Miongoni mwa waliofariki dunia ni mtoto mmoja, raia watatu wa kigeni, tunaendelea kufanya utambuzi wao kupitia hati zao za kusafiria na kuwasiliana na balozi zao," amesema.
Amesema lori lililosababisha ajali lilikuwa likitokea katika mpaka wa Namanga na lilikuwa limebeba mtambo maarufu kama kijiko na mengine yalikuwa yakitokea Arusha mjini kuelekea barabara ya Arusha-Namanga.
Endelea kufuatilia Mwananchi na mitandao yake kwa habari zais.