Zitto asema kusainiwa sheria za uchaguzi ni ushindi, dalili njema

Muktasari:
- Kiongozi mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amevitaka vyama vya siasa na wadau wanaodai katiba mpya kutopuuza kusainiwa kwa sheria za uchaguzi, akisema ni ushindi mdogo utakaowezesha kupatikana kwa ushindi mkubwa.
Dar es Salaam. Kiongozi mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kusainiwa kwa sheria za uchaguzi, ni ushindi mdogo kuelekea kupatikana kwa Katiba mpya ambayo wanaipigania.
Sheria zilizosainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ni pamoja na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani namba 1 ya mwaka 2024, Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi namba mbili ya mwaka 2024, Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa namba tatu ya mwaka 2024.
Akizungumza leo Jumatano, Aprili 3, 2024 katika mjadala wenye kichwa; Madai ya Katiba Mpya: Je Wananchi wanahitaji elimu ya miaka mitatu?’ ulioadaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Zitto amesema kusainiwa kwa sheria hizo kutawezesha kupata Bunge lenye nguvu kudai Katiba mpya.
“Kwenye vita kuna a war and a battle (vita kubwa na vita ndogo). Vita kubwa ni kuwa na Katiba mpya, lakini kuna battles nyingi hapa katikati za kutufikisha kwenye Katiba mpya,” amesema.
Amesema kupitia sheria hizo, wanapata uwezekano wa kupata Bunge litakaloweza kupitisha Sheria ya mchakato wa Katiba ambayo itaziungatia wananchi wanachokitaka.
“Ikifika mwaka 2025 hatujapata Katiba mpya, haina maana kwamba vita ya kupata katiba mpya itakuwa imekufa. Vita lazima iendelee, lakini iendelee ukiwa na bunge la aina gani?
“Kwa hiyo ni lazima wakati unapigana vita ndogo, lazima upigane vita ndogo, kuwezesha kuwa na Bunge lintakalokupatia Katiba unayotakiwa,” amesema.
Ametoa mfano wa kesi waliyofungua kupinga wagombea kupita bila kupingwa, akisema ni sehemu ya ushindi huo.
“Sheria ya uchaguzi imebadilishwa kwamba hakuna anayepita bila kupingwa, unapokwenda kwenye uchaguzi ukawa mgombea peke yako wananchi wanakupigia kura ya ndio au hapana, hapo umeshinda vita ndogo, huiachi hiyo vita unaishika unaendelea kupambana kupata vita kubwa.
“Mabadiliko yaliyofanywa katika miswada ya uchaguzi yanayowapa ahueni, hamtakiwi kuyadharau, mnatakiwa kuyakumbatia ili yawasaidie mnapoenda kupambana vita kubwa.
“Mnappokuwa na sheria ya uchaguzi inayowataka makamishna wa tume ya uchaguzi waombe wasailiwe ndio waendelee kusailiwa, haikuzuii kupata Katiba mpya,” amesema.
Kuhusu kucheleweshwa kwa mchakato huo, baada ya Serikali kusema inatoa miaka mitatu ya kutoa elimu ya Katiba, Zitto amesema kuna njia mbalimbali kulingana na tabia za wananchi wa nchi husika kulazimisha mchakato huo uendelee.
“Mashinikizo yanaweza kutumia njia mbalimbali lakini ni lazima kuwa wazi kwamba ni njia ipi tunayoitumia ya twende tukpate katiba inayokubalika na watu wote.
Hata hivyo, amesema kinachotakiwa kwa sasa ni kuendelea mchakato huo kuanzia pale ulipoishia.
“Kusiwe tena na kuitwa kwa Bunge la Katiba, isipokuwa timu ya wataalamu ipate rasimu, itakayoenda kupigiwa kura moja kwa moja na wananchi na ikishapitishwa, tunaweza kuamua kama ni simple majority asilimia 51 au theluthi mbili asilimia zaidi ya asilimia 67, basi Katiba hiyo iamuliwe kuwa ya Jamhuri ya Muungano,” amesema.
Awali, akizungumza katika mjadala huo, Katibu Mkuu wa zamani wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa ametaka kuheshimiwa kwa maoni ya wananchi yaliyotolewa wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipokusanya maoni mwaka 2012 na 2013.
“Kwa bahati nzuri nilizunguka kusikiliza maoni ya wananchi. Ndio maana ukiangalia maoni ya wananchi utaona walichosema. Kauli zao sio sheria, wala Katiba bali wanajua wanachohitaji,” amesema.
Amesema hatua ya Serikali kusogeza mbele mchakato huo ni kupuuza sauti za wananchi.
“Utaratibu sahihi ni kurejesha mchakato wa Katiba, kwa kurejesha Sheria ya mchakato wa Katiba. Wanasheria tunatofautiana kuhusu sheria hiyo, maana inasema sheria hiyo itakoma baada ya mchakato wote kwisha,” amesema.