Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Wimbo’ wa Bagamoyo umefungwa, kazi inaendelea

Muktasari:

  • Moja ya vipaumbele bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26  ya  Wizara ya Mipango na Uwekezaji ni kuzindua na kutangaza mradi wa Bagamoyo SEZ kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Dodoma. Wakati Serikali ikitaja vipaumbele katika bajeti yam waka wa fedha  2025/26 kwa Wizara ya Mipango na Uwekezaji, kitendawili cha ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo hatimaye kimefika mwisho.

Moja ya vipaumbele katika bajeti ya 2025/26 ni kuzindua na kutangaza mradi wa Bagamoyo SEZ kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa nia ya kuendeleza mradi ikiwamo ubia na sekta binafsi kwa kufuata mpango uliorejewa.

Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema katika bajeti inayoishia Juni, mwaka huu, Serikali imeendelea na kazi ya uendelezaji wa Kanda Maalumu ya kiuchumi ya Bagamoyo (BSEZ) kwa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita tatu.

Waziri amesema barabara hiyo inajengwa katika eneo lenye viwanda Zinga – Bagamoyo na utekelezaji wake mpaka sasa umefikia asilimia 70.

Waziri ametoa kauli hiyo wakati akisoma hotuba ya maombi ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2025/26 huku akiomba Bunge lipitishe Sh148.63 bilioni.

Kiasi hicho ni ongezeko la bajeti ukilinganisha na Sh121.33 bilioni zilizopitishwa kwenye mwaka wa fedha 2024/25 na baadaye kukawa na ongezeko la hadi kufikia Sh127.03 bilioni.

“Mheshimiwa spika, ofisi inaendelea kuratibu uendelezaji wa eneo maalumu la kiuchumi Bagamoyo, katika kipindi cha mwaka fedha 2024/25, Serikali imeendelea na uendelezaji wa Kanda Maalumu ya Kiuchumi ya Bagamoyo (BSEZ) kwa kuendelea na ujenzi wa barabara kwa kiwango,” amesema Profesa Mkumbo.

Mradi wa Bandari ya Bagamoyo na BSEZ,  ulianzishwa ili kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji katika Afrika Mashariki.

Mikataba ya kuanza ujenzi ilisainiwa Oktoba 2015 ikipangwa kukamilisha awamu ya kwanza 2017.

Hata hivyo, mradi huo umekumbwa na changamoto zilizochangia kusuasua kwake na Januari 2016, Serikali iliusitisha mradi huo kutokana na vipengele vya mkataba vilivyoelezwa kuwa na masharti magumu.

Rais wa wakati huo, hayati Dk John Magufuli alieleza kuwa, mkataba huo ulikuwa na vipengele visivyofaa kikiwamo cha sharti la kutojenga wala kuendeleza bandari yoyote kuanzia eneo la Tanga mpaka Mtwara.

Leo, Aprili 24, 2025  Waziri Mkumbo amesema ofisi yake inaendelea kuandaa andiko la mradi litakalotumika kupata mtaji wa kuendeleza eneo hilo hususani ujenzi wa majengo ya viwanda.

Akizungumzia vipaumbele vingine, waziri amesema Serikali itaendelea kuratibu maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano kwa kuzingatia dira mpya ya maendeleo ya 2050.

Nyingine ni kuratibu na kusimamia uwekezaji katika kanda maalumu za kiuchumi na kongani za viwanda ikiwamo usimamizi wa sekta binafsi.

Bajeti ya 2025/26 itawezesha pia kuanza maandalizi ya mpango wa maendeleo ya Taifa wa miaka mitano 2026/27 hadi 20231/32, kukusanya mapato ya Serikali yasiyo ya kikodi kutoka taasisi na mashirika ya umma ambako Ofisi ya Msajili wa Hazina imepangiwa kukusanya na kuchangia kwenye mfuko mkuu Sh1.56 trilioni kwenye kwenye vyanzo vya mapato yasiyo na kodi na kupitia gawio la Serikali.