Walimu wa Sayansi, Hisabati bado changamoto

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainab Katimba amesema hayo leo Jumatatu Aprili 22, 2024 alipojibu swali la mbunge wa viti maalumu, Esther Matiko

Dodoma. Serikali imesema kuna upungufu wa walimu wa Sayansi na Hisabati 39,610 sawa na asilimia 55.8.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainab Katimba amesema hayo leo Jumatatu Aprili 22, 2024 alipojibu swali la mbunge wa viti maalumu, Esther Matiko.

Matiko katika swali lake amehoji kuna upungufu wa walimu kiasi gani kwa shule za msingi na sekondari kwa masomo ya Sayansi na Hisabati.

Katimba amesema Serikali inatambua uwepo wa upungufu wa walimu wa masomo hayo katika shule za sekondari nchini.

“Kwa sasa mahitaji ya walimu wa Sayansi na Hisabati ni 71,027 waliopo ni walimu 31,417 na upungufu ni walimu 39,610 sawa na asilimia 55.8,” amesema Katimba.

Amesema kutokana na upungufu huo, Serikali imekuwa ikifanya jitihada kila mwaka kuajiri walimu wa masomo mbalimbali wakiwamo wa Sayansi na Hisabati.

Katimba  amesema katika kipindi cha mwaka 2020/21 hadi mwaka 2022/23, Serikali iliajiri walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati 10,853.

Amesema katika mwaka 2023/24, Serikali inatarajia kuajiri walimu 12,000 wakiwamo wa masomo hayo.

Katika swali la nyongeza, Matiko amesema Halimashauri ya Mji wa Tarime imekuwa na upungufu wa walimu wa Sayansi na Hisabati 83.

Amesema halmashauri hiyo ina walimu wa masomo hayo waliohakikiwa wanajitolea ni 44 ambao ni takribani asilimia 53.

“Kwa sababu Serikali inatarajia kuajiri walimu 12,000 kwa nini isitenge asilimia 50 ya ajira hizo kwa walimu wanaojitolea ili kutoa motisha kwa wanaojitolea, hivyo kupunguza upungufu wa walimu?” amehoji.

Amesema Shule ya Msingi ya Magufuli ambayo ni mahususi kwa watoto wenye ulemavu wa akili, kuona na viziwi ina upungufu wa walimu 13 ambao ni takribani asilimia 53.

Amehoji ni kwa nini Serikali isitoe kipaumbele kwa shule zote maalumu nchini kupeleka walimu wa kutosheleza mahitaji.

Akijibu maswali hayo, Katimba amesema wanayachukua maoni hayo na kuona namna ya kuyachakata wakishirikiana na wenzao wa utumishi ili kuona namna gani nzuri watazingatia miongozo na taratibu za kiutumishi.

Kuhusu kuajiri walimu kwa ajili ya wanafunzi wenye uhitaji maalumu, Katimba amesema katika kila ajira angalau asilimia tatu ni lazima wawe wanafundisha watoto wenye uhitaji maalumu.

Amesema mwaka 2023 waliajiriwa walimu kwa asilimia 2.7 kwa sababu kwa kawaida wanaojitokeza kuomba nafasi hizo hata asilimia tatu huwa hawafiki.

Katimba amesema watakaoomba wanaokidhi vigezo kwa mujibu wa taratibu wataajiriwa.