Wanafunzi watakaofanya vizuri masomo ya sayansi kupata ufadhili

Waziri wa Elimu Adolf Mkenda
Muktasari:
- Wanafunzi watakaofanya vizuri katika masomo ya kidato cha sita na Shahada ya pili katika masomo ya sayansi kupewa ufadhili wa kwenye Taasisi ya Teknolojia ya India visiwani Zanzibar.
Dar es Salaam. Wanafunzi watakaofanya vizuri katika masomo ya sayansi kupewa ufadhili wa masomo ya tehama kwenye taasisi ya teknolojia ya India (IIT).
Hayo yamesemwa leo Julai 7, 2023 na Waziri wa Elimu, Adolf Mkenda alipomkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Subrahmanyam Jaishankar amesema kuanzia Oktoba watachukua wanafunzi 50 wa Shahada ya kwanza na 25 wa Shahada ya pili na kuwapatia ufadhili wa masomo na mikopo.
Amesema wanafunzi watakaokuwa wamefanya vizuri katika masomo yao ya kidato cha sita wanatakiwa kuomba kusoma masomo ya tehama yatakayotolewa na IIT visiwani Zanzibar.
"Tungependa kuwapeleka wanafunzi wetu India lakini ni gharama kubwa na kwa sasa shahada hizo zitatolewa nchini kwa kuratibiwa na taasisi hiyo," amesema Mkenda.
Amesema elimu itakayotolewa na taasisi hiyo italingana na ile inayotolewa nchini India kwa kupitiwa na Seneta ya nchini humo ili kuepuka kuchakachua ubora wa elimu.
Mkenda amesema walishakubali vigezo ambavyo walivitaka na wapo tayari kupigania kutafuta pesa kwa ajili ya ufadhili wa masomo kwa wanafunzi hao.
"Tutaangalia na waziri wa fedha kuona tutaongeza fedha kiasi gani ili wanafunzi wa Tanzania ni namna gani wanaenda kusoma huko," amesema Mkenda.
Amesema India ni nchi ambayo imewekeza katika Elimu Sanyansi na Teknolojia hivyo ni muhimu kama nchi kujifunza kutoka kwao kwa ajili ya kuwa na nguvu ya kiuchumi kupitia teknolojia.
Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Mhandisi Dk Richard Masika amesema kituo cha umahili cha teknolojia kimekuwa ni lango la teknolojia kwa kutoa huduma za tehama kwa kasi nchini.
Amesema ushirikiano wao na India ni kwa ajili ya kuboresha ili teknolojia zake ziweze kuendana na maendeleo ya kitehama nchini ikiwepo katika huduma za kilimo, jeshi na utabibu kwa njia ya mtandao kwa kutumia tehama.
"Kwa sasa hivi kuna teknolojia mpya zimeingia ikiwepo mapinduzi ya viwanda kutoka taaluma hadi zana za kazi hivyo ujio wa taasisi ya teknolojia ya India itasaidia kupandisha ubora unaofanywa na taasisi yetu," amesema Dk Masika.