Wakulima wafundwa jinsi ya kuepuka mbegu feki

Washiriki wa mkutano wa mwaka wa Chama cha Sayansi ya Mazao Tanzania (Crosat) wakifuatilia mkutano huo jijini Dodoma hivi karibuni.
Muktasari:
- Mkurugenzi Mkuu wa Tosci, Patrick Ngediagi amesema ilikuwa ni vigumu kufahamu kama kuna mbegu feki
Dodoma. Wakati wakulima wakiendelea na msimu wa kilimo, Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (Tosci) imewataka kuhakikisha ubora wa mbegu wanazonunua kabla ya kuzitumia.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mkuu wa Tosci, Patrick Ngediagi katika mkutano wa mwaka wa Chama cha Sayansi ya Kilimo Mazao Tanzania (Crosat).
“Huko nyuma ilikuwa ni vigumu kufahamu kama kuna mbegu feki kwa sababu mkulima haoni tofauti. Lakini kwa sasa hivi tumeimarisha utaratibu wa udhibiti wa kutumia lebel za kieletroniki,” amesema.
Amesema kwa sasa kila mbegu inayouzwa nchini imewekewa lebo ya kieletroniki ambayo mkulima hugwangua na kuingiza namba anayoikuta ili taarifa zimwambie aina ya mbegu ni halali na imeidhinishwa na mamlaka za Serikali.
Kuhusu gharama kubwa ya mbegu bora inayolalamikiwa na baadhi ya wakulima, Ngediagi amesema inawezekana kweli mbegu ni ghali lakini mkulima akinunua mbegu kwa bei halali atapata mavuno na hivyo atapata faida katika uzalishaji wake.
“Tunawasihi wakulima kutumia mbegu bora haitagharimu badala yake mbegu bora italipa, watumie mbegu bora wakati wote waweze kupata mavuno na yapatikane katika hali ya tija, vinginevyo utatumia nguvu kubwa na eneo kubwa lakini unachokipata ni kidogo,”amesema.
Pia, amewataka wakulima kununua mbegu zinazofaa katika eneo husika ili kuepuka changamoto.
Rais wa Crosat, Profesa Kalunde Sibuka amesema chama hicho kinawaunganisha wadau wa mazao wakulima, mashirika ya wakulima, wahadhiri, watafiti, wakufunzi, maofisa ugani, vyombo vya udhibiti ubora wa kilimo mazao, wanafunzi na mashirika ya wanafunzi, taasisi zisizo za kiserikali, kampuni, wategenezahu, wasindikaji nawauzaji wa mazao mbalimbali na bidhaa.
Meneja wa Usimamizi na Majaribio ya Viatilifu katika Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viatilifu Tanzania, Profesa Eliningaya Kweka amesema kwa kushirikiana na chama hicho kutarahisisha upatikanaji wa habari ya afya ya mimea na hivyo kufanya wepesi wa kuwafikia wakulima.
“Tutapata habari kwa wakati stahiki na kuweza kudhibiti wakati stahili. Pia, katika pembejeo tunaposhirikiana tunaweza kufahamu sehemu yenye uhaba wa pembejeo,” amesema Profesa Kweka.