Mbegu za kisasa kunufaisha wakulima, Wajasiriamali

Njombe. Matokeo chanya ya uwekezaji wa zaidi ya Sh5 bilioni uliowekwa na mataifa ya Sweden na Denmark kwa wakulima umeanza kuonekana baada ya wakulima walioamua kutumia mbegu bora za kisasa kupata mavuno mengi.
Uwekezaji huo unaoratibiwa na Taasisi ya Kuboresha Mifumo ya Masoko ya Kilimo Tanzania AMDT kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (Tari) unazalisha mbegu za kisasa za alizeti na mikunde zinazotumia muda mfupi zaidi hadi kukomaa kwake.
Akielezea mafanikio ya matumizi ya mbegu hizo, Braunes Chengula mkulima mdogo wa zao la maharage anasema licha ya changamoto zilizopo ikiwemo hali ya hewa lakini bado hakati tamaa kwa sababu mbegu bora za maharage zina mavuno zaidi ya mbegi za asili.
Chengula ambaye ni mkazi wa kijiji cha Waging'ombe kilichopo wilaya ya Waging'ombe mkoani Njombe anasema kilimo cha uzalishaji maharage kwa kutumia mbegu za QDS one, kimemletea matokeo chanya akilinganisha na kilimo cha mbegu za asili alichokuwa akilima hapo zamani.
Anasema alianza kilimo cha mbegu bora kama zinavyoratibiwa na AMDT na kuzalishwa na kituo cha Tari mwaka 2017 na matokeo yake alianza kupata mavuno kwanzia debe 20, 30 hadi 40 ikiwa ni tofauti na mbegu za asili ambapo alkua akipata debe 4 hadi 5 kwa hekali moja.
"Ukanda huu tulikuwa hatujui mbegu hizi bora za QDS one, nilipewa elimu na Afisa Kilimo wa kituo cha Tari kilichopo Uyole Mbeya namna ya kulima kupanda na kutunza na bila hiyana nilianza kufanyia kazi.
"Mwaka wa kwanza nilipata debe 35 kwa hekali moja mwaka pili ulitokea ukame nilivuna debe 15 za mbegu baadaye wataalamu wa AMDT walinipa elimu zaidi na mwaka unaofatia nilipata debe 70" alisema Chengula ambaye ni mama wa watoto wanne anaowasimamia mwenyewe.
Akizungumzia mafanikio Chengula anasema toka aanze kilimo cha mbegu bora za maharage kimemfanya asomeshe watoto wake, ajenge nyumba yake na kufungua biashara zingine kijiji hapo.
"Kilimo cha mbegu bora kimenitoa kwenye nyumba ya tembe niliyokuwa nikiishi na sasa nimejenga nyumba ya matofali yenye paa," alisema Chengula.
Anasema kwa sasa maisha yanamuendea vizuri nyumbani hapo kwani ameshavuta bomba na anapata huduma ya maji, amenunua pikipiki na televisheni.
"Muitikio wa wakulima wenzangu ni mzuri na wengi wameanza kujiunga kutoka matumizi ya mbegu za asili na sasa wanatumia mbegu za Njano, 03, Mwaspenjere.
Anasema wakulima wenzake walikua wanashangaa akilima anapata debe zaidi ya 20, 30, hadi 40 wakati huo wenyewe wanapata debe 4, hadi 5.
Anasema amefikia hadi kufungua kikundi chake cha wakulima kinachoitwa (Tusongembele).
Naye Zuhura Mpinga, Mjasiriamali kutoka Njombe anasema aliamua kufungua mashine ya kukamua Alizeti akapokelewa na Taasisi ya AMDT kwa elimu zaidi.
Mpinga ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mayale, anasema ukamuaji wa mbegu bora za kisasa zilizofanyiwa utatiti na taasisi ya Tari ni rahisi zaidi na unatoa mafuta mengi tofauti na za asili.
"Mbegu bora kilo 100 zinatoa mafuta lita 40, mbegu za kienyeji inatoa lita 24 kwahiyo kuna utofauti mkubwa, hata wakulima wangu nawapa mbegu hizi wakalime halafu wanakuja kukamua hapa kwangu. Napata na faida za mashudu."