‘Waislamu endelezeni mema mliyoyafanya wakati wa Ramadhani’

Muktasari:
- Leo ni Jumatatu na ni Sikukuu ya Idd El-Fitr, ikiashiria kumalizika kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Dar es Salaam. Wakati Waislamu wakisherehekea Sikukuu ya Idd El-Fitr leo Jumatatu, Machi 31, 2025 waumini wa dini hiyo nchini Tanzania wameaswa kuendeleza mema waliyoyafanya katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Nasaha hizo zimetolewa leo Jumatatu wakati wa swala ya Idd katika msikiti wa Mtoro uliopo Kariakoo, jijini Dar es Salaam, na Sheikh Abdallah Al Mundhir ambaye amesisitiza kuendeleza mema kwa kuwa jambo hilo ndilo analotaka Mwenyezi Mungu.
"Saidieni wasiokuwa na uwezo, muwape wale ambao hawana. Endelezeni yale mliyoyafanya wakati wa Ramadhani. Kama uliweza kujizuia kuyafanya wakati huo, kwa nini usiweze wakati wa miezi ya kawaida?" amesema Sheikh Mundhir.
Amesema mfungo wa Ramadhani unaendana na Zakaatul-Fitr kwa ajili ya kuwasaidia wasio na uwezo ili wapate furaha na Mwenyezi Mungu atafanya wepesi.

Sheikh Mundhir, ambaye ni Jaji Mkuu wa Mashindano ya Kimataifa ya Qur'an, amesema hata katika suala la maadili halipaswi kukaliwa kimya, bali ni jukumu la kila mmoja wetu.
Kauli hiyo inaungwa mkono na muumini Hassan Hamis Hassan, aliyesema wenye familia na wasio na familia wanapaswa kuelezana bila aibu, ili kulinda na kukemea wale wote wanaokiuka maadili mema.
"Hata katika Uislamu suala hili limezungumziwa vizuri tu. Tunapaswa kuelezana ukweli. Inshallah, naamini kwa sababu tumetoka kwenye mfungo basi tutajirekebisha," amesema Hassan.
Haji Omar, amesema kufanya mambo mazuri, ikiwemo kuacha matusi, kusaidiana, na kuishi kwa upendo, ni suala lililoagizwa hata na Mwenyezi Mungu, hivyo haliepukiki.

"Ni kipindi tunachopaswa kuacha dhambi na kujikita kuendeleza yale tuliyotoka nayo wakati wa mfungo wa Mwezi Mtukufu. Tukirudi nyumbani tuelekeze na vijana wenzetu ambao wanaenda kinyume," amesema Omar.
Khadija Warid, amesema anashukuru wameiona sikukuu wakiwa na afya njema, hivyo jambo lililopo ni kusherehekea pamoja na wale wenye uhitaji.
"Sina kikubwa, lakini huwa napenda kusaidia wale wasiojiweza. Naamini nikitoa kidogo, mwenzangu naye kwingine atatoa kidogo. Ndondondo si chururu. Nasihi watu tupendane, tuombeane kheri," amesema Khadija.
Jamal amesema maisha ya Ramadhani ni chuo kinachopaswa watu wayaishi kwa yale waliyoyapata kujifunza huko.

"Jambo la msingi ni kuendeleza yale tulioishi. Tukiishi kwa upendo, tukaacha chuki, masengenyo, na fitina, basi maadili yatapatikana yenyewe kwa kuwa watu wataishi mazingira ya kumcha Mwenyezi Mungu," amesema.