Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

 Unajenga nyumba bila kibali Dar, fahamu yatakayokufika

Moja ya  nyumba ikiwa imewekwa alama ya kusimamishwa ujenzi katika Kata ya Zingiziwa, wilayani Ilala, mkoani Dar es Salaam, kwa madai ya kujengwa bila kuwa na kibali cha ujenzi. Picha na Nasra Abdallah

Muktasari:

  •  Gharama ya kibali cha ujenzi ni Sh200,000 kwa maeneo yasiyopimwa, kwa yaliyopimwa hutozwa kwa mita za mraba za eneo ulilolitumia kujenga.

Dar es Salaam. Kutokana na kukosa uelewa, baadhi ya wananchi wamekuwa wakijenga nyumba za makazi na biashara pasipo kutambua kuwa wanapaswa kupata vibali vya ujenzi.

Iwapo utakutwa umejenga nyumba bila kibali hicho katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, utapaswa kulipa faini ya asilimia 10 ya gharama ya ujenzi iliyotumika.

Mkuu wa Kanda ya Chanika, maarufu kanda namba saba ya Halmashauri ya Jiji hilo, Nickson Kyondo, amesema hayo Machi 19, 2024 katika mahojiano na Mwananchi Digital kuhusu nyumba zilizowekwa alama, wamiliki wakitakiwa kusimamisha ujenzi kutokana na kutokuwa na vibali vya ujenzi.

Kyondo amesema kwa utaratibu mtu anapojenga nyumba anapaswa kuwa na kibali, lakini hilo halizingatiwi,  akieleza ni kukosekana kwa elimu miongoni mwa wananchi.

“Baada ya kubaini hilo, tulitenga muda wa mwezi mmoja kwa ajili ya kutoa elimu kwa kushirikiana na wenyeviti wa Serikali za mitaa na watendaji  kata, kuhusu umuhimu wa mtu kukata kibali cha ujenzi kabla hajaanza kujenga,” amesema.

Kyando amefafanua: “Hii itamsaidia muhusika kuondokana na usumbufu, ikiwemo kusimamishiwa ujenzi au kutozwa faini, ambayo itakuwa ni asilimia 10 ya gharama alizozitumia katika ujenzi.”

Kwa nini alama?

Akieleza sababu ya kuweka alama za kusitisha ujenzi katika baadhi ya nyumba kwa sasa, amesema imetokana na halmashauri kugawa maeneo ya kiutawala katika kanda ikilenga kusogeza huduma karibu na wananchi.

Amesema ugawaji wa kanda umesaidia kuwafikia wananchi kwa urahisi, hivyo kuwabaini waliojenga bila vibali.

“Pia hii ni moja ya mikakati ya halmashauri katika kuongeza mapato kupitia vyanzo mbalimbali, utoaji vibali ni mojawapo ya eneo la ukusanyaji mapato,” amesema.

Kuhusu gharama anazopaswa kulipia mtu kupata kibali, Kyando amesema ni Sh200,000 kwa maeneo ambayo hayajapimwa na kwa yale yaliyopimwa mtu hutozwa kwa mita za mraba za eneo la ujenzi.

Amesema gharama hutofautiana kati ya nyumba za makazi, biashara, za ghorofa na zile za kawaida.

Kyando amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa vibali vya ujenzi, huku wakiwafikia hadi mafundi wanaowakuta eneo la ujenzi ili iwe rahisi kuwafikishia ujumbe waliowapa kazi.

“Tunashukuru tangu tumeanza kutoa elimu kuna mabadiliko, kwani awali tulikuwa tukipata watu wanne hadi watano kwa wiki wanaotaka vibali, lakini kwa sasa wanafika hadi 30, jambo lililosaidia pia kuongeza mapato kutoka Sh800,000 hadi Sh9 milioni kwa wiki,” amesema.

Unapataje kibali

Akizungumzia utaratibu wa kupata kibali cha ujenzi, Kyando amesema muhusika anapaswa kwenda kuchukua fomu Serikali ya mtaa ambako itasainiwa na kupigwa muhuri.

Amesema akitoka hapo ataenda ngazi ya kata na huko fomu hiyo itasainiwa na kupigwa muhuri, kisha ataipeleka ofisi ya kanda husika kwa ajili ya malipo na kupatiwa kibali cha ujenzi.

“Kazi hii haichukui zaidi ya saa moja hadi mbili,” amesema.

Walichosema wananchi

Wakizungumzia utaratibu huo, baadhi ya wananchi, akiwamo Hindu Jumanne, mkazi wa Chanika amekiri kutokuwa na uelewa kuhusu kupata vibali kabla ya kujenga.

Ametaka halmashauri kutoa elimu hiyo kwa njia mbalimbali ili kuwafikia watu wengi zaidi.

Steven Jamson, ameshauri mchakato wa kupata kibali urahisishwe ili watu wasione uvivu kwenda kuvifuatilia.

“Pia hawa watendaji wasisubiri mtu mpaka kajenga kafikia hatua ya kuweka paa au madirisha ndipo wanakuja kukagua, wawe wanapita mara kwa mara mtaani badala ya kukaa ofisini,” amesema.

Jamson amesema inaumiza pale mtu anapojinyima na kujenga hadi kufikia hatua ya kupaua ndipo anakuja kuambiwa asimamishe ujenzi.

Catherine Mwaisabula, amesema ni vema Serikali ikaangalia namna ya kupunguza gharama za vibali hasa kwa wananchi wa hali ya chini, ambao wengi wao huanza ujenzi wa chumba kimoja ili kupata mahali pa kulala.

“Sh200,000 kwake ni kubwa huenda angeongezea hata matofali kadhaa,” amesema.